YANGA kesho wanaanza bata rasmi la ubingwa kwenye Uwanja wa Mkapa. Ni zamu ya Dijei kuwaleta chini ya gwaride na saluti za aina yake watakazopigiwa na wachezaji wa Tabora United.
Liwake inyeshe, watakabidhiwa kombe lao la Ligi Kuu Bara na burudani zitakuwa za aina yake tangu asubuhi mpaka usiku.
Cha kushtua zaidi ni kwamba ndio mechi pekee msimu huu ambayo mashabiki wa jukwaa la mzunguko wataingia uwanjani kwa buku tu. Yaani Sh1000.
Burudani kadhaa za wasanii kama Harmonize, DJ Ally B,Chobs Twins zitakuwepo. Hata Foby naye atakuwepo kunogesha pati hilo la ubingwa wa 30 Yanga.
Mara baada ya mechi hiyo ambayo huenda ikashuhudia mabadiliko makubwa kikosini, Yanga itapewa Kombe kisha pati itaendelea likijumuisha mashabiki, wapenzi na mastaa wa timu hiyo sambamba na viongozi wa klabu kufurahia mafanikio ya msimu wa 2023-2024.
Hilo ni taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara na mechi dhidi ya Tabora itakuwa ni ya kukamilisha ratiba kwa timu hiyo ya Jangwani, lakini ikitaka kuboresha zaidi rekodi ilizonazo kwa msimu huu ikiwamo kwa mechi za nyumbani.
MAMBO YALIVYO
Tabora inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza, inajiuliza itakuwaje mbele ya wababe hao ambao haijapoteza mchezo wowote wa nyumbani kwa msimu huu, ilihali wageni hao hawajashinda mechi yoyote ya ugenini na wapo katika janga la kushuka daraja.
Timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam likiwa ni kati ya mapambano nane yanayopigwa leo kwenye ligi hiyo inayofikia tamati Jumanne ijayo.
Tabora inayoshika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi ikiwa naa na pointi 27, ikishinda michezo mitano, sare 12 na kupoteza 11, imekuwa na mwenendo mbaya msimu huu ndani ya ligi hiyo kwani kati ya michezo 13 iliyocheza ugenini imepoteza minane na kutoka sare mitano, haijashinda.
Katika michezo hiyo 13 ya ugenini ya ligi msimu huu, mbali na kutoshinda tu, pia imekuwa na wakati mgumu wa kufumania nyavu za wapinzani kwani hadi sasa imefunga mabao matano tu na kuruhusu 20.
Wakati Tabora ikikumbwa na changamoto hiyo, kwa upande wa Yanga hali ni tofauti kwani hadi sasa ikiwa imetangazwa kuwa mabingwa inashikilia rekodi ya kuwa timu pekee kati ya 16 msimu huu ambayo haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara ikicheza nyumbani.
Katika michezo 13 ambayo Yanga imecheza ikiwa mwenyeji imeshinda yote sawa na kukusanya jumla ya pointi 39 huku kikosi hicho chini ya Kocha Mkuu Muargentina, Miguel Gamondi kikifunga mabao 33 na kuruhusu matano pekee.
Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizi msimu huu, Tabora ilichapwa bao 1-0, mfungaji akiwa Stephane Aziz KI dakika ya 21, mechi iliyopigwa Desemba 23, mwaka jana kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mchezo wa pili kwao kukutana ulikuwa wa Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya robo fainali ambapo Tabora ilichapwa mabao 3-0, Mei Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI, Kennedy Musonda na Joseph Guede.
Hii ni mechi ambayo presha zaidi iko kwa Tabora United ambayo pointi 27 ilizonazo kwa sasa zinaweza kufikiwa na timu zilizopo chini yake kwa maana ya Mtibwa Sugar iliyoko mkiani na 21 sambamba na Geita Gold inayoshika nafasi ya 15 na pointi 25.
Yanga ambayo haina cha kupoteza baada ya kutetea taji lake,
inaingia katika mchezo huu ikiwa na matokeo mazuri ya hivi karibuni kwani mara ya mwisho kupoteza katika Ligi Kuu Bara ilikuwa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC, Machi 17, mwaka huu.
KAZI IPO HAPA!
Muhimili mkubwa wa Tabora United ni eneo la kati linaloundwa na Najim Mussa ambaye amekuwa katika kiwango bora na kuzitamanisha timu kadhaa za Ligi Kuu Bara ingawa haitokuwa rahisi kwake kupambana na viungo wa Yanga, Khalid Aucho, Mudathir Yahya na Salum Abukabar ‘Sure Boy’.
