Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema miongozi mwa sababu za kuwepo kwa migogoro kwa nchi za Afrika ni kutozingatiwa kwa miongozo ya uwepo wa uchaguzi ulio huru na wa haki.
Kikwete ameyasema hayo leo Mei 25, 2024 jijini Dar es Salaam katika mjadala uliokuwa sehemu ya mkutano wa maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Aamani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC).
Amesema migogoro mingi ya ndani ya nchi za Afrika inahusiana na upungufu wa kiutawala.
“Inaweza kuwa demokrasia, ambapo inafikia watu wanakosa imani na demokrasia, kunakuwa na chaguzi ambazo hazijaratibiwa vizuri.”
“Aliyeshinda hatangazwi na aliyeshindwa anatangazwa kuwa mshindi. Yote ni kwa sababu ni upungufu wa kiongozi, kukosekana usawa, ubaguzi, ukabila na upendeleo,” amesema Kikwete.
Amesema watu wanapokosa haki zao huamua kuzipambania na ndipo inapozuka migogoro.
Kikwete aliyekuwa akitoa uzoefu wake katika utatuzi wa migogoro, amesema alishiriki kwenye utatuzi wa mzozo wa Kenya uliotokana na uchaguzi mwaka 2007 akishirikiana na viongozi wenzake, akiwamo Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan, Rais mstaafu hayati Benjamin Mkapa na Rais wa zamani wa Ghana, John Kuffor.
“Ilifika mahali walishindwa kuendelea, nikaalikwa kujiunga nao. Ilikuwa ni kutokana na matokeo ya uchaguzi, yakaleta shida,” amesema.
Amegusia pia mzozo wa uchaguzi uliotokea nchini Zimbabwe kati ya hayati Rais Robert Mugabe na aliyekuwa mpinzani wake, Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC.
“Wakati ule nilikuwa nina safari ya kwenda Arusha, nikaiahirisha, nikapaa kwenda Harare, nikajadiliana na Rais Mugabe kujua nini kinaendelea?
“Katika majadiliano, hapo ndipo tulimalizia kwa kukubaliana naye kwamba Serikali ianze kujadiliana na chama cha Tsvangirai,” amesema.
Amesema alimshauri Mugabe wamshirikishe Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki kusuluhisha.
“Niliitisha mkutano Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hapa Dar es Salaam. Katika mkutano ule nilimwambia Mugabe aeleze hali ilivyo. Baada ya hapo nilipomteua Rais Mbeki kuwa msuluhishi. Lakini suala lilitokana na uchaguzi ulivyoendeshwa,” amesema.
Viongozi wa Afrika wahusishwe
Kikwete aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 1995, amekumbushia kazi yake ya kwanza ya kwenda kwenye mkutano wa usuluhishi uliofanyika nchini Tunisia.
“Huko nilikutana na marais akiwamo Rais mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, Mobutu Seseseko, Rais wa Rwanda. Mjadala ulikuwa ni mgogoro wa Burundi,” amesema.
Amesema katika mkutano huo Jimmy Carter alikuwa akitoa mapendekezo ya utatuzi wa mgogoro huo.
“Tuliporudi, Mwalimu Nyerere akaema niko tayari kusaidia, lakini siwezi kufanya kazi kwa ushauri wa Jimmy Carter, wako wapi viongozi wa Afrika? Kama wakiniomba ndio nitalibeba,” amesema akimnukuu Nyerere.
Ameendelea kueleza kuwa, ndipo liliundwa jopo la viongozi likiongozwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na makamu wake akawa hayati Benjamin Mkapa ambao ndio walimtuma Mwalimu Nyerere kutatua mgogoro huo.
“Rais wangu (Mkapa) akaniagiza, Mwalimu anakwenda Burundi, nenda naye na mwalimu alisema kazi hiyo itatuchukua miaka mingi,” amesema.
Akizungumza katika mjadala huo, Rais msataafu wa Burundi na mjumbe wa baraza la wazee la Umoja wa Afrika, Domitien Ndayizeye amepongeza kazi zilizofanywa na baraza la amani na usalama kusuluhisha mgogoro wa nchi yake.
Amesema mchakato wa kutafuta amani ulianza mwaka 1998 na mazungumzo yaliyofanyika Arusha.
“Hali ya mambo kule Burundi ilikuwa mbaya, kwa kiwango ambacho kupata suluhisho ilikuwa ngumu. Ilibidi kuomba nchi za Afrika ambao walianza hatua ya pili, tukaenda Umoja wa Afrika.
“Burundi ilikuwa inakabiliwa na kukosekana kwa usalama, kuwepo kwa wakimbizi wengi. Katika uchaguzi wa 1993 na mauaji ya rais na mauaji ya kabila, hayo yalisababisha mapigano ya kisiasa na kiraia,” amesema.
Ndayizeye aliyekuwa Rais wa Burundi kuanzia mwaka 2003 hadi 2005 amesema awali rais aliyekuwa madarakani Poierre Buyoya alikataa mazungumzo.
“Sisi chama kilichopinduliwa (Frodebu) tulitaka tufanye mazungumzo na chama kilichopindua (Uprona), kwa sababu tuliamini jumuiya ya kimataifa na kikanda ingeweza kutusaidia.
“Haikuwa rahisi kulazimisha kufanyika, kwa hiyo sisi chama kilichokuwa kimeshinda lakini kikapinduliwa tukaungana na kukubali kuzungumza.”