KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Aziz KI amesema kuhusu suala la kuongeza mkataba mpya ishu hiyo anaichia timu hiyo ambayo ameitumikia kwa msimu wa pili.
Aziz KI hadi sasa analingana mabao na Feisal Salum kwenye vita ya ufungaji katika Ligi Kuu Bara kila mmoja akiweka kambani mabao 18.
Akizungumza baada ya timu hiyo kukabidhiwa Kombe la Ligi Kuu Bara, kiungo huyo amesema ni kweli amepokea ofa kutoka nchi mbalimbali, lakini asilimia kubwa anaipa Yanga kusaini mkataba mpya.
Mchezaji ambaye msimu huu amekuwa moto katika kikosi hicho, mkataba wake wa miaka miwili uko ukingoni na awali ziliibuka taarifa kwamba alikuwa ameshasaini dili jipya, lakini hakukuwa na uthibitisho wowote kutoka pande hizo mbili.
Ndani ya wiki za karibuni kulizuka tetesi juu ya mchezaji huyo kuwa hajasaini na wengine wakisema amesaini mkataba mpya hivyo kauli hiyo inaonyesha bado hajapewa kandarasi mpya.
“Ni kweli nimezungumza na kupokea ofa timu nyingi, lakini kipaumbele nawapa Yanga. Nina furaha sana hapa tusubiri msimu uishe tutazungumza kuhusu mkataba,” amesema mchezaji huyo aliyetua Jangwani akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.