Mbeya. Viongozi wa dini mkoani Mbeya wamempokea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa vilio vya wananchi kuhusu barabara za lami na madaraja wakieleza kuwa kwa sasa wanasubiri kibali cha Serikali kumaliza changamoto hizo.
Viongozi hao wa dini wamebainisha hayo leo Mei 26, 2024 wakati wa misa ya kumsimika Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Godfrey Mwasekaga iliyohudhuriwa na mamia ya waumini na viongozi wa Serikali, huku Majaliwa akiwa mgeni rasmi.
Akizungumza kwenye misa hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbeya, Gervas Nyaisonga amesema kilio cha wananchi wa Mbeya ni barabara za lami.
Amesema Jimbo la Katoliki linasimamia pia Mkoa wa Songwe ambako changamoto zao kubwa ni madaraja, ambayo yanahatarisha maisha ya wananchi na ukosefu wa umeme.
“Waziri Mkuu (Majaliwa) pokea vilio vya wananchi, Mbeya tunahitaji barabara za lami kuunganisha mikoa ya Singida na Tabora lakini kwa Songwe shida kubwa ni madaraja na umeme,” amesema na kuongeza:
“Kule Songwe kuna daraja walijenga wamisionari mwaka 1957, lilibomolewa tangu 1979, hivyo kumekuwepo na changamoto hiyo sambamba na kukosa umeme katika vijiji vya Mukulwe na Tururu, upande wa Sumbawanga kilipo kituo cha afya lakini hakuna huduma hiyo licha ya juhudi zilizofanyika. Tanroads na Tarura wanasubiri kibali chako kazi ianze,” amesema Askofu Nyaisonga.
Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), ameongeza kuwa kuwepo kwa barabara zinazounganisha Mbeya, Singida na Tabora zitafanya uchumi wa wananchi wa mikoa hiyo kuimarika.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuendelea na msimamo wake wa kupinga vikali vitendo visivyoendana na utamaduni wa Tanzania, ikiwamo ndoa za jinsia moja na kwamba viongozi wa dini wataendelea kukemea kwa waumini wao.
“Lakini nimpongeze Askofu Msaidizi, Mwasekaga kwa kuteuliwa na tunaamini atatusaidia kuendelea kufanya vizuri na sisi tunamuahidi ushirikiano, Kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana pia na Serikali kuhakikisha tunafikisha maendeleo kwa wananchi,” amesema Askofu Nyaisonga.
Akitoa salamu kwa niaba ya TEC, Makamu wa Rais wa Baraza hilo, Askofu Francis Kasala amesema uteuzi wa Askofu Msaidizi ni mbegu iliyopandwa na wamisionari na zawadi ya injili ambayo imeanza kuzaa matunda.
“Kwanza tunakupongeza Askofu Mwasekaga na kukukaribisha, tunaamini katika utendaji kazi wako, hatuna shaka na tunatarajia mafanikio makubwa na Baraza litakupa ushirikiano wa kutosha,” amesema.
Akizungumza wakati wa ibada ya kumwekwa Askofu Mwasekaga, Mhashamu Polycarp Kardinali Pengo amemtaka askofu huyo kuhudumia waamini wa makanisa yote na kusambaza injili.
“Usiache kushughulika na makanisa yote kwani wanahitaji msaada wako, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe injili inafundishwa, kwani kutofanya hivyo ni kukiuka maelekezo ya Yesu Kristo,” amesema kardinali huyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Mbeya kuna utulivu kutokana na ushirikiano wa karibu na taasisi za dini na ameahidi kufanyia kazi changamoto zilizotajwa.
“Meneja Tanroads yupo hapa, Tanesco wapo hapa, hivyo changamoto hizi zitatekelezwa haraka kwani hadi sasa ipo miradi ya barabara nne inaendelea na mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Kiwira,” amesema Homera.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson amesema kwa kipindi cha miaka 125 ya Jubilei ya Uinjilishaji, Kanisa Katoliki linajivunia uongozi makini na imara kwani tangu kuwepo kwao halijawahi kuwa na migogoro.
“Ile FFU (Field Force Unity) sisi mitaani tunaiita Fanya Fujo Uone, lakini pamoja na yote hatujawahi kuona polisi wakienda Kanisa Katoliki kutuliza mgogoro, hii inaonyesha namna uongozi ulivyo makini chini ya Askofu Mkuu, Nyaisonga, tunaamini nguvu iliyoongezeka ya Askofu Mwasekaga itakuwa na tija,” amesema Dk Tulia.
Askofu msaidizi, Mwasekaga amewashukuru viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini na madhehebu yote waliofanikisha shughuli hiyo na kuwa jukumu lililobaki ni kuendelea kumtumikia Mungu.
“Hadi sasa mama yangu alishafariki, baba yangu umri umeenda, ana miaka 92 na leo ameshindwa kufika kwenye tukio hili, lakini kipekee nitashukuru maaskofu wenzangu, viongozi wa dini mbalimbali, Serikali, waamini na wananchi wote kwa kufanikisha hili na sasa naenda kumtumikia Mungu,” amesema Mwasekaga.
Akizungumzia changamoto hizo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwa sasa barabara ya Makongorosi hadi Rungwa yenye urefu wa kilomita 112 na Rungwa hadi Itigi (kilomita 219), bajeti yake itakuwa mwaka huu wa fedha wa 2024/25.
Amesema barabara ya Itigi hadi Rolanga mkoani Singida kilomita 219, ujenzi wake unaendelea huku kutoka Mbeya hadi Makongorosi, mradi umeisha na kwamba Serikali inapambana kukamilisha mradi huo ili wananchi kutoka mikoa ya Kaskazini na Kati wafike kirahisi Mbeya.
“Katika mwaka wa fedha ujao, serikali imetenga fedha za barabara kwa kiwango cha lami kutoka Rungwa hadi Ipole mkoani Tabora na kwa kipindi kifupi kijacho tutasafiri kwa mabasi kupitia mikoa hiyo kwa raha,” amesema Majaliwa.
“Kuhusu madaraja yaliyotajwa, naomba niiagize Tarura mkoani Songwe kufungua barabara na kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu utekekezaji wa miradi hii na Meneja wa Tarura aharakishe usanifu wa daraja hilo,” amesema Waziri Mkuu.
Kiongozi huyo wa Serikali ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imefungua milango kwa taasisi za dini katika kuishauri kwenye masuala ya maendeleo kwa wananchi na kwamba wanathamini mchango wa taasisi za dini.
Wakati huohuo, Majaliwa ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kupiga kura akieleza kuwa kutakuwapo maboresho ikiwamo kuhakiki majina.
“Vijana kama nguvu ya Taifa ambao walikuwa hawajafikisha umri wa kupiga kura, ambao sasa wamekidhi vigezo na wengine wenye sifa, shiriki vema haki yako ya uchaguzi, waliohama maeneo nenda kafanye mabadiliko usipitwe na haki hii ya msingi kikatiba,” amesema Majaliwa.