HISIA ZANGU: Ishu ya Aziz Ki, Yanga ina rangi nyingi kama batiki

NIKAMSIKIA mahala rafiki yetu Aziz Ki akisema hajawahi kuona akipendwa mahali popote kama anavyopendwa Tanzania. Nikamsikia akisema ana ofa nzuri kutoka kwingineko, lakini anawapa Yanga kipaumbele. Nikamsikia Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said akisema hakuna mchezaji muhimu ambaye ataondoka Yanga.

Lakini kabla ya hapo nikasikia mahala ndugu yetu Ally Kamwe akidai kwamba Yanga wapo katika hatari ya kumpoteza Aziz na baadhi ya wachezaji muhimu klabuni kama mashabiki hawatajitokeza kununua kadi za uanachama. Tumuamini nani? Aziz, Hersi au Kamwe. Twende tuchambue taratibu.

Tuanze na Aziz mwenyewe. Hiki ni kipimo chake kikubwa cha kutuonyesha kwamba ni mchezaji wa kulipwa. Kama mpaka sasa hajasaini mkataba mpya, basi tuseme anaonyesha ukomavu. Kuna nchi tamu kama Tanzania? Haihitaji kusimuliwa kuhusu utamu wa Tanzania. Amekaa hapa miaka miwili akijirusha nje ya uwanja. Baada ya mechi anazurura Kidimbwi, Tabata, Masaki na kwingineko. Anapokewa kama mfalme.

Lakini kwa klabu ambazo unaambiwa zinamtaka Aziz hasa baada ya kucheza vyema katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu unaamini kwamba zote zinaweza kumpa mshahara mkubwa maradufu kuliko ule anaolipwa Yanga. Kwanza ni kwa sababu ni klabu ambazo zinaonekana kuwa na pesa kuliko Yanga, lakini pia anapatikana kama mchezaji huru. Si amemaliza mkataba.

Aling’ara zaidi katika pambano la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns pale Pretoria, Afrika Kusini. Mechi ilionyeshwa moja kwa moja na televisheni zote za Afrika Kusini na hata bao lake lilipokataliwa mashabiki wa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates walikuwa wamekodoa macho. Ukijumlisha na mashabiki wa Mamelodi wenyewe waliokuwa uwanjani Aziz akaongeza dau lake katika soka la Afrika Kusini.

Kama Yanga alikuwa analipwa Sh23 milioni kwa mwezi, basi wengine wanaweza kumlipa Sh50 milioni kwa mwezi. Pesa ambazo wangeweza kutumia kuilaghai Yanga iwauzie zote watakwenda kuongeza katika mshahara wake. Wazungu huwa wanafanya hivyo. Haishangazi kuona wachezaji mahiri wanaofanikiwa kutoongeza mikataba huwa wanaishia kuwa mamilionea zaidi.

Hiki ndicho kipimo cha weledi kwa Aziz mwenyewe. Kuna mshahara mkubwa kwingineko, lakini kuna kupendwa sana Tanzania. Kuna kina Hamisa Mobetto wanakulilia hadharani. Unaamua kuwa mwanasoka wa kulipwa hasa au unaamua kuufuata moyo wako katika masuala mengine ambayo hayahusu pesa.

Hapa ndipo ambapo kila wikiendi tunamuona Bernard Morrison yupo Dar. Hapa ndipo tunamuona Fiston Mayele mwili wake upo Misri, lakini akili ipo Tanzania. Hapa ndipo unaona kina Emmanuel Okwi walikuwa wanaondoka na kurudi kila mara. Dar es salaam ina raha zake, lakini Watanzania pia wana maisha fulani poa ambapo hata ukiwaacha utawakumbuka kokote unakokwenda.

Sijui Aziz anawaza nini hasa kama bado hajasaini mkataba mpya. Angekuwa mdogo wangu ushauri wangu ungekuwa pesa kwanza, lakini wangapi hatujawahi kuwasikiliza washauri wetu kwa sababu ya mambo ya mapenzi?

Lakini kabla hatujawa washauri wa kina Aziz Ki tujiulize ni kwanini wachezaji wetu wengi hawapendi kutoka nje? Sababu ni zilezile ambazo pia zinawafanya wachezaji wanaocheza hapa kuona ugumu wa kuondoka.

Tuachane na hilo. Twende katika kauli ya Hersi. Kwamba hakuna mchezaji mkubwa ambaye ataondoka Yanga. Ana siri gani? Aziz amesaini tayari? Kama hajasaini ana uhakika kiasi gani kumbakisha Aziz Yanga? Majuzi hapa alitamba kwamba alitumia akili kuliko pesa nyingi kumleta Aziz makutano ya Twiga na Jangwani.

