Mwanza. Wadau wa siasa wamependekeza kufutwa kwa nafasi za ubunge wa viti maalumu kwa kile kinachotajwa nafasi hizo zinachangia ukatili, hazileti dhana ya usawa wa kijinsia na kuigharimu Serikali zaidi ya Sh200 bilioni kila baada ya miaka mitano.
Pendekezo hilo limetolewa leo Jumamosi, Mei 25, 2024 katika mdahalo wa wazi wenye lengo la kujadili mchakato wa kupata Katiba mpya ya Tanzania ulioitishwa na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Hata hivyo, alipopigiwa simu kuzungumzia mapendekezo ya kufutwa nafasi za ubunge wa viti maalumu, Halima Mdee ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa nafasi hizo amesema: “Sina comment.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Katiba Tanzania, Dk Ananilea Nkya amesema nafasi za ubunge wa viti maalumu zilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (B) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na ziliwekwa kwa kipindi cha mpito kutokana na uwakilishi mdogo wa wanawake.
Hata hivyo, Dk Nkya amesema hali imebadilika tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, wanawake wanachangamkia nafasi hizo.
“Viti vya wanawake tulivipigania kweli kweli, lakini viliwekwa kwa transition (kwa muda) kwa sababu wakati ule miaka ya 1970 hadi 1980 utafiti ulivyoonesha wanawake walikuwa wanaogopa kwa sababu mfumo ulikuwa unawanyima kufanya kazi nje ya nyumbani,” amesema.
Hata hivyo amesema tangu kuanzishwa kwa vyama vingi nchi imeshuhudia wanawake wengi wanakuwa viongozi katika ngazi mbalimbali hali inayoashiria lengo la nafasi hizo za viti maalumu limetimia na hakuna haja ya kuendelea navyo.
Dk Nkya ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake na watoto, amesema uzoefu unaonesha kuna udhalilishaji kwa wanawake wanaogombea nafasi za viti maalumu ndani ya vyama vya siasa huku baadhi ya viongozi katika vyama hivyo wakivitumia kwa masilahi yao binafsi.
“Katika kuvipata inakuwa kwa mbinde wanavipata kwa njia ya unyanyasaji, ni wachache wanavipata kwa njia halali. Pia hawana fursa sawa na wabunge wa kuchaguliwa majimboni mfano nafasi ya Waziri Mkuu hawezi kuingia mbunge wa viti maalumu,” amesema Nkya.
Huku akitaja idadi ya wabunge wa viti maalumu bungeni kufikia 113 wanaoigharimu Serikali zaidi ya Sh200 bilioni kila miaka mitano ya uchaguzi, Dk Nkya amesema wabunge hao pamoja na kutowajibika kwa wananchi, pia wanaiingiza Serikali katika matumizi yasiyohitajika.
Amesema Jukwaa la Katiba linapendekeza kufutwa majimbo badala yake wawakilishi wa wananchi bungeni wapatikane kutoka kila wilaya kwa kuzingatia jinsia (mwanamke na mwanamume) na watu wenye ulemavu wapatiwe nafasi tano za uwakilishi bungeni.
Amesema endapo wilaya zitageuzwa kuwa majimbo, idadi ya wabunge itapungua kutoka wabunge 393 hadi angalau wabunge 276.
Kwa mujibu wa Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Deus Kibamba, mwarobaini wa changamoto ya viti maalumu bungeni utaondolewa kwa kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya.
Kibamba amesema ili kufikia hayo wanayoyasema, Katiba itakayoanzishwa inatakiwa kuja pia na mapendekezo ya kufumua na kupunguza mamlaka ya Rais ikiwamo ya kiuteuzi na kuyarejesha kwa wananchi.
Amesema ili hilo lifanikiwe, halihitaji utashi wa kisiasa bali kijamii.
“Kuna shida ya kubwa pale Rais mmoja mmoja anaporidhia kwamba ameongoza nchi kwa awamu moja, sasa anaingia awamu nyingine kuna shida gani nikiisaidia nchi yangu kupata Katiba mpya amekuwa akikumbana na upinzani mkubwa kutoka ndani ya chama chake,” amesema Kibamba.
Amesema anatamani siku moja atokee Rais atakayetangaza kwamba anaandaa kipindi cha mpito cha kufumua na kufanya mageuzi makubwa ya kikatiba, huenda itapatikana.
“Unapata Rais anaridhia kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya lakini haurejeshwi na ananyamaziwa tu, tupo kwenye kitendawili cha kutegua kwa sababu hao wanaomsaidia ndiyo hao hao wanaoona Katiba mpya itakayokuja itaondoa unono wa madaraka waliyonayo,” amesema Kibamba.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Ziwa, Steven Kitale amesema mchakato wa mabadiliko ukianza, ushughulikie upungufu wa kisheria ulipo kwenye taasisi likiwamo Bunge.
“Mapendekezo haya yatasaidia kujenga msingi imara ya Katiba inayozingatia matakwa ya wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu. Ni rai yetu kwa Serikali na viongozi wetu kuyazingatia ili kuwapunguzia wananchi mzigo na kurejesha uwajibikaji zaidi,” amesema Kitale.