KANDA ya Kati kutakuwa na vita ya kipekee. Ihefu itakuwa nyumbani uwanja wa Liti kuikaribisha Dodoma Jiji.
Katika mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni itakuwa na vita ya kikanda kwani Ihefu kwa sasa maskani yake yapo Singida jirani na Dodoma iliyo makao makuu ya nchi hivyo kila timu itakuwa ikisaka heshima na ubabe katika soka kwenye kanda hiyo ya kati.
Ukiachana na vita hiyo ya Kijiografia, mtanange huo utakuwa na mambo mengi ndani yake lakini kubwa zaidi ni kila timu kuwania nafasi ya juu tofauti na ilipo sasa kwenye msimamo.
Ihefu ipo nafasi ya saba na alama 33 huku Dodoma ikiwa ya 12 na pointi 30 wakati timu zote zikiwa zimecheza mechi 28.
Timu yeyote itakayoshinda mchezo huo itabadili nafasi kwenye msimamo. Ikishinda Ihefu itafikisha alama 36 na kupanda hadi nafasi ya tano lakini ushindi ukiwa kwa Dodoma, itatimiza alama 33 na kukaa nafasi ya nane, vivyo hivyo kwa sare itabadili kila namba katika chati lakini yote hayo yatategemea matokeo ya mechi nyingine saba zitakazopigwa leo.
Hata hivyo, zikiwa zimebaki mechi mbili kwa kila timu kutamatisha msimu, Ihefu inaonekana kuwa na ahueni mbele ya Dodoma Jiji kutokana na matokeo ya mechi tano zilizopita.
Ihefu imeshinda mbili, kutoa sare mbili na kupoteza moja katika mechi zake tano za ligi zilizopita huku Dodoma ikiambulia sare mbili na kupokea kichapo mara tatu.
Timu hizo mbili zimekutana mara tano kwenye Ligi Kuu hadi sasa na rekodi zinaonyesha Ihefu imeshinda mara tatu na Dodoma kushinda mara mbili huku katika mechi zote kukipatikana bao/mabao.
Rekodi hizo zinaonyesha huenda leo ikawa mechi yenye mabao pia kutokana na kila timu kuwa na uhitaji wa kufunga zaidi ili kusogea katika nafasi za juu kwenye msimamo sambamba na kuendeleza ubabe kwani timu hizo zinakaribiana kwenye uwiano wa kufunga mabao ambapo Dodoma imefunga 17 na Ihefu imepachika 24.
Safu ya ulinzi ya Dodoma imeruhusu mabao 29 hadi sasa kwenye ligi lakini leo itkutana na ushindani kutoka kwa washambuliaji wa Ihefu wakiongozwana Elvis Lupia, Marouf Tchakei ambao wamekuwa bora kwa kufunga huku kila mmoja akifunga zaidi ya mara tano.
Wakati huo huo, Ushindani mwingine huenda ukawa eneo la kati ambaopo Kelvin Nashoni na Duke Abuya wa Ihefu wana ubora unaorandana na Salmin Hoza na Rajabu Athuman wanaocheza eneo hilo kwa upande wa Dodoma.
Kocha Mkuu wa Ihefu, Mecky Maxime alisema utakuwa ni mchezo mgumu lakini lengo kuu ni kushinda.
“Hakuna timu nyepesi kwenye ligi. Dodoma ni timu nzuri na ina wachezaji wengi wenye uzoefu. Tupo tayari kupambana nao na lengo letu katika mechi zilizobaki ni ushindi tu,” alisema Maxime aliyewahi kuzifundisha Mtibwa na Kagera Sugar za Ligi Kuu.
Kocha Mkuu wa Dodoma, Mkenya Francis Baraza alikiri kuwa katika wakati mgumu lakini aliweka wazi kuwa alama tatu zinaweza kuipa uhai timu yake na kuirejesha katika nafasi nzuri kwenye ligi.
“Ukiangalia msimamo ulivyo kila pointi ina umuhimu hivyo lengo la kwanza ni kushinda dhidi ya Ihefu kwani tutapata alama tatu ambazo naamini zitatusogeza juu pia kurejesha morali kwa wachezaji,” alisema Baraza.
Mechi ya mwisho ya ligi, Ihefu itacheza nyumbani dhidi ya Mtibwa huku Dodoma itakuwa ugenini na Mashujaa.