DC Mpogolo asisitiza usimamizi wa maadili kwa wanafunzi

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka walimu ndani ya wilaya hiyo kusimamia suala la  maadili ya wanafunzi.

Amesema walimu wanapaswa kusimamia suala la maadili kuanzia mavazi wanayovaa na tabia za wanafunzi hao, ambapo wapo baadhi yao wanatembea na vitu vyenye nchi kali zikiwamo bisibisi.

Kauli hiy inakuja ikiwa ni wiki chache zimepita tangu Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu kutoa taarifa bungeni akinyooshea kidole suala la maadili kwa wanafunzi, akieleza kuwa Shule ya Ukombozi iliyopo Kata ya Saranga Jimboni kwake wanafunzi wanatumia dawa za kulevya, huku wengine zaidi ya 600 wakiwa wanalala darasani asubuhi kwa ulevi.

Mpogolo ameyasema hayo leo Mei 25,2024 alipokuwa akizungumza na walimu kwenye Kongamano la Jukwaa la Walimu Wazalendo Halmashauri ya Dar es Salaam.

“Baadhi ya shule za mijini watoto wanapenda kutembea na bisibisi na bangi, sasa alipo mwalimu mzalendo maadili ya watoto shuleni lazima yawe vizuri kwa sababu atawafundisha misingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, lakini pia utasaidia ufaulu kuongezeka, ukiongezeka ni sifa kwa Serikali,”amesema.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa, Mpogolo amesema kwa kuwa walimu ndio watapata fursa ya kusimamia uchaguzi huo, wanapaswa kusimamia kwa uhuru na haki na kutanguliza mbele uzalendo wa Taifa.

Kwa upande wake Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM, Frank Haule amewataka walimu hao kuhakikisha malengo ya chama hicho ya yanatimizwa hasa kushika dola.

Naye Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ilala, Dk Mussa Ally amesema jukumu la Walimu Wazalendo hao ambao wapo zaidi ya 600 ndani ya wilaya hiyo ni kuhakikisha chama kilichopewa mamlaka uimarikaji wake unakwenda vizuri, akisisitiza hakuna chama kisichohitaji ushindi.

“Kazi kubwa ya mwalimu mzalendo anayetimiza wajibu wake hasa kwenye Serikali iliyopewa wajibu wa kutekeleza Ilani, ni lazima kwenye eneo lake ahakikishe suala la uimarikaji wa chama kilichopewa mamlaka unakwenda vizuri,”amesema.

Related Posts