Bukoba. Wakati Chama cha Drmokrasia na Maendeleo (Chadema) kikimtangaza Ezekia Wenje kuwa mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, mshindani wake wa karibu, John Pambalu ametoweka ukumbini wakati uchaguzi ukiendelea, huku akikataa kueleza sababu za hatua hiyo.
Uchaguzi huo wa kanda uliofanyika juzi hadi usiku, ulihusisha mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa kanda na viongozi mabaraza ya chama ngazi ya kanda.
Nafasi iliyokuwa na ushindani mkali ni mwenyekiti iliyokuwa inawaniwa na Wenje na Pambalu. Hata hivyo, habari zilizopatikana zilieleza kuwa Pambalu alijitoa dakika za mwisho.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Patrick Ole Sosopi alisema jumla ya kura zilizopigwa ni 72 na kati ya hizo Wenje amepata kura 59 dhidi ya Pambalu aliyepata kura 13.
Wakati upiga kura ukiendelea, Pambalu akiongozana na watu sita, walitoka nje ya ukumbi na hawakurejea tena.
Hata hivyo, mchakato huo wa uchaguzi ulikamilishwa na mshindi kutangazwa bila uwepo wake ukumbini humo.
Mmoja wa wajumbe walioshiriki uchaguzi huo, alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, akisema Pambalu aliandika barua kulalamikia udanganyifu kwenye uchaguzi huo huku akitaka urudiwe.
Mwananchi limemtafuta Pambalu ili kujua sababu iliyomtoa ukumbini wakati uchaguzi ukiendelea, lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo akidai si wakati mwafaka, bali akiwa tayari atafanya hivyo.
“Nakushukuru lakini kwa sasa siwezi kuzungumza kwa nini mimi nimetoka nje. Hili ni suala la ndani ya chama, ni mapema kuzungumza, ukifika wakati nitazungumza,” amesema.
Mjumbe mwingine aliyekuwepo wakati wa uchaguzi huo, amesema Pambalu alisusia uchaguzi akidai si wa haki na kuomba uahirishwe, ndiyo maana alitoka nje ya ukumbi wakati ukiendelea.
“Pambalu hajaridhishwa na uchaguzi kwa maana kuna kitu ambacho hakiko sawa, amesusa na ameandika barua kwa Katibu Mkuu akiomba urudiwe,” amesema mjumbe huyo kwa sharti la kutotaja jina lake.
Mjumbe huyo amedai kwamba usiku wa kuamkia Mei 25, 2024, Pambalu na watu wake walivamia hoteli waliyolala wasimamizi wa uchaguzi na wajumbe wengine na kuanzisha vurugu, wakidai wamepokea rushwa kutoka Wenje.
Amesema walidai pia kwamba Wenje amesafirisha wapigakura kutoka majimbo mbalimbali kama vile Buchosa, Geita na Mwanza kwenda kupiga kura, jambo ambalo amedai halikuwa sawa.
Akizungumzia tuhuma dhidi yake, Wenje amesema ni kawaida kwa sababu baadhi ya watu wakishindwa uchaguzi, mara nyingi wanatafuta sababu.
Hata hivyo, alisema kama Pambalu anasema kulikuwa na mianya ya rushwa ambayo ameisababisha yeye, ataandika barua ya kumtaka athibitishe hilo.
“Apeleke ushaidi kwenye chama na chama chetu kinasema mgombea anaruhusiwa kukata rufaa kwenye hatua mbili, tukiwa kwenye utaratibu wa kuteua wagombea unaruhusiwa kwa sababu umekatwa.
“Na hatua ya pili kama mchakato wa uchaguzi umekamilika, anaruhusiwa kukata rufaa kama hajaridhishwa na matokeo au uchaguzi ulivyoendeshwa,” amesema.
Wenje alisema kuwa wajumbe wa uchaguzi walishangaa kuona Pambalu anatoka nje wakati uchaguzi ukifanyika na alikuwa anafahamu kuwa atashindwa kwenye kinyanganyiro hicho.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema chama kina utaratibu wake, kama kuna kitu ambacho Pambalu hajaridhika nacho kwenye uchaguzi huo, anafahamu taratibu za kufuata kwa kuwa ni mjumbe wa kamati kuu.
“Kama kweli ana malalamiko, nafikiri atafuata utaratibu zilizoainishwa kwenye katiba yetu kwa kuleta malalamiko yake rasmi kwenye chama ili yafanyiwe kazi,” amesema Mrema.
Hata hivyo, amesema hakuwa na taarifa kama Pambalu ameandika barua, kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.