Unguja. Chama Cha ACT Wazalendo kimesema kuna mikataba mingi mibovu inayoigharimu nchi, hivyo kikiingia madarakani mwakani kitahakikisha mikataba yote inafumuliwa na kuweka mipya.
Hayo yamebainishwa leo Mei 25, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho upande wa Zanzibar, Ismali Jussa wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa chama hicho na wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Huku akinukuu habari iliyochapishwa na magazeti ya Mwananchi na The Citizen Mei 24, 2024 kuhusu mchakato wa zabuni wa pamoja wa kuagiza mafuta chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati ulivyozua kizaazaa kuifanya Zanzibar ikose mafuta Kwa siku kadhaa.
Katika zabuni hiyo kati ya kampuni tano zilizoomba zabuni ya kuingiza mafuta, iliyopendekeza zabuni ya Dola za Marekani 272.7 ndio ilipewa na kuachwa zilizopendekeza zabuni ya Dola za Marekani 66.53.
Hata alipotafutwa Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Omar Ali Yussuf hakuthibitisha wala kukana madai hayo baada ya kupokea simu na kukaa kimya.
Jussa amesema “hatuwezi kuendelea na mambo ya namna hii kuumiza watu, sisi tunasema tutakaposhika Dola mwaka 2025 na inshallah tutashika, mikataba yote ya namna hii inapitiwa upya,” amesema Jussa.
Amewataka wanachama kutochoka kukumbuka dhamira ya chama hicho.
Naye Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Othman Masoud amesema kiongozi makini ni yule anayepigania masilahi ya umma na Taifa lake.
“Ukishajua unapokwenda unapunguza nusu ya mwendo wa safari, kwa hiyo ndugu zangu tunatakiwa kushikamana kupigania masilahi ya Zanzibar na kama kuna wakati Wazanzibari wameamka ni sasa, huko mbele tunapokwenda kuna giza zaidi,” amesema.
Amesema harakati za kuipigania Zanzibar kupata mamlaka yake zinapaswa kuanza sasa, kwani wakisubiri mbeleni kuna giza kubwa.
Amedai kuwa asilimia 54 ya mapato katika uchumi wa Zanzibar inatokana na vyanzo vya Muungano na iwapo ikitokea akaja kiongozi akavichukua, Zanzibar haitabaki na kitu kwani kwa sasa ipo kutegemea hisani.