MAFURIKO. Jiji limesimama, hii ni baada ya jana Jumapili Jiji la Dar es Salaam nusu lilikuwa ni kama mali ya Yanga, baada ya timu hiyo kusimamisha shughuli nyingi ikilipitisha Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Bara baadhi ya maeneo ikikusanya maelfu ya mashabiki wa timu hiyo.
Baada ya Yanga juzi ilikabidhiwa kombe la ubingwa huo wa tatu mfululizo huku kihistoria ukiwa wa 30 jana ilifanya paredi kabambe kama kawaida yao ikitambia rekodi yao hiyo ya makombe.
Shughuli hiyo ilianzia Mbagala na kule ilikuwa ni gari maalumu lililotumika pia kwa kazi kama hiyo msimu uliopita ambalo ni la wazi la kubebea wachezaji likiwa na mashabiki wachache na msemaji wa klabu, Ally Kamwe bila ya kikosi chao likitoka huko hadi Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hapo Kwa Mkapa kulikuwa na mamia ya mashabiki wao na klabu zingine na walikuwa wanaamsha mwili kwa kupata supu ya nyama ya ng’ombe sambamba na mikate na chapati za kutosha wakijiandaa na msafara huo.
Hakukuwa na ubosi hapo, kwani vigogo wa klabu hiyo wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wakiongozwa na Alexander Ngai na Munir Said walikuwa wakiwahudumia wanachama supu hiyo ikilezwa zaidi ya ng’ombe 25 zilichinjwa.
Ilipotimu saa 4:46 msafara huo wa Yanga ukaanza kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiingia Barabara ya Taifa kuitafuta Keko na baadaye kwenda hadi taa za Karume kisha kuifuata njia ya kwenda Kariakoo.
Msafara huo ukiwa njiani kulikuwa na furaha na wakati mwingine maumivu na moja ya tukio lililojiri ni pamoja na shabiki mmoja kujikuta kwenye maumivu ya muda baada ya kutandikwa teke mgongoni na farasi wa Polisi.
Msafara ulipofika eneo la Temeke Chang’ombe pale Chuo cha Ufundi (Veta) shabiki huyo alimsogelea farasi wa Polisi kwa nyuma katika harakati za furaha aliyonayo na kujikuta akipokea teke la nyuma na kuanguka chini kwa sekunde moja kisha kuinuka haraka huku akishika mgongo wake kwa maumivu na kuanza kukimbia taratibu kabla ya kuendelea na vaibu la ubingwa huo.
Msafara huo ulipofika karibu na Soko la Karume neema ikamwibukia beki wa Yanga Yao Kouassi alijikuta akipewa zawadi ya aina yake.
Yao akiwa kwenye furaha na mashabiki waliokuwa wamesimama kando ya barabara kikarushwa kiroba kidogo cha nyanya kisha akakidaka kwa umakini.
Baada ya kukidaka kiroba hicho, beki huyo anayejulikana kwa jina la jeshi akaanza kushangiliwa kwa nguvu huku naye akiinua juu.
Baada ya Yao kukipokea kiroba hicho akamkabidhi kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara Stephanie Aziz KI kisha kuanza kufurahia zawadi hiyo.
Biashara zilikuwa zinaendelea muda wote wa paredi hiyo ambapo waendesha boda boda walikuwa wakiwabeba mashabiki waliochoka kutembea, wauza maji na ice cream nao waliendelea kuna pesa kutoka kwa mashabiki hao ambao walikuwa wakitembea na kukimbia huku wakiimba licha ya jua kuwa kali.
Wakati wote msafara huo ukiwa unapita kulikuwa na watu wengi wamesimama kando ya barabara wengine wakiimba, wakichukua kumbukumbu za picha na hata video huku wale wa Simba wakiwaangalia watani wao kwa simanzi.
Msafara huo ulipotinga Kariakoo hapo hakuna kilichokuwa kinaendelea tena eneo hilo kubwa la biashara hususan kando ya barabara hiyo ambapo kila mtu alisimama nje akitazama paredi hiyo huku hakukuwa na gari iliyokuwa inasogea kwa kutembea zaidi ya yale ambayo yanahusika kwenye shangwe hilo la Yanga.
YAITEKA MSIMBAZI KWA DAKIKA 17
Pale Makao Makuu ya Klabu ya Simba gwaride hilo lilisimama kwa dakika 17 ambapo basi lililowabeba wachezaji lilianza kuwatambia watani wao kwa kulinyayua kombe hilo huku mashabiki wa Yanga wakiimba jina la mfadhili na mdhamini wao GSM kwa muda mrefu.
Staa wa kwanza wa Yanga kulianzisha hapo alikuwa ni winga Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ aliyeanza kucheza dansi ya muziki wa kwao Amapiano lilowapagawisha mashabiki wa timu yake na kumshangilia kwa nguvu.
