Dar es Salaam. Wazazi nchini wametakiwa kuacha kuwaogopa watoto wao na badala yake wanaoaswa kuwafanya marafiki ili wafahamu kila changamoto inayowakabili.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata jijini Dar es Salaam, ASP David Mwakinyuke, akisema kama kuna jambo ambalo mzazi anapaswa kulipa kipaumbele ni kuacha kuogopa kuzungumza na mwanaye na kumweleza ukweli wa mambo yanayoendelea kimaisha.
Msingi wa hoja yake unaendana na ukweli wa matukio ya ukatili na unyanyasaji ndani ya familia hali inayoashiria kwamba, kuna uzembe unaotokana na ukimya wa wazazi kwa watoto.
Mathalani, tukio lilotokea Machi 30, 2024 katika Mtaa wa Hangoni Halmashauri ya Babati mkoani Manyara kwa binti mdogo (13) aliyedaiwa kubakwa na baba yake mdogo aliyemfanyia kitendo hicho kwa zaidi ya mara tatu.
Akizungumza wakati wa Ibada Maalumu kuadhimisha Miaka 85 ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) na miaka 45 ya (DCRC) yaliyofanyika Mei 26, 2024 ASP Mwakinyuke amesema: “Dunia tunayopitia ni ya kipekee, kuna kada ya watoto, leo sitaongelea kada ya wakubwa walioolewa au walio kwenye ndoa au waliopo chuo nataka niongelee walio chini ya miaka 18. Hawa wanapita kwenye nyakati ngumu sana. Sisi polisi tunafahamu kwa sababu tunayashuhudia magumu hayo.”
Hata hivyo, amesema kuwa wazazi wana nafasi kubwa kukabiliana na ukatili huo kama wataacha kuwaogopa watoto kwani, kuna wajomba, marafiki hawamuogopi mtoto huyo.
“Nawaomba sana tuache kuwaogopa watoto kwa sababu wajomba au ndugu zako hawamuogopi mwanao na dunia ya sasa inahitaji tuwaambie watoto wetu black and white ‘nyeupe na nyeusi’ sio wa kike wala wa kiume.
“Sio mama sio baba waambieni hii nyeusi na hii nyeupe ukiendelea kumuogopa utakuja naye pale kwetu (Kituo cha Polisi), usimuogope ongea naye sema naye ili afahamu yaliyopo duniani,” amesema Mwakinyuke.