Lissu: Ugumu wa maisha utamalizika tukipata Katiba mpya

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-Bara, Tundu Lisu amesema suluhisho la kumaliza ugumu wa maisha uliotamalaki nchini Tanzania ni kwa wananchi wakubali kuanza kutafuta Katiba Mpya.

Amesema ugumu huo unachangiwa na upungufu wa Katiba iliyopo kiasi kwamba imezalisha utawala wa viongozi wenye miungu wengi wanaopanga maisha ya watu badala ya kuwa na Mungu mmoja wa mbinguni.

Lissu ameyasema hayo leo Jumapili, Mei 26, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembeyanga Temeke, mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi huku akieleza bila kupatikana Katiba Mpya hali ya maisha itaendelea kubaki ya kutisha.

“Umungu wa viongozi unaoendelea nchini usipobadilishwa kwa Katiba tutaangamia. Niwakumbushe tangu miaka 17 tuliyokutana hapa Mwembeyanga kuzungumzia orodha ya mafisadi tatizo ilo limeendelea kuwa la kutisha nchini mpaka sasa,” amesema.

Lisu aliyekuwa anataja na historia ya viwanja vya Mwembeyanga jinsi vilivyotumika kutoa orodha ya mafisadi, amesema nchini imeendelea kukumbwa na tatizo hilo kwa sababu ya matokeo ya utawala unaosababishwa na mfumo wa Katiba iliyopo.

“Kama tunataka kupata suluhu ya kudumu, lazima turudi kwenye misingi ya utawala wetu, turudi kwenye Katiba tutengeneze Katiba itakayokuwa hivi tumiungu miungu na tubaki na Mungu mmoja tu wa Mbinguni,” amesema Lissu.

Wakati akieleza hayo, Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza Mei 5, 2024 na wanachama wa chama hicho wa Mkoa wa Dodoma alisema suala la Katiba Mpya wameshakubaliana  kupitia Halmashauri Kuu ya chama hicho kuwa ni muhimu isipokuwa wanachobishana na Chadema ni lini itaanza.

“Sisi (CCM) ukiwa na hoja tunaisikiliza na tunaikubali. Kwenye Baraza la Vyama, wote tulikubaliana kwamba katiba ni muhimu lakini tunachobishania ni lini? CCM hatukatai na Watanzania wanaitaka Katiba; lakini wenzetu (Chadema) wanataka katiba leo,” alisema. 

Msingi wa hoja ya Katiba mpya kuendelea kuzungumzwa mara kadhaa katika mikutano mbalimbali ya Chadema na leo Jumapili kwenye mkutano huo imeanzia kwa mwenyekiti wa Chadema-Temeke, Sina Manzi aliyesema hali ya uchumi wa wananchi imekuwa taabani kila uchwao na kuwaomba wananchi kupigania upatikanaji wa Katiba mpya.

Katika mkutano huo, alikuwepo Askofu Maximilian Machumu Maarufu ‘Mwanamapinduzi’ ambaye ameanza kwa kumpa pole Lissu kwa madhila aliyokutana nayo tangu mwaka 2017 hadi sasa huku akieleza safari ya kiongozi huyo imekuwa ya kumuamini Mungu.

“Nakuita mujiza unaotembea na umewekwa kwa ajili ya kuikomboa nchi,” amesema

Amesema licha ya Tanzania kuwa na rasilimali ardhi lakini ukosefu wa siasa safi ni tatizo la kutokupiga hatua kimaendeleo na imekuwa ikizaa safu ya uongozi mchafu.

“Maaskofu tukija kwenye siasa tunaambiwa msichanganye dini na siasa ili wabaki wachache wachafue siasa ili waseme siasa ni mchezo mchafu,” amesema.

Related Posts