Mke atupwa jela miezi 6 kisa mumewe kutoroka chini ya dhamana

Moshi/Mwanga. Ni kilio cha kusaga meno, ndio maneno unaweza kuyatumia kuelezea hatua ya Neema Malya (43) na shemejie, kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela, baada ya mumewe kuruka dhamana aliyowekewa na mke huyo.

Ilikuwa ni siku ngumu kwa watoto wa wili hao waliokuwepo mahakamani Ijumaa ya Mei 24, 2024 wakati Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Mwanga, Miriam Mfanga, alipotamka kuwa wadhamini hao ama walipe dhamana ya Sh19.5 milioni au waende jela miezi sita.

Neema na shemejie Valerian Lyamuya (44) ambao walimdhamini Akalufoo Sauli Munisi, hawakuwa na kiasi hicho cha fedha, hivyo wakaenda gerezani, hali ambayo iliibua vilio nje ya mahakama kutoka kwa watoto wa mwanamke huyo.

Wanasheria wamezungumzia hukumu hiyo wakiitaka jamii isikurupuke tu kumdhamini mtu kama hawana uwezo wa kuhakikisha anahudhuria kortini. Mashirika ya kutetea haki za binadamu nayo yamefunguka juu ya hukumu hiyo.

Munisi ambaye ni mume wa Neema, alikuwa anakabiliwa na shtaka la wizi wa vifaa vya umwagiliaji vyenye thamani ya zaidi ya Sh30 milioni, kosa analodaiwa kulitenda Januari 17, 2023.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kivisini Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro na mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela bila kuwapo mahakamani.

“Munisi alihukumiwa jela miaka saba Mei 24, 2024 bila kuwepo hivyo wadhamini wawili hao wawili walitakiwa kulipa fungu la dhamana la Sh19.5milioni au kwenda jela miezi sita, wadhamini hao wameenda jela hawakuwa na hiyo pesa,”amesema.

Wanasheria, wanaharakati wafunguka

Wakili wa Mahakama Kuu na mahakama za chini yake, Patrick Paul amezungumzia kesi hiyo akisema amri hiyo ya hakimu inaweza isiwe na makosa kama wadhamini walisaini bond (dhamana) ya maandishi ya Sh19.5 milioni mahakamani na wameshindwa kuilipa.

“Wadhamini wanahusika pale mshtakiwa anashindwa kufika mahakamani. Unapomdhamini mtu maana yake unadhamini uwepo wake na akiruka dhamana ile bond uliyosaini inatumika, kama huna ndio kifungo kinakuhusu,” amesema.

Kwa upande wake, Wakili David Shillatu aliitaka Jamii kuwa makini wanapodhamini mtu mahakamani na kutambua madhara yanayoweza kujitokeza kama anayedhaminiwa ataruka dhamana.

“Mtuhumiwa akiruka dhamana sheria iko wazi, kwamba ama ulipe ile dhamana uliyosaini au jela. Kwa hiyo jamii iwe inajionya wanapomdhamini mtu. Sio kukimbilia kutoa kitambulisho na kusaini, wajue nini kitatokea akiruka dhamana,” amesema.

Naye Wakili Elia Kiwia amesema mshtakiwa anaporuka dhamana, kinachotakiwa ni mdhamini kulipa fungu la dhamana alilojifunga kulilipa lakini akishindwa kunakuwa hakuna adhabu nyingine zaidi ya kwenda jela na mara nyingi ni miezi sita.

“Mshtakiwa anapokuja kukamatwa baada ya kuhukumiwa bila kuwepo, atafikishwa kortini na kusomewa hukumu yake na atapewa nafasi ya kusikilizwa kama ana sababu mahsusi zilizomfanya ashindwe kufika kortini,” amesema.

Walichokisema wanaharakati

Mkurugenzi wa Shirika la Kilimanjaro Women Information Exchange and Consultancy Organization (Kwieco), Elizabeth Minde, amesema taasisi yake inafuatilia kujua nini kilichotokea hadi mwanamke huyo akafungwa jela.

“Tumesikia hili jambo na sisi tunawasiliana na NPS (Ofisi ya Taifa ya Mashitaka) na Ofisi ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) hapa Kilimanjaro kufahamu kwa undani kabla hatujasema tutachukua hatua gani,” amesema Minde.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Shirika la Action For Justice in Society (AJISO), Virginia Silayo, amesema:  “Hapa kinachotakiwa ni apate wakili wa kumtetea ili afungue shauri dogo kuiomba mahakama imuachie kwa sababu mhusika ameshafungwa na yeye aeleze namna atakavyotoa ushirikiano wa kumtafuta mumewe aje atumikie adhabu yake,” amesema.

