BAADA ya kujihakikishia kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, Coastal Union imesema haitakubali kuondokewa kirahisi na nyota wake walioonyesha viwango bora, bali ni kwa maslahi mapana ya timu hiyo.
Costal Union inatarajia kushiriki michuano hiyo kufuatia kumaliza katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu, ambapo itakuwa mara ya pili kucheza kimataifa baada ya miaka 36 kupita tangu ilipofanya hivyo 1988 ilipotwaa ubingwa Bara.
Wagosi hao wamekuwa na matokeo mazuri tangu walipofanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa kumtema Mwinyi Zahera na kumpa kazi Mkenya David Ouma ambaye ameifikisha nusu fainali Kombe la Shirikisho (FA) na nafasi ya nne Ligi Kuu.
Hivi karibuni kumekuwapo na tetesi za baadhi ya mastaa wa timu hiyo ya jijini Tanga kuhusishwa na vigogo vya soka nchini Yanga na Simba wakiwamo kipa Ley Matampi na beki Lameck Lawi kutokana na ubora waliouonyesha.
Meneja wa Mashindano na Katibu wa Kamati ya Usajili wa timu hiyo, Jonathan Tito amesema kwa sasa wanasubiri kumaliza mchezo wa kufunga msimu utakaopigwa kesho Jumanne dhidi ya KMC, kisha kusubiri ripoti ya benchi la ufundi.
Amesema baada ya mafanikio hayo watafanya mabadiliko ikiwa ni kuachana na wachezaji ambao wameonekana kutoendana na kasi ya timu, lakini kuwabakiza waliofanya vizuri kwa ajili ya msimu ujao.
Ameongeza kuwa kwa ajili ya maslahi ya timu wataruhusu wachezaji kuondoka iwapo timu zitakazowataka zitaweka ‘mzigo’ wa maana ambao utaiwezesha Coastal Union kutafuta wengine.
“Muda mwingine mpira ni biashara. Kama kuna timu zitaweka pesa ya kueleweka inayoweza kutufanya kuingia sokoni kutafuta mbadala hatuna tatizo, ila msimamo wetu ni kuondoa waliocheza chini ya viwango na kubakiza waliong’ara,” amesema Tito.
Kuhusu mabadiliko kwenye benchi la ufundi, Tito amesema hawana mpango wa kufanya hivyo kwani Ouma bado ni mali halali ya Wagosi na alisaini kandarasi ya miaka miwili na amefanya vizuri.