Serikali imeonyesha nia nje, kazi kwa TFF

WIKI iliyopita Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka 2024/25 yaliyoonyesha ongezeko kubwa la zaidi ya asilimia 700 kutoka bajeti yake iliyozoeleka iliyokuwa ya takriban Sh35 Bilioni.

Bajeti ya safari hii imefikia Sh285.3 Bilioni ukilinganisha na ya mwaka uliopita wa fedha iliyokuwa Sh35.4 Bilioni.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro alisema kati ya fedha hizo, Sh258.2 Bilioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 2,082 kitu ambacho ni rekodi kwa wizara hiyo.

Dk. Ndumbaro alisema makadirio hayo ni maandalizi ya nchi kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.

Mbali na fainali hizo, Tanzania pia itakuwa mwenyeji wa fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zitakazofanyika Septemba. Fainali hizo hushirikisha wachezaji wanaosakata soka ndani ya Bara la Afrika.

Ni wazi wizara hiyo inashughulikia michezo yote, lakini hili la kutenga fedha nyingi za maendeleo linahusu zaidi mchezo wa soka kutokana na mashindano hayo makubwa ya mwaka 2027 yatakayohusisha ujenzi wa uwanja mpya mkoani Arusha na uboreshaji wa viwanja vingine.

Hata hivyo, michezo mingi itanufaika baada ya kumalizika kwa fainali hizo kwa kuwa serikali inajenga viwanja vya viwango vya Olimpiki ambavyo hutumiwa kwa michezo mingine kama riadha na raga.

Ni wazi kwamba kwa makadirio hayo, serikali imeonyesha nia ya dhati ya kuhakikisha fainali za Afcon 2027 zinakuwa na mafanikio kwa upande wa miundombinu ya michezo, ambayo bila shaka itafuatiwa na miundombinu mingine ya usafiri na mawasiliano na hivyo kunufaisha hata wasiopenda michezo.

Tayari uwanja wa Benjamin Mkapa uko kwenye maboresho huku kukiwa na taarifa kuwa viwanja vingine sita kwa ajili ya mazoezi vitafanyiwa kazi jijini Dar es Salaam kuhakikisha timu hazipati shida kimaandalizi.

Pia uwanja mpya unaotarajiwa kuwa wa kisasa umeanza kujengwa mkoani Arusha na unatarajiwa kupewa jina la Samia Suluhu. Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 30,000 na utatumiwa na michezo mingine. Ujenzi wa uwanja huo utagharimu Sh. Bilioni 286, zaidi ya bajeti nzima ya wizara ya 2024/25.

Kwa kiasi kikubwa serikali imejitengenezea msingi mzuri kwa ajili ya kufanikisha fainali hizo kwa kuwa bajeti ya mwakani itahitaji ongezeko dogo tu kujazia kile kikubwa kilichotengwa mwaka huu. Mwaka 2027 hauko mbali sana, hasa unapokuwa unaandaa fainali hizo kubwa katika soka barani Afrika.

Ujenzi wa miundombinu ya michezo na hasa viwanja, unatakiwa ukamilike mapema kuondoa kadhia ya kupokonywa uenyeji, uamuzi ambao huchafua taswira ya nchi, ikizingatiwa mataifa mengine yaliomba uenyeji huo.

Tatizo litabakia kuwa utoaji wa fedha kulingana na mkataba ili uwanja wa Samia Suluhu umalizike mwakani kama ilivyopangwa. Lakini nia hiyo ya dhati ya kutenga kiasi kikubwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo haitaishia kwenye kupanga tu, bali kutekeleza.

Kilichobaki sasa ni kwa wadau wengine kuanza maandalizi mapema kama serikali ilivyoonyesha katika bajeti yake.

Wadau wengine kama wahusika katika sekta ya utalii ni lazima waanze kuangalia mapema watatumiaje fursa hii kwa kuwa katika baadhi ya nchi kulikuwa na ongezeko kubwa la wageni wakati wa fainali za mashindano makubwa, lakini halikuwa endelevu na hivyo nchi kuachwa kavu.

Kazi hapo ni kuhakikisha huduma katika utalii zinaboreshwa kiasi cha kushawishi wale watakaofuata mechi za Afcon 2027 waone Tanzania ndio sehemu sahihi ya kutalii na mapumziko.

Lakini kikubwa ambacho kasoro zake zitaonekana mapema kama hakutakuwa na maandalizi ya kutosha, ni mafanikio ya timu yetu itakayoshiriki fainali hizo.

Tumeona jinsi Ivory Coast ilivyopambana kuinua hamasa kwa timu baada ya kufanya vibaya mechi za makundi hadi kuwa bingwa wa Afcon 2023.

Mashabiki walikuwa na hamasa, lakini timu haikuonekana kuandaliwa vizuri kisaikolojia na ikabidi ziwepo jitihada za magwiji wan chi hiyo pamoja na chama kumtimua kocha na ndipo ari iliporejea hadi timu kuwa bingwa.

Lakini nchi kama Burkina Fasso, ambayo haikuwa ikipewa nafasi kubwa sana wakati wa fainali za mwaka 1998. Lakini maandalizi mazuri mazuri yaliwashangaza wengi na timu hiyo ikatolewa katika hatua ya nusu fainali.

Ili kuepuka kadhia ni muhimu Shirikisho la Soka (TFF) likaanza maandalizi sasa ya kiufundi kwa kuwa ndilo eneo ambalo linahusika zaidi kwenye maandalizi.

Ni lazima benchi la ufundi la Taifa Stars lianze kujengwa sasa kwa kuweka watu wenye utaalamu na ubora stahiki, badala ya kundi la watu waliosadia katika siasa za uchaguzi, ndugu, marafiki au wapambe, maarufu kama machawa.

Ni ajabu kwamba baadhi ya watu walio katika benchi la ufundi la Taifa Stars, hutumika kama wahudumu uwanjani wakati wa mechi za Ligi Kuu, hasa zile kubwa kama za mwishoni mwa msimu.

Huwezi kusema hawa wanastahili kuwemo kwenye benchi la ufundi la timu ya nchi inayoandaa fainali na inayotaka ipate mafanikio.

Ni muhimu kufumua benchi hilo na kutafuta kocha anayeijua Afrika au ambaye hajachafuliwa na siasa za soka la Afrika, kumuamini katika kile anachopanga kitaalamu na kumvumilia huku tathmini ya uhakika ikifanyika ili kuepuka kufanya maamuzi katika dakika za mwisho ambayo yatavuruga timu.

Tunaweza kufanikiwa kuandaa fainali hizo kwa ubora wa hali ya juu, lakini tukaacha rekodi mbovu kwa mashabiki wa soka wa Tanzania iwapo timu itaendeleza mazoea yake ya kutolewa katika hatua ya makundi kama ilivyokuwa katika fainali tatu ambazo nchi imeshashiriki.

Uamuzi wa serikali kuonyesha nia yake ya dhati unatakiwa uwe deni kubwa kwa Shirikisho la Soka (TFF) ili lianze kufanya maandalizi yanayolingana na nia hiyo njema ya serikali.

Related Posts