Wauguzi na wakunga tisa wasimamisha kutoa huduma

Dodoma. Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) limewasimamisha kutoa huduma wauguzi na wakunga tisa huku wengine wanane wakipewa onyo, baada ya kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

Kwa mujibu wa tovuti ya baraza hilo, uamuzi huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa TNMC, Profesa Lilian Mselle, baada ya baraza hilo kukaa na kusikiliza tuhuma zinazowakabili kwa muda wa siku mbili.

Kwenye taarifa hiyo ya Mselle wauguzi na wakunga hao kutoka mikoa mitano nchini, walipewa adhabu hizo kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga na kanuni zake ya mwaka 2010.

Imefafanua kuwa  wauguzi na wakunga wawili ambao wametoka Kituo cha Afya Mikanjuni jijini Tanga mmoja  kutoa huduma kwa kipindi cha miaka miwili na mwingine mwaka mmoja kwa kosa la kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

Imeeleza pia  wauguzi wanne wa kituo cha Afya kibaoni Mjini Ifakara mkoani Morogoro, wamepewa adhabu ya onyo kwa kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

Kwenye taarifa hiyo Profesa Mselle amesema wauguzi wanne wa Hospitali ya Mji Geita mkoani Geita waliadhibiwa kutokana na makosa ya kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

Imesema taarifa hiyo kuwa  kati ya watumishi hao, mmoja amesimamishwa kutoa huduma kwa kipindi cha mwaka mmoja, wawili kwa miezi sita na mmoja alipewa onyo.

Katika  Kituo cha Afya Nyakumbu mkoani Geita, baraza hilo limesimamishwa watumishi wawili kwa muda wa miezi sita huku wengine  wawili wamepewa onyo kwa kushindwa kwa makosa hayohayo.

Pia wauguzi wawili kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walipewa adhabu ya onyo baada ya kubainika kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

“Adhabu zote zimetolewa chini ya Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya Mwaka 2010 kwa kuzingatia uzito wa kosa na ushiriki wa mtuhumiwa katika kosa husika,” imebainisha taarifa ya Profesa Mselle.

Januari 27, mwaka huu, TNMC, limemuachia huru muuguzi na mtaalamu wa idara ya usingizi na ganzi katika Kituo cha Afya cha Kabuku, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga baada ya kushindwa kumtia hatiani kwa tuhuma za kumtelekeza mjamzito.

Mbali na hilo, TNMC iliwasimamisha kutoa huduma ya uuguzi na ukunga kwa kipindi cha mwaka mmoja, wauguzi wawili wa Halmashauri ya Bunda, Mkoa wa Mara kwa makosa mawili ikiwemo kuharibu na kupoteza nyaraka zilizotumika kumuhudumia mgonjwa.

Related Posts