WACHEZAJI wa gofu kutoka klabu mbalimbali nchini, wameanza kujinoa kwa ajili ya mashindano, yanayotarajia kufanyika Morogoro Gymkaha, kuanzia Juni 14 hadi 16.
Mashindano hayo yapo katika kalenda ya Chama cha Gofu Tanzania (TGU) na hadi sasa wachezaji kutoka klabu Kili Golf (Arusha), TPC Club (Moshi), Arusha Gymkhana, Mufindi(Iringa), Lugalo (Dar es Salaam), Moshi Gymkhana, Dar es Salaam Gymkhana Club na wenyeji Morogoro Gymkhana club.
Mzuka wa gofu umefanya mahojiano na nahodha wa klabu ya Morogoro Gymkhana, Seif Mcharo na anasema mashindano hayo ni maalumu kwa wachezaji wa ridhaa, kuwapa nafasi ya kuendelea kuonyesha ushindani na wanaofanya vizuri kupunguza handcup zao.
“Mashindano haya ni ya pointi zitakazotolewa kwa wachezaji watakaocheza upande wa grosi (handcap 0-9),” anasema.
Kwa upande wa zawadi za washindi anasema;
“Zitatolewa kwa washindi wa grosi, neti, junior, senior na Ladies na mashindano hayo yameandaliwa na klabu ya Morogoro Gymkhana, ila kufuata kalenda ya TGU.
Anasema anatarajia kuona ushindani mkali katika mashindano hayo na kama klabu mwenyeji, wanajipanga kuona kila kitu kinakuwa sawa.
“Viwanja vinafanyiwa marekebisho, ili mashindano yatakapoanza kila kitu kiwe safi kwa wachezaji, kitu ninachokitarajia ni ushindani, maana klabu zinazoshiriki zina wachezaji wazuri,” anasema Mcharo.
Mbali na nahodha huyo, Mzuka wa Gofu, umezungumza na wachezaji mbalimbali ambao wanajiandaa na mashindano hayo.
George Sembi kutoka klabu ya TPC, Moshi anasema baada ya kukosa ubingwa katika mashindano ya Morogoro open mwaka jana, anaweka nguvu ya kuhakikisha anafanikisha hilo.
“Katika mashindano ya mwaka jana, nilishika nafasi ya pili, bingwa alikuwa Godfrey Leveriana kutoka Morogoro, hivyo yajayo nataka niwe bingwa,” anasema.
Anasema kwa sasa anafanya mazoezi kila siku akimaliza viwanja 18,
“Pia mazoezi ya upigaji wa mipira maeneo ya mbali ‘range’ nikiwa eneo hilo huwa napiga mipira 200 kila siku, hadi kufikia siku mashindano, nitakuwa nipo fiti.”
Mchezaji mwingine kutoka klabu hiyo, Elisha Bwambo anasema; “Nimejiandaa vizuri, mashindano hayo yanaonyesha ubora wa mchezaji, malengo yangu mwaka huu ni kuvuna mataji mengi.
Mchezaji mwingine wa TPC, Ally Mcharo anasema; “Mashindano hayo yatakuwa na ushindani, kulingana na jinsi ambavyo wachezaji wameyapania, binafsi napenda kucheza viwanja vya Morogoro ni vizuri.”
PROSPER EMANUEL-LUGALO CLUB
Kwa upande wa Prosper Emmanuel kutoka klabu ya Lugalo anasema “Nafanya mazoezi kwa kucheza viwanja 36 na wachezaji wenzangu, naamini yatanifanya niwe na uwezo wa kufanya vizuri kwenye mashindano hayo, kuna wakati mwingine tunachangisha pesa, ili anayefanya vizuri achukue pesa.
Malius Kajuna kutoka klabu ya Lugalo, anasema; “Kwa namna nilivyojiandaa natamani mashindano yaanze muda wowote kuanzia sasa, nipo tayari na nimepania kuchukua taji.
Imeandikwa na Brown Msyani, Olipa Assa na Nevumba Abubakar