Dodoma. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake ya CCM, (UWT), Mary Chatanda amelaani na kuchukizwa na kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kinachodaiwa kumdhalilisha mtumishi wa Serikali mwanamke wa mkoa huo.
Chatanda ameyasema hayo leo Jumamosi, Mei 25, 2024 jijini Dodoma wakati wa semina ya wabunge wa viti maalumu, manaibu waziri, mawaziri, makatibu wa jumuiya ya wazazi ngazi ya mkoa na wilaya.
Katika semina hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania bara, Abdurahman Kinana, Chatanda amesema amesitishwa sana na baadhi ya viongozi wanaoteuliwa kuwanyanyasa watendaji wanawake.
“Nimesikitishwa sana na ‘clip’ imezunguka kule Arusha, Longido jana haikuwa jambo jema wala sio zuri hata kidogo. Kama wewe ni kiongozi mkuu wa Serikali na umemuona mtendaji wako amekosea, huwezi kuwa na kauli na ulimi usiokuwa mzuri.”
“Ni vizuri ukakaa nao na kuzungumza nao. Una nafasi ya kukaa nao na kuwaambia. Kwa suala la udhalilishaji wa wanawake, mheshimiwa mwenyekiti hatutakubaliana nalo.”amesema.
Ameomba wanawake waheshimiwe na kwamba haiwezekani udhalilishaji wa namna hiyo.
Chatanda amesema kuwa clip hiyo tayari ameshamtumia Kinana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mara baada ya kuiona.
“Nimeona natapatapa nalo, sikupendezwa hata kidogo, Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti nimeona niliseme hili, niweze kupona nisipolisema naweza kufa. Naweza kupata presha bila sababu,”amesema.
Baadhi ya mitandao ya jamii, imemuonyesha pia Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), Dk Anna Henga akilaani kitendo hicho.
Dk Anna amesema mtumishi huyo mbali ya majukumu yake ni mama, ambaye kama binadamu mwingine anapaswa kulindwa na kutodhalilishwa utu wake.
“Maneno aliyokuwa anamwambia hayaendani na mtu ambaye unamuheshimu na kumuona kuwa ana thamani. Kwa hiyo tunakemea tabia kama hizi sio njema hasa kwa watumishi kama yeye mkuu wa mkoa lakini hata kwa jamii, ”amesema.
Amesema jamii inapaswa kuheshimu wasichana, wanawake na kila mmoja kwa sababu haki za wanawake ni haki za binadamu.
Amependekeza Makonda aombe radhi kwa Watanzania na aache tabia hiyo kwa sababu inatweza harakati za siku zote za kutetea haki za wanawake.
Katika clip hiyo inamuonyesha Makonda akijibizana na mtumishi huyo wakati akimuuliza kuhusiana na mradi (haujatajwa) kutokamilika kwa wakati kwa sababu ujenzi ulikuwa unahitaji utaalamu.
Baada ya kusema hivyo mtumishi huyo alikiri kuwa ni kweli ujenzi unahitaji utaalamu.
Lakini wakati akimweleza hivyo Makonda alimweleza mtumishi huyo afahamu kuwa anaongea na wananchi na kwamba haongei na mchumba wake.
“Usifanye kama vile umekutana na mtu unataka kumposa, mimi nina mke mzuri, ongea na wananchi,”alisema.
Akiendelea kuzungumza mtumishi huyo, alikatishwa na kelele ya Makonda akimtaka kuweka vizuri kipaza sauti chake.
“Hivi wewe unajua hawa ndio waliokuajiri mbona unawafanyia dharau sio kitchen party hii. Hawa unaongea nao ndio wanakatwa hela yao ya jasho, hawalali wanatafuta pesa ili ulipwe.”