KATIKA msafara wa Yanga, bodaboda wamepata fursa ya kupiga pesa, kutoka kwa mashabiki ambao wamechoka kutembea na kuamua kutumia usafiri huo.
Mwanaspoti lipo kwenye msafara huo, limeshuhudia baadhi ya mashabiki wakikubaliana bei na bodaboda ambao wamebeba abiria mmoja na wengine hawana watu kabisa.
Kutokana na msafara kuwa na magari mengi yanayotembea taratibu,kumekuwa na foleni, inayosababisha bei kuchangamka.
Pamoja na bei wanazotajiwa haionekani kuwasumbua mashabiki waliojawa na shangwe ya kusherehekea ubingwa wa msimu huu, Ukiwa wa mara 30 tangu Yanga ianze kucheza Ligi Kuu.
Bodaboda hao kutoka Keko hadi Jangwani, wanataja Sh 7000-10000 na bado wanapata wateja.
Mbali na hao wanaobebwa kwenye bodaboda, wapo wanawake ambao wanaonekana na watoto wadogo wanaowavuta mikono kuendelea na msafara huo.
Yanga inatembeza Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliyotwaa kwa mara ya tatu mfululizo na la 30 kwa klabu hiyo tangu mwaka 1965 ikiwa ndio vinara wa ligi hiyo ikifuatiwa na Simba yenye mataji 22 na Mtibwa iliyoshuka daraja kwa sasa, ikiwa ya tatu na mataji mawili iliyotwaa mwaka 1999 na 2000.