Wadau wa elimu wataja mbinu kukabiliana na tatizo la ajira nchini

Arusha. Elimu ya ubunifu imetajwa kuwa suluhisho la kukabiliana na tatizo la ajira linalowakumba vijana wengi wanaohitimu masomo hapa nchini.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Mei 26, 2024 na wadau wa elimu kwenye uzinduzi wa kampeni ya uchangiaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya jamii inayotarajiwa kujengwa Ngaramtoni mkoani Arusha.

Kampeni hiyo inayoendeshwa na shirika la kusaidia watoto wa kike wanaotoka kwenye familia duni  inaitwa The Girls Foundation Tanzania,  yenye lengo la kukusanya Sh112 milioni kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa vitabu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa TGFT, Estahappy Mariki amesema changamoto ya ajira nchini imesababishwa na vijana wengi wasomi kuelekeza akili zao katika kutafuta nafasi ya kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo yao.

“Katika kukabiliana na hili, wadau wa elimu tuanze kuwatengenezea wanafunzi wetu kufikiria matatizo yaliyopo kwenye jamii, nao watafute ubunifu wa kukabiliana nayo, hii itazalisha fursa za kujiajiri wao baadaye na kuajiri wengine,” amesema Estahappy.

Amesema kwa kushirikiana na Shirika la Twende, wametumia mbinu ya kuwajengea uwezo wa ubunifu vijana wanaowalea na wenye uelekeo wa mafanikio kwa kiasi kikubwa.

“Hadi sasa tuna wanafunzi 86 wanaofadhiliwa na shirika letu kwa miaka 10 ya masomo yao ngazi mbalimbali za elimu, lakini wameweza kutengeneza bunifu za changamoto wanazoziona kwenye jamii ikiwamo mashine ya kukatakata mboga za majani, mashine ya kuparua samaki, kupukuchua mahindi na inayochanganya mbolea ya mboji,” amesema Estahappy.

Amesema kwa ngazi zao, wanafunzi hao wameona hizo ndiyo changamoto kwenye familia wanazoishi na kadri wanavyoendelea kukua ndivyo wanaongeza maboresho zaidi ambayo hata baadaye wakihitimu wanaweza kupata fursa ya kuanzisha kampuni zao kwa mikopo ya taasisi za kibenki.

Akizungumzia maktaba hiyo wanayotarajia kuijenga, Estahappy amesema wameamua kuwa na jengo lenye rasilimali hizo ili kuwapa fursa wanafunzi wanaowalea na walioko kwenye jamii.

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu la GLAMI, Anande Nnko amesema ipo siri kubwa kwenye usomaji wa vitabu katika malezi na makuzi ya mtoto.

“Wazazi wa siku hizi wameachia watoto wao walelewe na ulimwengu na teknolojia yake, ndio maana kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili, hivyo niwatake wazazi wenzangu kuwekeza nguvu kubwa katika kuhamasisha watoto wetu wasome vitabu, hiyo ndiyo njia pekee ya kumkomboa na dunia,” amesema.

Mmoja wa wanafunzi hao, Janeth Mduma amesema maktaba hiyo itawasaidia kujisomea wanapotoka shule.

Pia, amesema vitabu vya stadi za maisha na kazi watakavyokuwa wanasoma wakiwa likizo vitawajengea bunifu mbalimbali kama ambazo wamekwisha kutengeneza.

“Naomba jamii ihamasike kuchangia maktaba hii kwa kuwa haitakuwa kwa manufaa yetu na wasichana wa kituo pekee, bali uongozi umesema utakuwa wazi kwa ajili ya watu wote wanaotuzunguka,” amesema Janeth.

Related Posts