Jeshi la Israel limesema hayo baada ya taarifa ya Wizara ya afya na idara ya Ulinzi Gaza inayoongozwa na Hamas kuripoti kuwa watu arobaini na tano wamekufa kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye kambi ya wakimbizi, yaliosababisha moto mkubwa.
Msemaji wa serikali ya Israel Avi Hyman amesema kwamba wanachunguza mkasa huo kujua nini hasa kilitokea, huku akiongeza kuwa kupotea kwa maisha ya raia ni kitu kibaya na kisichovumilika.
Soma pia:Mataifa ya Kiarabu yalaani mashambulizi ya Israel, Rafah
Hata hivyo akifafanua kuhusu oparesheni hiyo ya usiku wa kuamkia leo iliyosababisha takriban watu 45 kupoteza maisha kwa mujibu wa Idara zinazoongoizwa na Hamas, Avi amesema jeshi lilikuwa likiwalenga wapiganaji wa Hamas.
“Kulingana na taarifa za awali moto ulizuka baada ya shambulio hilo. Magaidi walikuwa wamejificha kwenye mahandaki.” Alisema afisa huyo wa Israel.
Aliongeza kwamba kuna raia ambao walijeruhiwa katika mkasa huo. “Ninachoweza kusema ni kwamba hakika lilikuwa ni la kutisha.”
IDF: Tumewauwa maafisa wawili wa Hamas
Jeshi la Israel IDF likieleza kwa undani juu ya mkasa huo limesema, shambulio hilo lilifanywa na vikosi vyake saa chache baada ya kurushwa roketi kutoka Rafah kuulenga mji wa Israel, Tel Aviv.
Kulingana na Israel shambulio lake huko Rafah limefanikiwa kuwaua maafisa wawili waandamizi wa kundi la Hamas.
Soma pia:Ujerumani: Shambulizi la Israel huko Rafah huenda lilikuwa ni ‘kosa’
Kufuatia shambulio hilo Israel imekumbana na ukusoaji mkubwa wa kimataifa kuhusu namna inavyoendesha vita vyake na Hamas.
Marekani ambae ni mshirika wake wa karibu imeoneshwa kukerwa na vifo vya raia katikla eneo hilo linalokabiliwa na mzozo wa kiutu pamoja na mzingoro wa vikosi vya Israel.
Umoja wa Afrika wasikitishwa na shambulizi la Rafah
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat kupitia Ukurasa wake wa X zamani Twitter aliandika kwamba, mashambulizi hayo ya Israel ya kutisha yanaonesha kile alichokiita “dharau” licha ya uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Utoaji Haki ICJ kuimamuru Israel isitishe mashambulzii yake kwenye mji wa Rafah.
Hata hivyo Israel inasisitiza kwamba, inazingatia sheria za kimataifa inapoendesha oparesheni zake katika eneo la Ukanda wa Gaza, hata inapokabiliwa na uchunguzi katika mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa.
Soma pia:Mashambulizi katika mji wa Rafah yanaweza kuzuia makubaliano ya amani
Moja wapo ikiwa ni wiki iliopita ilidai kusitisha mapigano katika mji wa Rafah ambao unawahifadhi zaidi wa Wapalestina milioni moja ambao wamekimbia mapigano katika maeneo mengine ya Gaza.
Shambulio hilo ambalo linatajwa kuwa ni baya zaidi katika vita hivyo, huku Wizara ya afya Gaza inayoongozwa na Hamas ikisema, vifo kutokana na shambulio hilo vinafikisha jumla ya vifo vya Wapalestina 36,000 tangu kuzuka kwa vita mwaka uliopita.