Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene amewataka mawakili kuwa makini dhidi ya rufaa zinazokatwa na Serikali.
Amesema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka wananchi dhidi ya rufaa zinazokatwa na Serikali na kuwataka mawakili kuwa waangalifu kwenye suala hilo.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo mawakili wa Serikali leo Jumatatu, Mei 27, 2024 jijini Dodoma, Simbachawene amesema kwenye utawala bora ni lazima kuzingatia haki za watu na za Serikali na kuna wakati haki hizo zimekuwa na msuguano.
Ametoa mfano wa mwanafalsafa wa Kirusi na Kimarekani ambaye aliishi kati ya mwaka 1905 hadi 1982 ambaye alisema Serikali inaundwa ili kumlinda mtu dhidi ya wahalifu, huku Katiba ikiundwa kumlinda mtu dhidi ya Serikali.
Simbachawene ambaye kitaaluma pia ni mwanasheria, amesema unapoangalia mizania ya haki za watu na za Serikali ni lazima kuwa waangalifu.
“Sio kwamba nyie ni mawakili wa ushindi wa Serikali katika kesi, na wakati mwingine sisi hupokea malalamiko mbalimbali kesi inaanza Mahakama ya Mwanzo, mwananchi kashinda dhidi ya Serikali, Mahakama ya Wilaya mwananchi kashinda, Mahakama Kuu mwananchi kashinda dhidi ya Serikali lakini Serikali hukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa licha ya kushindwa kwenye mahakama zote za chini.”
“Mnapambana Serikali na mwananchi yaani hadi ngazi zote hizo bado unakata rufaa. Na maeneo mengine yanayosemwa sio masilahi ya Serikali, unakuta ni ya mtu ama kikundi fulani hiyo sio sawa na huo sio utawala bora,” amesema.
Amesema kazi ya mawakili ni kulinda haki za watu au mtu lakini pia kulinda haki za Serikali.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Harold Sungusia amesema Katiba ya Nchi ibara ya 13 inaeleza watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Amesema kwa mujibu wa kipengele hicho watu wote wana haki ya kukata rufaa.
Amefafanua Tanzania ina mahakama ya juu ni ya Rufaa lakini kwa nchi nyingine zina mahakama za upeo na katiba zinazowapa uwanda mpana wa kukata rufaa.
Sungusia ametaka suala la haki kutoangaliwa kwa upande mmoja bali pande zote mbili kwa kuwa mwananchi naye asiporidhika anaweza kukata rufaa.
“Mtu akiapa kwa kutumia Katiba anapaswa asome kilichomo ndani ya Katiba,” amesema.
Hata hivyo, amewataka watu kutotumia sheria kama fimbo ya kuwachapia wasioifahamu na badala yake kutanguliza ubinadamu kwenye masuala ya sheria.
Katika mkutano huo, Waziri Simbachawene amesisitiza umuhimu wa kuingia katika matumizi ya akili bandia ili iwasaidie kulinda uaminifu, taaluma lakini pia na kasi ya kutoa huduma kwa kuwa dunia ya leo inavihitaji hivyo kwa pamoja.
“Akili ya kibinadamu, mawazo ya kibinadamu pekee yake yanaweza kutuchelewesha kwa sababu dunia inakwenda kwa kasi, hivyo akili bandia haiepukiki katika utendaji wetu,” amesema.
Pia amesema mawakili hao wanahitaji kujenga mtandao wa ushirikiano na vyombo vingine vya kisheria, asasi za kiraia na mashirika ili kuhakikisha wanaboresha mifumo yao kwa manufaa ya wananchi wote.
Amesema mawakili hao wana wajibu wa kulinda masilahi ya umma kwa kuhakikisha haki inatendeka na wanatekeleza hilo kwa kutoa ushauri kwa Serikali na kusimamia kesi za Serikali.
Simbachawene amesema pia mawakili hao wana nafasi ya kusaidia katika kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka na kupambana na ufisadi kwa katika kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu.
Awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi amesema ofisi yake inasimamia mawakili 3,486.
Amesema mafunzo hayo yanalenga katika kuwajengea uwezo mawakili wa Serikali.
“Kila tulipokuwa tukisoma taarifa mbalimbali kwa mfano ile ya Blue Print kuna maeneo mengi ambayo yanaitaka Serikali kutengeneza mazingira rafiki kwa uwekezaji,” amesema.
Pia, amesema Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Haki Jinai ambapo kuna maeneo mengi yamependekezwa na yamekwishaamuliwa.
Ametaja mojawapo ya maeneo hayo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Mambo ya Ndani kutengeneza mkakati wa kubaini na kuzuia uhalifu.
Amesema pia mawakili hao wana dhamana ya kufanya mabadiliko ya sheria kwa kushirikiana na wadau wao.
“Kumekuwepo na mikataba, tumeona kuna mambo mapya ambayo yametusukuma (kuandaa mafunzo hayo) sio mawakili bali hata wengine kwenye Serikali walio katika shughuli za kisheria kuwa na uelewa wa pamoja,” amesema.