Akazungumza na gazeti hili, Wilson Munisi (21) mkazi wa Machame Wilaya ya Hai, amesema kufungwa kwa mama yao kumewaacha njiapanda yeye na mdogo wake, kwa kuwa mama yao ndiye kila kitu na msingi wa maisha yao.

Wilson ambaye alitarajia kujiunga na Chuo Kikuu Oktoba 2024, amesema kwa sasa anaona ndoto zake zinakwenda kufifia kwa kuwa mama yake ambaye ndiye alikuwa tegemeo, yupo jela.

Kijana huyo ambaye alikuwepo kortini adhabu ikitolewa, amesema kwa sasa amebeba jukumu la kumlea mdogo wake wa kike wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 13, kwa kuwa hawana msaada mwingine.

Wilson alieleza kuwa, katika maisha yao kwa sehemu kubwa wamelelewa na mama yao kwa kuwa baba yao alikuwa anaishi Kifaru Wilaya ya Mwanga akijishughulisha na kilimo, huku wao wakiishi Machame na mama yao.

“Binafsi sijaishi sana na baba, nimeishi na mama hata kwenye kusoma mama ndiye nguzo yetu na ndiye tunamtegemea,” amesema kijana huyo na kuongeza kuwa;-

“Nimemaliza kidato cha sita mwaka jana, sikufanikiwa kwenda chuo kwa sababu ya hali ya maisha na kukosa fedha, lakini nilikuwa nimejipanga kwenda chuo Oktoba, lakini kwa changamoto hii, naona itakuwa vigumu,” amesema.

“Mbali na mimi, niko na mdodo wangu yuko kidato cha kwanza ni msichana na bado ni mdogo, hivyo kwa sasa nimeachiwa jukumu la kumwangalia, kuhakikisha anaenda shule na anapata mahitaji yake wakati huu mama hayupo,” amesema.

“Hili jambo limetuathiri sana, maana nikimwangalia mdogo wangu, alishazoea kuishi na mama, lakini sasa nimeachiwa mzigo huu na siwezi kutoka kwenda mbali kwenye vibarua, kutafuta fedha.

“Napaswa kuwa nyumbani ili kumuangalia mdogo wangu kwani siwezi kumuacha alale peke yake nyumbani. Nashindwa kutafuta fedha za kujikimu kimaisha, amesema kijana huyo ambaye baada ya kuhitimu kidato cha sita amekuwa anajishughulisha na vibarua vya ujenzi.

“Nilikuwa napaua nyumba na mama alikuwa akijishughulisha na shughuli za kilimo cha mbogamboga na alijipanga Oktoba niende chuo, lakini kwa sasa siwezi kutoka maana kazi nyingi ziko mbali na nililazimika kwenda kulala huko.”

Mtoto huyo aliziomba mamlaka zinazohusika ikiwamo ustawi wa jamii kuangalia uwezekano wa kumpa mama yake kifungo cha nje, ili aendelea kuiangalia familia, huku akimsihi baba yake kujitokeza kukabiliana na tatizo lililopo mbele yake.

Aeleza dhamana ilivyokuwa

Munisi amesimulia jinsi mama yake alivyohangaika ili baba yao aweze kuachiwa kwa dhamana hadi alivyokamatwa na kutupwa gerezani.

“Kuanzia Mei mwaka jana mama alikuwa akipambania dhamana ya Mzee na ilipofika Februari 19 mwaka huu akafanikiwa kuipata, mzee akatoka, akawa anafuatilia kesi yake akiwa nje,” amesema kijana huyo.

Amesema baadaye baba yao alikwenda nyumbani Machame ambako alikaa kwa siku nne, kisha akaondoka na kurudi Mwanga kuendelea na shughuli zake.

Amesema baada ya kutoonekana mahakamani, walimtafuta bila mafanikio na simu zake hazipatikani na mpaka leo hawajui aliko.

“Baba yeye alikuwa anakaa Mwanga na sisi na mama Machame, sasa alivyoondoka sisi hatukujua na hukumu ilikuwa Aprili 23,2024 lakini hakuonekana mahakamani kwenye kesi yake, hivyo mama akakamatwa,” alisimulia.

“Mama alipoenda mahakamani Aprili 23 alikamatwa, tukaambiwa tutafute wadhamini watatu ili atoke nikakosa wadhamini. Mei 10 akapandishwa mahakamani nikaambiwa nitafute Sh1 milioni niende nazo siku ya hukumu”

Amesema siku ya hukumu Mei 24, 2024 ilishindikana kupata fedha hizo ambazo hakufahamu kama zingekuwa faini au za nini, ndiyo hukumu ikatoka na mama yake akafungwa miezi sita jela.

Related Posts