Maloto alivyochambua urafiki, uhasimu wa Kikwete na Lowassa kupitia kitabu

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi mitatu tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa afariki dunia, mwandishi nguli wa masuala ya kisiasa amechapisha kitabu cha urafiki na ukaribu wa mwanasiasa huyo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 baada ya kuugua magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Mwili wake, ulizikwa Kijijini kwake Ngarash, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.

Aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Waziri Mkuu Desemba 30, 2005, lakini alijiuzulu nafasi hiyo Februari 7, 2008 baada ya kamati maalumu iliyoundwa na Bunge kuchunguza utata wa mkataba wa Richmond kuelekeza lawama kwake na Wiziara ya Nishati na Madini.

Kitabu hicho chenye jina la “Kikwete Lowassa; Urafiki, Ndoa Yao ya Kisiasa, Uadui” tayari kimeshaingizwa sokoni, kikieleza urafiki wa wanasiasa hao hadi hali ya kutoelewana.

Akizungumza leo Jumapili, Mei 26, 2024 na Mwananchi Digital, mwandishi wa kitabu hicho, Luqman Maloto, amesema Kikwete na Lowassa ni wahusiku muhimu katika ujenzi wa aina ya siasa zilizopo Tanzania kwa sasa.

“Upacha wao waliotengeneza tangu uchaguzi Mkuu 1995, kisha wakaambatana bega kwa bega kuelekea Uchaguzi Mkuu 2005. Athari waliyoitengeneza kwenye siasa za Tanzania hadi Uchaguzi Mkuu 2015, inawafanya kuwa wahusika muhimu ambao wanahitaji kuandikwa na kusimuliwa.

“Vilevile uhusiano (upacha wao) wao, ni somo la kizazi kipya cha siasa na wasomi wa sayansi ya siasa,” amesema. 

Suala la kudorora kwa uhusiano baina yao lililozua mjadala mkubwa katika msiba wa Lowassa, pia limejadiliwa katika kitabu hicho, ambapo Maloto anaeleza ulianza kuingia dosari tangu mwanasiasa huyo akiwa waziri mkuu.

“Kutafsiri uhusiano wa Kikwete na Lowassa ulivyokuwa nyakati za mwisho za uhai wa Lowassa ni kukosea pointi. Safari ya kudorora uhusiano wa Kikwete na Lowassa, ilianza tangu Lowassa akiwa Waziri Mkuu na Kikwete Rais, halafu Lowassa akajiuzulu uwaziri mkuu.

“Vita ya urais mwaka 2015, ikadhihirisha kila kitu kwamba marafiki wawili, waliokuwa na ushirikiano mkubwa kisiasa, hawakuwa wakiiva tena kwenye chungu kimoja.

“Hili ni eneo ambalo kitabu cha ‘Kikwete Lowassa’, limeandikwa, kufafanuliwa na kuchambuliwa kwa kina.”

Akifafanua sababu za kudorora kwa uhusiano huo, Maloto ametaja wivu, tamaa, hofu, haraka, majungu na kutoshughulikia maneno ya uchonganishi mapema.

“Hayo ukiyaweka kwenye kapu moja, unaweza kuwa karibu na jibu la kwa nini uhusiani wa Lowassa na Kikwete ambao ulikuwa mzuri mno awali, baadaye ulidorora kabisa,” amesema.

Maloto amesema kuna mambo mengi ya kipekee kuhusu Kikwete na Lowassa yanayofanya kitabu cha “Kikwete Lowassa” kiwe somo muhimu kwenye siasa za nchi.

“Kwanza, ndoa yao ya kisiasa hayakuwa na nyaraka walizoandikishiana. Uhusiano wao uliundwa kwa kuaminiana bila kujua ungefika wakati wakageukana.

“Pili, kitabu kimechambua ndoa ya kisiasa ya Kikwete na Lowassa, dhidi ya ndoa nyingine maarufu duniani, Gordon Brown na Tony Blair, Uingereza; Thabo Mbeki na Jacob Zuma, Afrika Kusini; Uhuru Kenyatta na William Ruto, Kenya; na nyingine,” amesema.

Amegusia nadharia nyingi kuhusu kudorora kwa uhusiano baina ya wanasiasa hao na jinsi kitabu hicho kinavyozifananisha.

“Uhusiano wa Kikwete na Lowassa, ulikuwa lazima uvunjike kwa sababu ya asili ya kitu kilichowaunganisha.

“Mamlaka si kitu ambacho watu wanaweza kuchangia. Mamlaka ni kitu ambacho hutengeneza wivu ajabu, ndiyo sababu wote waliofunga pingu za kisiasa, waliishia kugombana.

 “Ndivyo ilivyokuwa lazima kwa Kikwete na Lowassa wagombane, maana mamlaka huwa na wivu mkubwa mno,” amesema.

Related Posts