DC James: Badala ya kupishana kusikiliza kero, tuzitatue

Iringa.  Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James amesema badala ya kufanya ziara za kusikiliza malalamiko, watendaji wa Serikali kwenye wilaya hiyo wana jukumu la kuhakikisha wanatoa huduma zinazomaliza kero hizo.

Amesema ukiona wananchi wanajazana uwanjani kutoa kero zao maana yake kuna baadhi ya watendaji hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.

Akizungumza kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa leo Mei +25,2024, James amesema anaanza kufanya ziara na ikiwa atakutana na kero nyingi kwa wananchi, maana yake watendaji wa eneo hilo hawatoshi.

“Kwa nini tufanye ziara za kusikiliza kero badala ya kuzitatua, tukitatua  changamoto zilizopo  hatutakutana na mikutano ya kusikiliza kero,” amesema na kuongeza;

“Ukiona wananchi wanajazana uwanjani kuleta kero maana yake mfumo wa utatuzi umekwama, kwa hiyo ongezeko hili ni  dalili kuwa mifumo yetu ya utendaji na utekelezaji wa majukumu ya Serikali sio mzuri kwa kiwango fulani,” amesema James.

Amewakumbusha watendaji wa Serikali kuwa sifa sio ziara ya kutatua kero za wananchi isipokuwa ni kumaliza changamoto zinazosababisha wananchi hao kulalamika.

“Kwa hiyo nataka kuwakumbusha watendaji wangu wa kata mpo hapa, nakuja kwenye ziara, nikiona kero nyingi kwenye kata maana yake ni ishara hutoshi, hufanyi wajibu wako vizuri,  hutoshi,” amesema na kuongeza;

“Sasa hivi imekuwa sifa kusikiliza kero za wananchi, sifa ni kumaliza changamoto zinazotengeneza kero. Sifa ni kuwa na utumishi uliotukuka, huduma bora, ziwafikie kwa wakati, uwezo wa kuwasikiliza wananchi vizuri.”

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa walitoa maoni kuhusu kauli hiyo ya mkuu wa wilaya wakidai kuwa imelenga kubadilisha mitazamo ya baadhi ya viongozi wanaotumia muda mwingi kusikiliza kero zao badala ya kuzitatua.

“Kweli, unakuta kero ni huduma mbovu za afya, badala ya kuja kunisikiliza nilalamikie huduma mbovu, boresheni huduma. Kero za barabara dawa yake ni kutengeneza barabara na sio kuja kusikiliza nikilalamika kuhusu barabara,” amesema Wikesi Ndendya, mkazi wa Isakalilo.

Naye Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema zaidi ya Sh2.4 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo.

Amesema jukumu lao kama madiwani ni kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo, ili kufikia viwango vinavyotakiwa na iweze kutatua changamoto za wananchi.

Related Posts