Unguja. Wakazi wa Mtumwajeni, Mkoa wa Mjini Magharibi wamesema katika shehia hiyo hawapati huduma ya maji kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, bila kuelezwa tatizo na mamlaka inayohusika.
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti Mei 24, 2024 wamesema siyo tu kukosa huduma, bali maji yanapotoka huwa na uchafu jambo linalohatarisha afya zao.
Hata hivyo, Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) imesema kukosekana kwa huduma katika shehia hiyo kunatokana na ujenzi wa Barabara ya Amani Kwerekwe uliosababisha laini ya maji kukatwa.
Hata maeneo yanapotoka, yanakuwa na uchafu kiasia kwamba hayawezi kutumiwa katika matumizi ya kawaida.
Mkazi wa eneo hilo, Jamila Haji Pandu amesema hakuna maji lakini mamlaka imekaa kimya bila kutoa taarifa.
“Maji yanatoka na uchafu, tunaiomba Mamlaka ya Maji, watueleze tatizo ni nini kwa sababu tulishalalamika lakini bado hatujaona hatua zikichukuliwa,” amesema Jamila.
Zainab Abdalla amesema wananunua dumu moja la maji kwa Sh500.
Sheha wa Mtumwajeni, Rajabu Ally Ngauchwa amesema baadhi ya maeneo ya shehia hiyo hawapati maji na alishatoa taarifa kwa wahusika.
“Tunachohitaji ni taarifa ikiwa kuna shida yoyote watuambie kuliko kukaa kimya, watuambie maji hayapatikani kwa sababu gani na lini yatapatikana ili wananchi wajue kipindi cha kumalizika kwa shida hii,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Zawa, Amina Abdalla Daudi amesema ujenzi wa barabara utachukua muda mrefu na hawajui utakamilika lini, hivyo mamlaka inatafuta njia ya kuirejesha laini hiyo haraka.
“Tunatafuta sehemu mbadala ya kuwaungia maji wakati sisi tukiwa tunajipanga kuwawekea miundombinu mipya kwa lengo la kuondoa tatizo hilo,” amesema.
Amina amesema madai ya maji kutoka yakiwa na uchafu hayajaripotiwa kwao akiwataka wananchi wasipuuze wanapoona tatizo kama hilo kwa kuwa ni hatari kwa afya zao.
Amesema matukio ya maji kutoka yakiwa na uchafu yanakuwa mengi kutokana na mmomonyoko wa ardhi na baadhi ya mabomba yaliyochakaa kupasuka.
“Wananchi wanapoona maji yanatoka na uchafu wasipuuze kwa sababu hawajui maji hayo yamechanganyika na nini, hivyo watoe taarifa ifanyiwe kazi,” amesema.
Amesema shehia hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto za watu kujenga nyumba juu ya mabomba ya kupitishia maji.
Amina amesema mamlaka imeshirikiana na Manispaa inayohusika kutoa vibali vya ujenzi na kuwataka wananchi hao wahame.
Ameeleza baadhi yao wameondoka ila wengine wanadai hawana sehemu nyingine za kuishi bado wapo katika nyumba hizo.