MATARAJIO YA SERIKALI NI KUONA UZALISHAJI KATIKA KIWANDA CHA SUKARI MTIBWA UNAREJEA KWA HARAKA: WAZIRI NDEJEMBI

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MVOMERO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema ni matarajio ya Serikali kuona uzalishaji katika kiwanda cha sukari cha Mtibwa unarejea kwa haraka.

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipofika katika kiwanda hicho ili kujionea mwenyewe hali halisi iliyopelekea ajali ya kupasuka kwa bomba la kusafirisha mvuke (steam) iliyotokea Mei 23, 2024 na kusababisha wafanyakazi 11 kufariki papo hapo na wengine wawili kufariki baadaye wakiwa wanapatiwa matibabu hospitalini.

Amesema “Uzalishaji ukirejea haraka maana yake wafanyakazi watarudi kufanya kazi, wakulima watauza miwa yao kiwandani na hivyo mtazalisha na sukari itapatikana sokoni”.

Mhe. Ndejembi ameelekeza uchunguzi wa kina wa ajali hiyo ukamilike haraka ili tupate taarifa ya kitaalamu itakayo saidia kutumika kwa njia salama zaidi na kuepuka ajali

Ametoa pole kwa wote walio poteza wapendwa wao na kuwahakikishia, kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) uko bega kwa bega na uongozi wa kiwanda tangu ajali ilipotokea ili kuhakikisha familia zote zilizo poteza wapendwa wao wanapatiwa fidia stahiki na kwa wakati. “Mmeona umuhimu wa kujisaji WCF? Ni kwamba ajali zikitokea kutokana na kazi basi Serikali inalipa fidia wahusika kupitia WCF.” Mhe. Waziri ameuhakikishia Uongozi wa Kiwanda.

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma ambaye naye alikuwepo kwenye ziara hiyo, alisema tayari timu ya wataalamu kutoka Mfuko huo imeanza mchakato wa kuwezesha wategemezi wa wafiwa kupata fidia kwa mujibu wa sheria.

“Baada ya tukio la ajali kujulikana tulituma timu yetu maramoja kutokea ofisi yetu ya Morogoro na kufika kiwandani na tayari imekwsiha chukua taarifa za awali ili kuwatambua walengwa na kuanza kuchakata fidia kwa wale walioachwa – wawe ni wenza au watoto.” Amebainisha Dkt. Mduma

Naye Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa ubadilishaji wa mfumo wa kusafirisha mvuke ndio uliopelekea tatizo hilo. Hata hivyo alisisitiza kwamba chanzo halisi cha ajali kitajulikana hapo uchunguzi utakapomalizika.

Aidha mmiliki wa kiwanda hicho Bw. Nassor Ali Seif, amesema tayari kiwanda kimeanza kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na kuanza mipango ya muda mrefu ili kuhakikisha kwamba tukio kama hilo halijitokezi tena.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi (mwenye mic), akizungumza mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kulia) na Uongozi wa kiwanda cha kuzalisha sukari, Mtibwa Sugar chini ya mmiliki wake Bw. Nassor Ali Seif (mwenye balaghashia), akizunguzma mbele ya eneo ilipotokea ajali kiwandani hapo

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi (mwenye mic), akizungumza mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (wapili kulia), Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda (wakwanza kulia) na Uongozi wa kiwanda cha kuzalisha sukari, Mtibwa Sugar chini ya mmiliki wake Bw. Nassor Ali Seif (mwenye balaghashia), akizunguzma mbele ya eneo ilipotokea ajali kiwandani hapo

Mhe. Ndejembi akitoa maeleekzo ya Serikali

Mhe. Ndejembi akiwa na mmiliki wa kiwanda, Bw. Nassor Ali Seif, wakati akiangalia uharibifu uliotokana na ajali hiyo.

Mhe. Ndejembi (mwenye kofia) akitembelea ndani ya kiwanda mahali palipotokea ajali.

Mmiliki wa kiwanda, Bw. Nassor Ali Seif, akieleza mikakati ya kiwanda baada ya ajali hiyo.

Kiongozi wa wahandisi wa kiwanda cha sukari Mtibwa, Mhandisi Juma Said (aliyenyoosha mkono, akieleza jinsi ajali ilivyotokea. Wakwanza kushoto ni Mkuu wa KItengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge.

Mhe. Ndejembi akimsikiliza Bw. Nassor Ali Seif.

Related Posts