Ina maana anaweza kumbakisha Aziz kwa akili hii hii na kumfanya Aziz aachane na pesa za kina Kaizer Chiefs na kubakia Yanga? Kwanini Injinia anajiamini hivi wakati Aziz ameshasema bado hajatoa uamuzi kuhusu ni wapi anaweza kucheza msimu ujao?

Kama amesaini na anaficha ukweli, anamfichia nani huu ukweli? Labda wana kitu wanakipanga kwa sababu Yanga wamekuwa wataalamu wa sinema za kuongeza mvuto katika biashara zao za mitandaoni. Hauwezi kuwatabiri sana katika siku za karibuni. Kila kitu wanataka kukigeuza kuwa biashara kubwa.

Halafu akaja kijana mvaa miwani, Kamwe. Kwamba Yanga wapo katika hatari ya kumpoteza Aziz na wachezaji wengine mastaa kama mashabiki wa timu hiyo hawatajiunga katika uanachama wa Yanga. Alidai kwamba anasema kweli anapodai kuwa Aziz hajasaini mkataba mpya Jangwani. Kwamba Kamwe hana uhakika lakini rais wake ana uhakika kuwa Aziz atabaki Yanga.

Tumsikilize nani kati ya rais wa timu na msemaji wa timu? Hapa kwa Kamwe kunatia shaka kidogo. Tangu lini kiongozi wa Yanga au watani zao Simba katika hali kama hii ya Aziz akajitokeza na kudai kwamba hawana uhakika wa kumbakisha mchezaji staa klabuni. Siku zote mabosi wa timu hizi huwa wana majigambo hata kama mambo yanawaelemea.

Kamwe anataka kufanya biashara ya wanachama kwa kutumia sakata la Aziz? Lakini kama tunadhani Kamwe hasemi kweli mbona Aziz mwenyewe amedai bado hajasaini Yanga? Inachekesha kwelikweli, lakini kwa mpira wa Kiafrika hasa Tanzania ni kitu ambacho ni cha kawaida sana. Filamu zetu huwa zina ‘episodes’ nyingi.

Kwa mfano, watu wengi wanaamini kwamba uhusiano wa Clatous Chotta Chama na Simba ni mbovu. Uwezekano wa Chama kuondoka Simba unasemwa kuwa mkubwa, lakini viongozi wa Simba hawajawahi kuja hadharani na kuweka wazi mustakabali wa Chama kama Kamwe alivyojitokeza kuongea kuhusu Aziz. Inakuwa rahisi kusema kwamba Kamwe alikuwa anataka kusogeza biashara ya wanachama.

Kitu ambacho kinaniacha mdomo wazi katika sakata zima ni namna ambavyo watani wao wamekaa kando. Wamekaa mbali. Kuna goli tumelitanua na linatutisha. Aziz anaweza kupatikana bure, lakini kuna rafiki zangu kutoka upande mwingine wanadai hawana ubavu wa kumchukua kutokana na dau lake la usajili na mshahara, lakini ni bora tu Aziz aondoke Yanga aende kwingineko.

Itakapohitajika Aziz aondoke Twiga na Jangwani, basi bora tu aende kwingineko hata kama sio kwao kwa sababu hawana ubavu wa kushindana na kina Kaizer Chiefs. Inanikumbusha hadithi ya Mayele pia. Kwa sasa kila ukifikiria kumpata Fiston unahisi ni ndoto isiyowezekana labda aachwe huru na Pyramids kama ambavyo Luis Miquissone aliachwa huru na Al Ahly.

Unaweza kumuomba kwa mkopo wakakupa kwa sharti la kumlipa mshahara, lakini bado ukashindwa. Wachezaji wanaocheza Tanzania wameanza kuwa ghali siku hizi. Hata hawa wanaopita nchini na kwenda kwingineko wakiwa na mishahara mikubwa wamekuwa ghali kama unataka kuwarudisha. Konde Boy ni mfano halisi.

Suala la Aziz mpaka wakati huu ninapoandika limekuwa na rangi nyingi kama batiki. Njano humohumo. Kijani humohumo. Nyekundu humohumo. Bluu humohumo. Wakati utatuambia. Wala haiwezi kuwa mbali sana. Inaweza kuwa hata wakati huu ninapoweka peni ya chini.

Related Posts