SERIKALI KUREJESHA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIKA NA MVUA-MAJALIWA

-Asisitiza mpango wa Serikali wa kukuza sekta ya kilimo

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kurejesha miundombinu yote ya barabara zilizoathiriwa na mvua zilizonyesha nchini.

Amesema hayo leo (Jumamosi Mei 25, 2024) alipokagua daraja lililopo katika kijiji cha Nambilanje ambalo limeharibika kutokana na mafuriko. Daraja hilo linaunganisha Wilaya za Liwale na Ruangwa.

“Kwa wakati huu ambao barabara nyingi zimekatika na kuharibiwa na mvua, Sio mkoa wa Lindi pekee, eneo hili TANROADS wameshafika, wameangalia hii hali na Waziri wa Ujenzi ameshatoa taarifa kwamba wanaendelea na uhakiki”

Amesema kuwa Serikali inasubiri taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kuisha kwa mvua ili itoe fedha na kutangaza zabuni za ujenzi za ukarabati na matengenezo ya maeneo yote yaliyoathiriwa.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa watanzania wote waliopata athari ya mvua hizo “Nawasihi muendelee kuwa watulivu na mjenge imani na Serikali yenu Mheshimiwa Rais katika mipango yake nina uhakika daraja litafanya kazi”.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amegawa pampu ishirini na mabomba yatakayotumika kumwagilia kwenye bustani za mbogamboga kwa wakazi wanaojishughulisha na kilimo hicho eneo la Nandagala wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wachangamkie fursa ya kilimo hicho kwani kilimo cha mbogamboga kinawezesha mkulima kupata kipato cha haraka “Tunataka eneo hili liwe kituo kikuu cha upatikanaji wa mazao ya mbogamboga”

Aidha amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati endelevu ya kukuza sekta ya kilimo ikiwemo mpango wa kutumia mabonde mbalimbali nchini ikiwemo yaliyo katika wilaya ya Ruangwa kukusanya maji ya mvua na kuyatumia katika kilimo na mifugo.

Related Posts