KMC sasa yakubali yaishe Bara

KIPIGO cha bao 1-0 ilichopewa na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa jana jijini hapa kutokana na bao la mapema la Saido Ntibazonkiza, limelifanya benchi la ufundi la KMC kukiri mambo yamewatibukia na sasa wanapambana kumaliza nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo.

KMC ilikuwa ikiwania nafasi ya nne ili ikate tiketi ya mechi za CAF kwa mara ya pili, ikichuana na Coastal Union iliyoinasa tiketi hiyo baada ya jana kutoka suluhu na JKT Tanzania, mipango imetibuka kwani hata ikimaliza mechi ya mwisho keshokutwa dhidi ya Coastal hao itafikisha pointi 39 tu.

Kocha Msaidizi wa KMC, John Matambala ameweka wazi mikakati iliyopo kwa upande wao ni kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo nafasi inayoviziwa pia na Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya sita kwa sasa ikiwa na pointi 34.

Pia timu za Namungo, Singida Fountain Gate, Dodoma Jiji na Ihefu zenye alama 33 zina uwezo wa kuzikifia pointi hizo za KMC iwapo nazo zitashinda mechi zao za kufungia msimu zitakazopigwa keshokutwa Jumanne na hilo ndilo ililoliamsha benchi la timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni.

Matambala amesema kikubwa kwa upande wao ni kuona namna gani wanapambana katika mchezo wa mwisho ili kumaliza nafasi ya tano ambayo ndio malengo ambayo yamebakia baada ya Coastal Union kujihakikishia uhakika wa kumaliza nafasi ya nne.

“Timu yetu ni nzuri na inacheza vizuri mpaka hapa niwapongeze wachezaji wangu kwa upambanaji wao lakini malengo ilikuwa ni kumaliza nafasi ya nne ila baada ya kupotea sasa inatakiwa tumalize wa tano,” amesema Matambala.

Ameweka wazi ligi ya msimu huu ilikuwa mgumu kwani kila timu ilisajili wachezaji wazuri ndio maana unaona mpaka inabaki mchezo mmoja dado timu nyingi zinapambania kubaki katika Ligi na kutumia fursa hiyo kuwaomba mashabiki wa KMC FC kuendelea kuiunga mkono timu yao na ameongeza watawafurahisha kuhakikisha wanashinda mchezo wa mwisho na kumaliza nafasi ya tano.

Related Posts