Dar es Salaam. Sekretarieti ya Maadili ya Uongozi wa Umma imesema wakurugenzi watendaji wa halmashauri (Ma-DED), watendaji wakuu wa taasisi na mameneja wanaongoza kwa kulalamikiwa na wananchi.
Imeelezwa kiwango cha kulalamikiwa kwa makundi hayo ni asilimia 100.
Hayo yamebainishwa jijini hapa jana wakati taasisi hiyo, ilipoeleza taarifa yake ya maadili kwa kipindi cha miaka mitano (2019/20 hadi 2023/24), kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari nchini.
“Wakurugenzi watendaji wa halmashauri (wilaya, miji, manispaa na majiji) wameendelea kuongoza kwa kulalamikiwa, wakifuatiwa na watendaji wakuu wa taasisi na mameneja. Malalamiko mengi yanatoka kwa wananchi,” alisema Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa taasisi hiyo, Omary Juma.
Juma alitoa mfano akisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita uwasilishaji malalamiko kwa mwezi umeongezeka kutoka 16 kwa mwaka 2021/22 hadi 18 kwa mwaka 2022/23 sawa na asilimia 13.
“Kuongezeka kwa wastani wa malalamiko kunatokana na utoaji elimu kwa umma uliosababisha uelewa wa wananchi kudai haki zao,” alisema.
Alisema malalamiko kwa kada hizo yaliyopokewa ni yanayohusu sheria, matumizi mabaya ya madaraka, rasilimali za umma na madai.
“Mathalani, malalamiko kwa wakurugenzi wakuu katika mashirika ya umma asilimia 200, mameneja katika mashirika ya umma kama vile Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) asilimia 114, wabunge asilimia 83, wakuu wa polisi wilaya asilimia 60,” alisema Omary
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka taasisi hiyo, Emma Gelani alisema licha ya Sheria ya Maadili kifungu cha 12, kuwataka viongozi wa umma kuwasilisha tamko pindi wanapopokea zawadi inayoanzia Sh200,000 wengi hawatekelezi.
“Tamko hilo la zawadi linapaswa kuwasilishwa kwa ofisa masuuli wa kiongozi husika katika kipindi cha siku saba tangu kupokea,” alisema Gelani.
Alisema sheria hiyo imekuwa ikipuuzwa, mathalani katika kipindi hicho walituma barua 800 kwenda kada mbalimbali kuomba kuwasilisha tamko la zawadi, lakini ni barua 12 pekee zilikubaliwa.
Alisema hata viongozi wachache waliowasilisha waliorodhesha zawadi zenye thamani ndogo ikijumuisha kalenda, daftari za kumbukumbu, picha za viongozi, kadi za sikukuu, mvinyo na maua, na wengine waliwasilisha zawadi za wafanyakazi bora.
“Hii inamaanisha baadhi ya maofisa masuuli hawafahamu zawadi zinazotakiwa kutolewa taarifa kwa kamishna kuwa ni zile zenye thamani ya zaidi ya Sh200,000,” alisema.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Sadick Yassin aliishauri taasisi hiyo kuondoa baadhi ya masharti magumu kwenye ofisi hiyo.
“Tatizo lenu mna sheria nyingi katika ofisi zenu, mara unachokiona humu na alichokisema kiache humuhumu wakati mwingine kunatengeneza woga wa watu kuja kueleza shida zao,” alisema.
Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema katika kufanya kazi zao kwa weledi bado wanategemea vyombo vya habari kupitia taarifa za uchunguzi wanazofanya.