Skudu aliwanyamazisha mashabiki wa Simba ambao waliingia ndani na kutoka na kombe moja wakiwatambia pia watani hao, kisha Aziz KI akamaliza kwa kulinyanyua mara tatu huku akisema; “Nilinyanyau kombe lile mara tatu nikiwakumbusha kwamba nimewafunga mara tatu tangu nimekuja hapa, achilia mbali nilipowafunga kabla ya kuja Yanga,” alisema Aziz KI.
Saa 7:38 hatimaye msafara huo ulitinga makao makuu ya klabu hiyo jangwani, kisha kikosi hicho kuingia eneo maalum la utambulisho ukianzia kwa viongozi wao, maafisa wa sekretarieti na baadaye kikosi kamili cha Yanga.
Wakati wakiwa hapo beki na nahodha msaidizi wa Yanga Dickson Job alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kuwashukuru mashabiki kwa sapoti yao, tangu msimu huu kuanza hadi kufanikiwa kuchukua ubingwa.
Job amesema wanatambua mchango wa mashabiki ni mkubwa,unawapa nguvu ya kujituma zaidi uwanjani.
“Bado tuna kibarua kingine mbele yetu,msichoke kutuunga mkono katika fainali ya Kombe la FA tutakapokwenda kucheza Zanzibar.
“Tunataka kuchukua taji la FA, hivyo kama mlivyotuunga mkono katika mechi za Ligi Kuu, tunaomba msichoke, imebakia sehemu ndogo.
Rajab Abdul ‘Harmonize’ a.k.a Konde Boy au Jeshi amewapagawisha mashabiki kwa kuwaimba vionjo vya baadhi ya nyimbo zake kisha kumpandisha jukwaani Stephane Aziz Ki mbele ya mashabiki katika Makao Makuu ya klabu hiyo, eneo la Jangwani.
Mara baada ya Konde kupanda jukwaani aliwachizisha wanayanga kwa kuimba kionjo cha wimbo wake wa Sijalewa, kisha alimwita Aziz Ki na kumuuliza maswali machache.
Msanii huyo alimwambia Aziz Ki awaahidi mashabiki wa Yanga kama ataendelea kusalia katika klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili huku pia akimsimamsha Yao akisema atabaki zaidi kwa miaka mitatu.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alitema cheche kwa kuwahakikishia mashabiki wa Yanga kwamba, hakuna mchezaji muhimu hata mmoja katika kikosi chao ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu.
Hersi amesema hayo kuzima uvumi wa nyota Stephane Aziz KI ambaye amekuwa akihusisha na vigogo mbalimbali wa soka ndani na nje ya Afrika kufuatia kiwango bora alichoonyesha akiwa na timu hiyo kuanzia katika Ligi ya Mabingwa Afrika hadi katika mashindano ya ndani.
Kigogo huyo amesema hayo baada ya kushukuru wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo kwa kazi kubwa ya kutwaa ubingwa wa 30 kwa timu hiyo huku akisisitiza kwamba haikuwa rahisi.
“Tunawaahidi tutaenda kuupigania ubingwa na kutambulisha hapa (FA dhidi ya Azam), zaidi ya hapo tunajukumu kubwa la kujenga timu yetu, tunaenda kujenga timu bora kuliko msimu huu, tunaenda kusaini wachezaji bora zaidi,” amesema Hersi na kuongeza;
“Mungu akipenda tutarudi hapa mwakani tena kufurahia mafanikio yetu kwa upande wa kimataifa tunataka kufanya zaidi ya kile ambacho kimefanyika mwaka huu.”
Katika kile ambacho Hersi amekisema alionekana wiki chache zilizopita akiwa DR Congo ambako alienda kufanya mazungumzo ya kusajili wachezaji wapya ikiwa ni mapendekezo ya kocha Miguel Gamondi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Gamondi miongoni mwa maeneo ambayo Yanga inayafanyia kazi ni pamoja na upande wa beki ya kushoto na safu ya ushambuliaji kwa kuongeza mtu wa nguvu ambaye atasaidiana kazi na Joseph Guede.
Katika sherehe hizo, baada ya kuzungumza kwa Hersi wakati Harmonize akitumbuiza kwa dakika chache alimwita Aziz Ki na kumweleza vile anatamani kuendelea kumuona Jangwani kwa miaka mingine ijayo.
Aziz akiwa na tabasamu usoni alionyesha vidole viwili juu ikiwa ni miaka mingine miwili ambayo ameripotiwa kuwa anaweza kusalia zaidi akiwa na timu hiyo.
Fundi huyo wa Burkinafaso, ana vita mbili mbele yake ya kwanza ni kuwania kiatu cha ufungaji bora akiwa na Feisal Salum wa Azam nyingine ni kuipa ubingwa timu hiyo upande wa FA katioka mechi itakayopigwa Juni 2 kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja.