Geita Gold, Singida ni vita ya kubaki Ligi Kuu

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Geita Gold na Singida Fountain Gate utakaopigwa leo kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida utakuwa ni vita ya kupambana kubaki katika ligi na kwa yeyote atakayeteleza atajiweka pabaya katika janga la kushuka daraja ikiwamo kucheza mchujo (play-off).

Kikosi cha Singida Fountain Gate

Timu hizo ambazo zimewahi kukutana mara tatu katika Ligi Kuu, zikiwamo mbili za msimu uliopita katika mazunguko wa kwanza zilitoka suluhu, kisha Singida ikaibua na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano. Msimu huu katika mzunguko wa kwanza Geita ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Geita Gold yenye maskani yake mjini Geita inaingia katika mchezo huo ikiwa nafasi ya 15 kwa pointi 25 na kama itashinda inaweza kupanda hadi nafasi ya 14 kama Tabora United iliyopo nafasi hiyo kwa pointi 27 itapoteza mechi dhidi ya Yanga ambazo zinakipiga leo pia.

Ikiwa Geita itamaliza nafasi ya 14, itapata nafasi ya kucheza mechi za mtoano ili kubakia katika ligi.

Kwa upande wa Singida iliyopo nafasi 11 kwa pointi zao 30, ikiwa itashinda mechi hii itajiweka katika mazingira mazuri ya kubaki katika ligi kwa msimu ujao ambapo inaweza kupanda hadi nafasi ya 10, tisa au  nane ikiwa JKT Tanzania, Kagera Sugar na Namungo mojawapo itapoteza mechi leo kwani tofauti ya pointi na JKT na Kagera ni moja wakati Namungo ni mbili.

Vilevile kama ikipoteza mechi hiyo kisha Mashujaa au Dodoma Jiji zikishinda zitaishusha hadi nafasi ya 12 au 13 na itakuwa imejiweka katika mazingira magumu ya kushuka zaidi ya hapo hadi 13 ambapo itatakiwa kucheza mechi za mtoano ili kubaki.

Singida FG ambayo imefunga mabao 25 na kufungwa 35 katika mechi 27 za ligi hadi sasa itatakiwa kuwa makini na mshambuliaji wa Geita, Valentino Mashaka ambaye hadi sasa amefunga mabao sita.

Geita inayoshika nafasi yanne kwa kuruhusu mabao mengi zaidi katika ligi hadi sasa itatakiwa kuwa makini na Habib Kyombo ambaye amefunga mabao tangu kuanza kwa msimu huu.

Matokeo ya Geita katika siku za hivi karibuni hayaridhishi kwani katika mechi 15 za mwisho imeshinda moja tu, kisha ikatoka sare mara sita na michezo ikapoteza michezo nane.

Kwa upande wa Singida katika mechi zao 15 zilizopita, tisa ilipoteza, sare nne na imeshinda miwili tu. Tofauti na Geita ambayo mara yamwisho kuonja ladha ya ushindi ilikuwa 09/03 mwaka huu mbele ya Dodoma Jiji, Singida mara yamwisho kushinda mchezo ilikuwa ni tarehe 04/05 dhidi ya hao hao Dodoma.

Ofisa habari wa Singida Fountain Gate, Jose Mkoko amesema mchezo huo ni muhimu kwao kwani wanahitaji alama tatu ili kujihakikishia kubaki Ligi Kuu, pia alizungumzia mabadiliko ya uwanja ambapo mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana badala ya CCM Kirumba kama ilivyopangwa hapo awali.

“Kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kutusapoti na wajue kwamba tunawaitaji sana hususani katika kipindi hiki,” amesema.

Kwa upande wa nahodha wa Geita Gold, Elias Maguri amesema: “Mchezo utakuwa mgumu, tupo nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu, hivyo tumejipanga kupambania pointi tatu.” 

Related Posts