Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema hatishiki na kauli zinazotolewa na baadhi watu wanaomkosoa na kuwa atawapiga ‘spana’ (atawasema) wazembe hadi wanyooke.
Amesema kauli hizo za wakosoaji zinamsaidia kufanya kazi kwa morali kubwa zaidi.
Makonda ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku nne tangu alipodaiwa kumdhalilisha mhandishi wa kike katika halmashuri ya Longido mkoani Arusha, alimpomtaka asogeze kipaza sauti karibu na mdomo ili sauti yake isikike.
“Huongei na mchumba wako hapa, usifanye kama zile umekutana na mtu unataka kumposa. Mimi nina mke, tena mke mzuri,” alisema Makonda.
Kauli hiyo iliibua mjadala, huku Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (CWT), Mary Chatanda na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), na Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla) wakiikemea kwa kumdhalilisha wanawake huyo.
Lakini akizungumza leo Mei 27, 2024 na watendaji wilayani Monduli kwenye ziara yake aliyoipa jina la Siku sita za moto, Makonda ameeleza kushangazwa na wanaokosoa kauli zake, akisema hata Rais Samia Suluhu Hassan alipotukanwa hakusikia mtu akimtetea, badala yake wanaume ndiyo walijitokeza kumtetea.
“Naomba mnivumilie, mtapata watu wengine watakaowasaidia kuwapetipeti, lakini kwangu mimi hilo hapana.
“Nasikia sikia kuna watu wanahangaika na mitandao yao, mimi wananipigia, ni kama umeshawahi kupigiwa muziki ukiwa unataka kulala, mimi kwa umri huu nitishike kwa kauli za watu?” amehoji.
“Umeshawahi kwenda kwenye chumba cha masaji halafu wakakuwekea kale ka-muziki kale, sasa mimi nasikia hiyo hali yaani,” amesema.
Ameendelea kusema kuwa wanaopinga kauli zake ni kama wanambembeleza.
“Wananibembeleza kwamba nenda Makonda endelea, endelea na leo niko Monduli kuwapiga spana wavivu wote lazima wanyooke, hatuwezi kwenda hivyo.
“Nawaambia tena, nitawapiga spana na mnavyojitokeza mnapata nafasi ya kujua naye kumbe huyo yumo,” amesema.
Makonda amesema haiwezekani kwenda kwa kubembeleza watumishi na ndiyo maana hata miradi ina ukomo na usipotekelezwa ndani ya muda inaongeza gharama kwa wananchi.
“Umeshafika Monduli, upande mmoja una Sokoine (Waziri Mkuu wa zamani (Edward Sokoine), mwingine una Lowassa (Edward, pia waziri mkuu wa zamani), halafu unakuwa mwoga, uanze kutetemeka hivi?
“Siku moja nilisema umoja wa waovu wala rushwa na wazembe ni mkubwa sana, ukitaka kujua kama upo mguse mvivu mmoja, wavivu wote unaona wanajitokeza,” amesema.
“Alidhalilishwa hapa Rais wetu mwenyekiti wa chama, mwanadiplomasia namba moja, mama mwenye familia katukanwa asubuhi mpaka asubuhi, sikusikia kauli ya mtu yoyote, halafu wanaume sisi ndiyo tulijitokeza kumpigania yule mama.
“Leo mzembe mmoja, mlarushwa mmoja, mvivu mmoja mnapigapiga kelele huko, eboo! Twende kwenye kazi, amesema”