ACT-Wazalendo yapanga kufumua mikataba, CCM yasema wanatafuta huruma kisiasa

Unguja. Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuna mikataba mingi mibovu inayoigharimu nchi na kwamba kikiingia madarakani mwakani kitahakikisha inafumuliwa na kuweka mipya.

Kauli hiyo iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo-Zanzibar, Ismali Jussa imejibiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kikisema chama hicho hakina uwezo huo, bali kinalenga kupata huruma ya wananchi na kutafuta umaarufu wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Jussa ametoa kauli hiyo jana Jumamosi, Mei 25, 2024 wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa chama hicho na viongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja Dunga Zanzibar.

 Jussa katika maelezo yake, amenukuu habari iliyochapishwa na magazeti ya Mwananchi na The Citizen Mei 24, 2024 kuhusu mchakato wa zabuni wa pamoja wa kuagiza mafuta chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Zura), ulivyozua kizaazaa kuifanya Zanzibar ikose mafuta kwa siku kadhaa.

 Kwa mujibu wa nyaraka, zabuni zilizotolewa kwa Dola za Marekani kwa tani ambapo Petro Kenya ilipendekeza zabuni ya Dola 66.53 za Marekani, Oilcom (Dola 50), Addax (Dola 194), Hapco (Dola 248) na GBP (Dola 272.7)

 Licha ya kanuni zinazoelekeza mkataba kupewa mzabuni mwenye bei ya chini, lakini mkataba huo ilipewa GBP Tanzania Ltd iliyopendekeza bei ya juu zaidi.

 Hata alipotafutwa Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Omar Ali Yussuf zaidi ya mara tatu, hakuthibitisha wala kukanusha madai hayo, alipokea simu na kukaa kimyaa.

 Katika mkutano huo wa Jussa, amesema, “hatuwezi kuendelea na mambo ya namna hii kuumiza watu, sisi tunasema tutakaposhika dola mwaka 2025 na inshallah tutashika, mikataba yote ya namna hii inavunjwa na kuanza upya.”

 Lakini leo Jumapili Mei 26, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Khamis Mbeto amezungumzia sakata hilo akisema Serikali ilifanya uamuzi wa kuipa zabuni kampuni ya GBP kwa sababu ilikuwa tayari kuingiza mafuta nchini kwa mkopo.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Zanizbar, Khamis Mbeto akizungumza kuhusu madai ya ACT-Wazalendo.

 Kwa mujibu wa Mbeto, kampuni zingine zilikataa kuingiza mafuta kwa mkopo zikidai bei ya nishati hiyo imepanda duniani.

 “Nishati ya mafuta ni uti wa mgongo wa nchi, inapokosekana kwa dakika moja sote tunajua hali inavyokuwa Zanzibar, watu wanaangaika hawafanyi kazi kwa ufanisi wakitafuta nishati ya kuendesha mashine, magari na matumizi mengine,” amesema Mbeto.

Amesema Serikali haiwezi kuacha watu wakihangaika kwa kuendekeza kampuni zinazojali masilahi binafsi na faida badala ya masilahi ya nchi.

 Amesema kampuni ya GBP imejitolea kusambaza mafuta zaidi ya mwaka sasa ikilipwa fedha kidogo kidogo huku kampuni nyingine zikishindwa masharti ya kutoa huduma hiyo.

 Pamoja na hayo, Mbeto ameeleza kuwa kinachofanywa na viongozi wa ACT- Wazalendo ni kutafuta huruma ya wananchi na kutafuta umaarufu wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kufanya siasa za porojo zisizokuwa na ushahidi.

 Mbeto amesema Zanzibar inahitaji kuwa vyama vya upinzani imara vyenye viongozi wenye maono na fikra za kujenga hoja zenye mashiko, kukosoa, kufanya utafiti na kusimamia dhana ya uzalendo na utaifa.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud amesema kiongozi makini ni yule anayepigania masilahi ya umma na Taifa lake.

“Ukishajua unapokweda, unapunguza nusu ya mwendo wa safari, kwa hiyo ndugu zangu tunatakiwa kushikamana kupigania masilahi ya Zanzibar na kama kuna wakati Wazanzibari wameamka ni sasa, huko mbele tunapokwenda kuna giza zaidi,” amesema. 

Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema harakati za kuipigania Zanzibar kupata mamlaka yake zinapaswa kuanza sasa kwani wakisubiri mbeleni kuna giza kubwa.

Kwa mujibu wa Othman, asilimia 54 ya mapato katika uchumi wa Zanzibar yanatokana na vyanzo vya Muungano na ikitokea akaja kiongozi akavichukua, Zanzibar haitabaki na kitu kwa kuwa hivi  sasa ipo kwa kutegemea hisani.

Amesema yapo mambo ambayo kwa mujibu wa Katiba ni ya Muungano lakini kwa sasa yametolewa kama hisani, akitaja ushuru wa forodha, Bandari, Uhamiaji na Mafuta na gesi.

“Haya yote kwa Katiba ni ya Muungano, lakini kwa sasa yametengwa, sasa ikifika wakati akaja kiongozi akasema anayapeleka kwenye Muungano tutabaki bila kitu. Sasa ndio maana sisi ACT tunataka mamlaka kamili kuondoa changamoto hizi ili Wazanziari waache kuishi kama hisani,” amesema.

Related Posts