Wizara nne kuibua mijadala bungeni

Dodoma. Wakati wabunge kesho Jumatatu, Mei 27, 2024 wakihitimisha mjadala mkali wa changamoto ya migogoro ya ardhi, wiki itakuwa na bajeti tatu ikiwamo ya Wizara ya Ujenzi na ya Maliasili na Utalii. 

Mjadala ulianza Ijumaa ya Mei 24, 2024 wakati wabunge wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyowasilishwa na waziri wake, Jerry Silaa.

 Hoja za wabunge wengi kwenye wizara hiyo, iliyopewa siku mbili za mjadala wa bajeti, ni migogoro ya ardhi ambayo mingi inachangiwa na kutokuwepo kwa mipango bora ya matumizi ya ardhi, weledi kwa watumishi, ucheleweshaji na fidia isiyo na maslahi kwa wananchi. 

Waziri Silaa atakuwa na shughuli ya kupangua hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wabunge na kuwaomba wampitishie bajeti yake.

Baada ya mjadala huo, kiti kitahamia kwenye makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Ujenzi  kisha Wizara ya Maliasili na Utalii itafunga dimba kwa wiki hiyo. 

Kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Kimataifa inayoongozwa na Waziri, January Makamba miongoni mwa mambo yatakayoibua mjadala ni mchango wa Watanzania waliopata uraia wa nchi nyingine na ulipofikia mchakato wa kutoa hadhi maalumu kwa kundi hilo. 

Pia ukarabati na ujenzi wa majengo katika viwanja vya Tanzania vilivyopo kwenye balozi mbalimbali duniani, nayo ni miongoni mwa hoja inazotarajiwa kutikisa kwenye mjadala huo wa siku moja. 

Katika taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa mwaka 2023, iliyojadiliwa bungeni Februari 2024, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vita Kawawa alizungumzia kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa majengo ya ubalozi. 

“Kutokuwa na ukomo wa muda wa majadiliano kuhusu ujenzi wa majengo ya ubalozi yakiwamo majengo ya vitega uchumi ni jambo linalochangia miradi ya ujenzi wa majengo ya ubalozi kuchelewa kuanza utekelezaji,” amesema Kawawa. 

Amesema pia ufinyu wa bajeti inayoidhinishwa na Bunge kwa pamoja na upatikanaji wa fedha pungufu ya bajeti iliyoidhinishwa tena kwa kuchelewa ni mambo yaliyotarajiwa kukwamisha miradi ya ujenzi wa majengo ya balozi nje ya nchi. 

Mwaka 2023/24, Bunge liliidhinishia wizara hiyo bajeti ya Sh247.97 bilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh230.08 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Sh17.88 bilioni zikiwa ni za maendeleo. 

Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, miongoni mwa hoja kubwa zinazotarajiwa kuzua mjadala ni urekebishaji wa barabara zilizoathiriwa na mvua nchini ambazo zilisababisha baadhi ya maeneo kutofikika. 

Miongoni mwa barabara hizo ni ile ya Kilwa (Pwani) hadi Nangukuru (Lindi) kutokana na kukatika kwa daraja, kipande cha barabara chenye urefu wa mita 50 kilicopata mpasuko mkubwa eneo la Busunzu wilayani Kibondo mkoani Kigoma. 

Hoja nyingine ambayo inatarajiwa kuzua mjadala katika bajeti hiyo ni jinsi Serikali ilivyojipanga kulipa madeni wanayodaiwa na makandarasi na wahandisi washauri wa ndani na nje ya nchi wanaotekekeleza miradi mbalimbali. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu shughuli zilizotekelezwa kwa mwaka 2023, walisema makandarasi na wahandisi washauri wa ndani na nje ya nchi walikuwa wanadai Sh6.37 trilioni. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso alisema deni hilo la Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ni la hadi kufikia Desemba mwaka 2023. 

Hoja nyingine ni uwezeshaji wa makandarasi wa nchini kuweza kuchukua kandarasi katika miradi mbalimbali na pia utoaji wa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR). 

