Pemba. Kujengwa kwa kituo jumuishi cha utoaji wa haki za kimahakama Kisiwani Pemba, kutawaondolea usumbufu wananchi kufuata huduma ikiwamo ukataji rufaa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Kai Bashiru Mbarouk amesema hayo leo Mei 24, 2024 katika hafla ya utiaji saini mkataba kati ya Mahakama ya Tanzania na Kampuni ya M/S Deep Construction Ltd ya Morogoro kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho Pemba.
Amesema kwa muda mrefu wananchi wa Pemba wamekuwa wakiingia gharama kufuata huduma za kimahakama sehemu nyingine, hivyo ujenzi wa kituo hicho utawezesha kupatikana huduma zote zinazofanywa na Mahakama kuanzia ya Mwanzo hadi Rufaa.
“Mahakama ya Rufani ndiyo chombo cha mwisho cha utoaji wa haki ambacho kilikuwa hakipo kisiwani hapa, kwa hiyo hii ni hatua muhimu katika mazingira ya upatikanaji wa haki,” amesema.
Amesema kituo hicho kitaendeshwa kwa mifumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) itakayorahisisha utendaji na kuweka uwazi kwenye mashauri yatakayoendeshwa katika Mahakama zote shirikishi na kumpa nafasi mwananchi kufungua mashauri akiwa nyumbani.
Hata hivyo, amesema kuwa na jengo zuri ni jambo moja lakini kinachoangaliwa zaidi ni kuondoa changamoto za wananchi.
Aliwataka watendaji wa Mahakama kuhakikisha wanatafuta taaluma ya teknolojia ya habari itakayowasaidia katika utendaji wa kazi zao kutokana na huduma zitakozokuwepo kwenye Mahakama hiyo kutumika kwa mifumo ya kielektroniki.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema ujenzi wa kituo hicho unatokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kutoa fursa za kupatikana huduma jumuishi na haki kwa wananchi Kisiwani Pemba.
Amesema kituo hicho kitajengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB).
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amesema kuwepo kwa kituo hicho ni jambo la kihistoria kwa Zanzibar ikiwa ni katika kudumisha Muungano wa Tanzania.
Ujenzi wa kituo hicho unatarajia kuanza Mei mwaka huu na kukamilika Februari 2025 chini ya mkandarasi Kampuni ya M/s Deep Construction kwa gharama ya Sh9 bilioni.