Dar es Salaam. Ili kudhibiti kuenea kwa Ukimwi Tanzania wadau wa maendeleo na ustawi wa jamii, wamezindua kampeni ya kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia jitihada za Serikali katika kupambana na ugonjwa huo.
Hatua hiyo inakuja wakati Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi (THIS) ya mwaka 2022/2023, unaonyesha Tanzania ina watu milioni 1.5 wanaoishi na VVU, maambukizi mapya ya mwaka yamepungua kwa asilimia 16.7 kutoka 72,000 2016/17 hadi 60,000 2022/23), huku maambukizi yakiongezeka maradufu miongoni mwa wasichana wenye umri wa miaka 15-24.
Hivyo wadau hao wanazikusanya fedha kupitia kampeni ya Kilimanjaro Challenge ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ikiwa ni shirika la ushirikiano wa hisani linaloleta pamoja Serikali kupitia Tume yaTaifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na GGML ili kuhamasisha juhudi za kupambana na ugonjwa huo.
Katika kutekeleza hilo, kupitia kampeni ya GGM Kili Challenge 2024 ambayo inahusisha kupanda na kuzunguka Mlima Kilimanjaro kila mwaka fedha hizo zitakusanywa, huku lengo ikiwa ni kupata kiasi cha Dola za Marekani milioni 1 ambazo ni zaidi ya Sh 2.6 bilioni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Balozi wa Marekani nchini, Tanzania, Michael Battle amesema ahadi za michango zinatarajiwa kukamilishwa ifikapo katikati ya Julai 2024.
“Kama wengi wenu mnavyofahamu, Mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi, unaojulikana kama PEPFAR, umekuwa nguzo katika mapambano ya kimataifa dhidi ya Ukimwi kwa zaidi ya miaka 20, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003,” amesema.
Amesema Pepfar imewekeza nchini, ikiunga mkono miradi mbalimbali ya kudhibiti janga hili na huku ikiwa imepiga hatua, ambapo zaidi ya watu milioni 1.5 wanapata matibabu ya kuokoa maisha kupitia msaada.
Aidha, wamepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyohusiana na Ukimwi na idadi ya maambukizi mapya.
“Hata hivyo, sasa tupo katika hatua ambapo uendelevu ni muhimu kwa sababu Pepfar haikuwahi kuwa suluhisho la kudumu; ilibuniwa kukidhi hitaji la dharura, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti janga la Ukimwi, viwango vya maambukizi mapya vimepungua kwa kiasi kikubwa, pamoja na vifo vinavyohusiana na Ukimwi,” amesema.
Aidha Balozi Battle amezisifu GGML na TACAIDS kwa kushirikiana kwenye kampeni kama hii inayosaidia Serikali kupambana na kuenea kwa Ukimwi nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duan Archery amesema michango inathamani na itasaidia kufikia lengo letu la ‘kufikia sifuri’, ambalo ni kutokuwepo kwa maambukizi mapya, kutokuwepo kwa ubaguzi, na kutokuwepo kwa vifo vinavyohusiana na Ukimwi.
Pia,Makamu wa rais wa AngloGold Ashanti wa Masuala ya Uendelevu na Mambo ya Ubia (Afrika), Simon Shayo amesema vikundi mbalimbali vimefaidika na kampeni hiyo, ikiwa ni pamoja na watoto wa Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma, ambacho pia kinawatunza watoto wengine walio katika mazingira magumu.
“Kundi la kwanza la watoto waliokulia katika kituo hicho sasa wanasoma vyuoni, wakiwemo wawili wanaosoma digrii za udaktari,” amebainisha Shayo.
Hata hivyo, akizungumza katika hafla hiyo, Jumanne Isango akimwakilisha Dk Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, amesema fedha zote zitakazokusanywa zinagawanywa kwa mashirika yanayohusiana na Ukimwi akisema vita inahitaji msaada zaidi wa ndani, hasa wakati michango ya kigeni inapopungua.