Raia milioni 1.6 wa Afrika Kusini wapiga kura ya mapema – DW – 27.05.2024

Raia wa Afrika Kusini wapatao milioni 1.6 waliokidhi vigezo vya kupiga kura mapema wameanza kufanya hivyo leo chini ya kiwingu cha wasiwasi wa kuvurugika usalama kwenye jimbo la kwaZulu-Natal kutokana na wafuasi wa chama cha uMkhonto we Sizwe kuvamia kituo cha kuhifadhia vifaa vya kupigia kura jana Jumapili.

Vituo vya kupigia kura, vilifunguliwa saa tatu asubuhi na vilitarajiwa kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Kusini na kuendelea tena kesho, Jumanne. 

Zoezi la upigaji kura maalumu limefanyika kwa amani nchini kote kwani hakuna kitendo cha uvunjifu wa usalama kilichoweza kuripotiwa.

Siphiwe Kabini ni mlemavu asiyeweza kutembea aliyezungumnza na DW Kiswahili nchini humo na kusema baada ya kupiga kura kwamba mchakato umeandaliwa vizuri.

“Nilipoingia nimeona ndani ya kituo kila kitu kimepangwa kisha nikachukua karatasi ya kupigia kura nikaenda nayo kuweka alama kisha nikaitumbukiza kwenye sanduku,” alisema Siphiwe.

Soma pia: Kiwango cha ukosefu wa ajira Afrika Kusini kimeongezeka hadi asilimia 32.9

Afrika Kusini Pretoria | Sherehe za "Siku ya Uhuru"
Rais Cyril Ramaphosa akicheza kwenye moja ya matukio ya katika “Siku ya Uhuru” nchini Afrika Kusini. Ramaphosa ndio kiongozi wa sasa wa chama tawala cha Africa National Cogress, ANCPicha: Themba Hadebe/AP/dpa/picture alliance

Watu milioni 1.6 watengewa siku za mbili za kupiga kura

Kwa mujibu wa tume huru ya uchaguzi hapa Afrika Kusini IEC, watu walioomba kupiga kura maalumu idadi yao ni milioni moja na laki sita na wametengewa siku mbili za kuhakikisha wanapiga kura, ikiwa ni leo na kesho. Uchaguzi mkuu utakaojumuisha wapiga kura wote wengine utawafanyika Mei 29.

Japo hakuna tukio la uvunjifu wa usalama ambalo hadi kufikia wakati huu limeripotiwa, lakini katika jimbo la kwaZulu-Natal kumekuwepo na hali ya taharuki kufuatia tukio la jana la wafuasi wa chama cha uMkhonto we Sizwe la kuvamia chumba cha kuhifadhia vifaa vya kupigia kura kwa madai kwamba ANC kilikuwa na njama za kuchakachua kura hata kabla ya zoezi la upigaji kuanza.

Ni tukio ambalo lililaaniwa vikali na Rais Cyril Ramaphosa na katika hotuba yake ya mwisho kabla ya uchaguzi jana usiku Rais alisema, “Sote tunapaswa kuwa na wasiwasi kutokana na ripoti zilizotoka leo kuhusu kuzuiwa kwa shughuli za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na watu kuingia kinyume cha sheria katika maeneo ya kuhifadhia vifaa vya tume ya uchaguzi IEC huko KwaZulu-Natal.”

ANC yapambana kupata viti bungeni

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) John Steenhuisen katika kampeni za mwisho jijini Johaannesburg jana, aliwataka wapiga kura kutokosa fursa ya mara moja maishani ya kuandika historia kwa kukiondoa chama tawala cha African National Congress (ANC) na kukichagua DA kuwa serikali.

Soma pia: Vyama vya kisiasa nchini Afrika Kusini vimefanya kampeni katika wiki ya mwisho kabla ya uchaguzi mkuu

Chama cha EFF Afrika Kusini I Julius Malema
Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Afrika Kusini cha EFF Julius Malema akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika maadhimisho ya miaka 10 tangu kuzaliwa kwa chama hicho Picha: Guillem Sartorio/AFP

Chama cha wapigania uhuru wa kiuchumi EFF ambacho kilihitimisha kampeni zake katika jimbo analotoka kiongozi wake Julius Malema jimbo la Limpopo, kiliahidi mambo makuu matano ambayo ni ardhi, ajira, nishati ya kuaminika, kutokomeza uhalifu sanjari na kupambana na ufisadi.

Rais Cyril Ramaphosa na ANC wanaohangaika kujaribu kupata wingi wa viti katika bunge lijalo wakati ambapo utafiti wa maoni ukionesha kwamba huenda wakapata chini ya asili mia 50 katika uchaguzi huo alihitimisha kampeni zake katika uwanja wa FNB uliopo Soweto jijini Johannesburg na Ramaphosa aliahidi kukuza uchumi.

Afrika kusini taifa kuu la kiuchumi barani afrika inakabiliwa na umaskini, ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana, uhalifu na ukosefu wa nishati ya kuaminika.
Kati ya wakazi milioni 62 wa taifa hili asilimia 32 hawana ajira  na milioni 28 wanapokea msaada wa huduma za jamii kutoka serikalini ili kuweza kuishi, hayo ni kulingana na takwimu za serikali.

Related Posts