Metacha atajwa kutua Ihefu | Mwanaspoti

BAADA ya uwepo wa taarifa za Yanga kutaka kuachana na kipa Metacha Mnata, timu ya Ihefu inahusishwa kuzungumza naye na huenda msimu ujao akawa sehemu ya kikosi chao.

Metacha aliwahi kuichezea Singida Big Stars kabla ya kubadilishwa na kuwa Singida Fountain Gate akitokea Yanga, kabla ya kurejea tena Jangwani.

Mmoja wa viongozi wa Ihefu, ameiambia Mwanaspoti kwamba mazungumzo na Metacha yamefikia pazuri na huenda akasaini muda wowote kuanzia sasa.

“Metacha ni kipa mzuri na tumefuatilia tumeona Yanga hawatakuwa na mpango wa kuendelea naye ndio maana tumeweka nguvu ya kuhitaji huduma yake,” amesema kiongozi huyo.

Msimu uliopita Yanga, ilimsajili Metacha kwa mkopo wa miezi sita akitokea Singida Big Stars, lakini ulipoisha ikamuongeza mkataba mwingine na sasa inadaiwa kwamba haitaendelea naye.

Hii ilikuwa mara ya pili Metacha kucheza Yanga, kwani msimu wake wa kwanza ulikuwa ni ule wa 2019/20 akitokea Mbao FC alipocheza hadi 2021 kisha ikaachana naye.

Alipotafutwa kuzungumzia ishu yake na Yanga pamoja na kuhusishwa na Ihefu, mchezaji huyo amesema hayupo tayari kuzungumzia kwani siyo wakati sahihi na utakapofika muda mwafaka kila kitu kitakuwa wazi. 

Related Posts