Sekta ya ujenzi iliyokuwa katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kabla ya kugawanywa na kuwa wizara inayojitegemea iliidhinishiwa na Bunge bajeti ya Sh1.46 trilioni katika bajeti ya mwaka 2023/24. 

Kati ya fedha hizo, Sh48.39 bilioni zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya Sh1.41 trilioni zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Wizara hiyo, inayoongozwa na Waziri Innocent Bashungwa itakuwa na wajibu wa kueleza kinachoendelea juu ya hali ya vivuko vinavyotishia hali ya abiria wanaovitumia.

Wizara nyingine ni ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Angellah Kairuki kukiwa na mjadala wa uvamizi wa wanyama waharibifu pamoja na kiwango kidogo cha fidia wanacholipwa wananchi ambao wanadhurika, kuuawa ama mali zao kuharibiwa na wanyama hao. 

Hoja nyingine ni kuharibika kwa miundombinu katika maeneo ya utalii kutokana na mvua kubwa zilizonyesha nchini na hivyo kusababisha maeneo hayo kupitika kwa shida.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilishauri wizara hiyo kushirikiana na Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro baina ya hifadhi na wananchi. 

“Kuweka mikakati ya kuchimba mabwawa na visima vya maji kwa ajili ya wanyamapori kwenye maeneo ambayo yana upungufu wa maji ili kupunguza kasi ya wanyama hao kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi kutafuta maji,” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo Timotheo Mnzava. 

Akisoma taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2023, Februari mwaka huu, Mnzava alitaka itolewe elimu kwa wananchi kuhusu maeneo ya shoroba za wanyamapori ili kupunguza muingiliano kwa wanyama na binadamu. 

Mwaka 2023/24, Bunge liliidhinisha matumizi ya Sh624.14 bilioni kwa wizara hiyo ambapo Sh 443.70 bilioni zilikwenda katika matumizi ya kawaida huku Sh180.43 bilioni zikiwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mkazi wa Somanga, Kilwa mkoani Lindi, Karimu January amewaomba wabunge kupambania urekebishaji wa barabara zilizoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha katika mkoa huo na kukatisha mawasiliano. 

“Sisi ni watu tulioathirika kwa kiasi kikubwa na mvua zilizonyesha mapema mwaka huu kwa sababu maji mengi yamepita mashambani licha ya kuharibu barabara na kukatiza mawasiliano kwa siku kadhaa,” amesema. 

January ameshauri Serikali kuweka miundombinu ya mifereji na makalivati yatakayowezesha kupunguza adha ya maji endapo mwakani kutakuwa na mvua nyingi kama zilizonyesha mwaka jana. 

Kwa upande wake, Mkazi wa Dodoma, Eveline Mwakagenda amesema Watanzania wengi waliopata uraia wa nchi nyingine, wanapenda kuchangia maendeleo nchini lakini bado hakujawa na mipango mizuri ya kuwawezesha ushiriki wao kwenye uchumi kutambuliwa. 

“Tunasubiri katika bajeti hii kuona kama hizo hadhi maalumu zimefikia wapi maana naona hili suala la uraia pacha limekuwa gumu kukubalika nchini. Lazima tuelewe wengine wameamua kuchukua uraia wa nchi nyingine sababu ya kutafuta maisha tu,” amesema Mwakagenda. 

Mbunge wa viti maalumu Cecilia Pareso amesema kumekuwa na changamoto ya wanyama wakali kwa hiyo bajeti ijayo wanategemea Serikali kujikita katika eneo hilo kwa kuhakikisha inakuja na suluhisho. 

Pia, amesema wanatarajia kuona mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha utalii unakuwa endelevu na pia kuendelea kubuni vivutio vingine zaidi ya vilivyopo ikiwamo na vitu vinavyoendelea kuvutia watalii vya kiutamaduni na mila. 

“Hali ya miundombinu bado sio nzuri katika hifadhi zetu, kama umeona clip za video zinatembea za Ngorongoro na Serengeti zikionyesha kuharibika kwa barabara wakati wa mvua nyingi zilipokuwa zikinyesha. Tunarajia sasa Serikali inaweka bajeti ya kutosha kutengeneza barabara rafiki kwenye maeneo ya hifadhi,” amesema.

Related Posts