Tabora imekuwa haina safu bora ya ushambuliaji na kwa kuthibitisha hilo katika michezo 28 iliyocheza imefunga jumla ya mabao 18 tu ikiwa ni timu ya tatu inayoongoza kwa kufunga idadi ndogo nyuma ya Dodoma Jiji na Geita Gold zilizofunga 17.
Nyota anayeongoza kwa kufunga ndani ya kikosi hicho ni Eric Okutu aliyefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara hadi sasa huku ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza hapa nchini tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Hearts of Lions ya kwao Ghana.
Mastaa wengine waliofunga mabao mengi ni Mganda, Ben Nakibinge mwenye manne na raia wa DR Congo, Andy Bikoko aliyefunga matatu.
Wakati Tabora ikiwa na safu butu ya ushambuliaji, hali ni tofauti kwa upande wa Yanga kwani ndio inayoongoza kwa kufunga idadi kubwa ya mabao ikifikisha 64 ikifuatiwa na Azam FC na Simba ambazo kila moja imefunga 56.
AZIZ KI NA REKODI BARA
Mabao mawili ya nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki aliyoyafunga katika mchezo uliopita wa ushindi wa 4-0, dhidi ya Dodoma Jiji, yamemfanya kufikisha 17 katika Ligi Kuu Bara huku akibakisha moja tu kuivuka rekodi ya msimu uliopita ya Fiston Mayele na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.
Msimu uliopita aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga Mkongomani, Fiston Mayele ndiye aliyeibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 17 sawa na kiungo nyota wa Simba Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.
Endapo Aziz Ki atafunga katika mchezo huu, ataivuka rekodi ya nyota hao huku akijiwekea nafasi nzuri ya kuibuka na Tuzo ya Mfungaji Bora kutokana na ushindani wake na nyota wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye 16.
YANGA KUKABIDHIWA KOMBE
Mbali na mchezo huu kubeba ishu ya matokeo, lakini jambo litakaloteka hisia na kuvutia mashabiki wa Yanga ni kutokana na siku ya leo kukabidhiwa Kombe la Ligi Kuu Bara walilolitwaa kwa mara ya tatu mfululizo na la 30 kwa ujumla tangu mwaka 1965.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe alisema, licha ya burudani zitakazotolewa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya leo kabla ya mchezo huo, pia kutakuwa na helikopta maalumu iliyoandaliwa itakayolibeba kombe hilo.
“Helikopta ya gwaride la ubingwa itaanza safari yake saa nne asubuhi ikiwa imebeba kombe, itapita maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, tumempa rubani maelekezo kuna maeneo akifika pale Kariakoo aishushe chini kidogo ili kila mtu ashuhudie,” alisema.
MITAZAMO YA MAKOCHA
Kazi kubwa itakuwa kwa Kocha Mkuu wa Tabora United, Mrundi, Masoud Djuma tofauti na mwenzake Muargentina, Miguel Gamondi anayesaka heshima tu kwani hesabu za ubingwa zimeshatimia.
Djuma aliyeanza kukinoa kikosi hicho Aprili 23, mwaka huu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mfaransa, Denis Laurent Goavec, alisema ni mechi ngumu kwao japo wamejipanga vyema kukabiliana na washindani wao ili kupata pointi zote tatu.
“Tunashukuru hali ya kikosi ni nzuri kwa sababu tangu mchezo wetu wa mwisho na Ihefu hakuna mchezaji majeruhi, kikubwa ninachopambana nacho ni kutengeneza namna nzuri katika uzuiaji kwani tumekuwa na changamoto hiyo msimu huu,” amesema.
Kwa upande wa Gamondi ambaye ni msimu wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho na kukipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara amesema licha ya mafanikio waliyofikia ya kutetea taji lao lakini wanaendelea kupambana kuhakikisha kila mchezo wanapata matokeo chanya.
“Kuonyesha umakini tuliokuwa nao msimu huu utaona ni kwa jinsi gani hata mchezo wetu wa karibuni tulifanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji na unaona wote walitimiza kile ambacho tulikikusudia,” amekaririwa Gamondi baada ya mechi dhidi ya Dodoma Jiji.
Gamondi ameongeza kwamba hali ya wachezaji ni nzuri isipokuwa wanaendelea kuangalia utimamu wa beki wa kushoto wa timu hiyo, Nickson Kibabage aliyeumia wakati wa mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Ihefu. Nini utabiri wako kuhusiana na mechi za leo. Tuma kwenye namba hapo chini.