Spika aunda kamati kuchunguza mgogoro shamba la Ephata Malonje

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameunda kamati maalumu ya Bunge ya kuchunguza mgogoro kati ya wawekezaji wa shamba la Efatha la Malonje mkoani Rukwa na wanakijiji wanaolizunguka shamba hilo.

Dk Tulia ametoa uamuzi wake leo Jumatatu, Mei 27, 2024 katika taarifa yake aliyoisoma muda mfupi kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge, jijini Dodoma.

Amesema Februari 14, 2024 alipokea barua kutoka Kanisa la Efatha ikiwasilisha utetezi wake kuhusu mchango alioutoa Mbunge wa Kwela, Clement Sangu dhidi ya kanisa hilo.

Amesema mchango huo ulihusu mgogoro kati ya wawekezaji kwenye shamba la Malonje na vijiji vinavyolizunguka shamba hilo, kikiwemo Kijiji cha Sikaunga mkoani Rukwa.

Amesema kwa kuzingatia maombi ya kanisa hilo kukutana na kamati inayohusika ,alipeleka suala hilo kwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ili lifanyiwe.

Amesema kamati hiyo ilikutana na viongozi wa kanisa la Efatha, Sangu na wawakilishi Mei 9, 2024 na iliwasilisha taarifa kwake kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu.

Amesema pia kamati hiyo ilieleza kuwa mgogoro huo umekuwa ukizungumzwa bungeni na wabunge na kwa nyakati tofauti kabla ya Sangu kuingia bungeni.

Dk Tulia amesema licha ya kuwepo kwa kumbukumbu za mawasiliano kati ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wawekezaji hao, kuonyesha mgogoro huo umekwisha, kiuhalisia bado upo na umedumu kwa miaka 13 ukiwa na madhara kwa pande zinazohusika.

Amesema hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Novemba mwaka jana, haziendani na kumbukumbu rasmi za Bunge zilizoko bungeni mwaka 2014 hadi 2015.

Amesema kumbukumbu hizo zinahusu majibu ya Serikali kwa maswali ya wabunge Ignas Malocha (aliyekuwa Mbunge wa Kwela) na Hilary Aeshi (Sumbawanga Mjini).

Amesema pia kamati hiyo ilibaini wanavijiji vinavyozunguka shamba la Malonje hawaridhiki na namna wizara inavyoshughulikia mgogoro huo.

Dk Tulia amesema baada ya kupitia taarifa ya Efatha na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na utalii pamoja na taarifa rasmi za Bunge, ameamua kuunda kamati maalumu chini ya kanuni ya ya 144 ya Bunge.

Amezitaja hadidu za rejea zitakuwa ni kubaini eneo la shamba hilo lilikoanzia na mipaka halisi ya shamba hilo na vijiji vinavyolizunguka.

Nyingine ni kubaini kama taratibu za uongezaji wa eneo zilifuatwa katika uongezaji wa eneo la shamba hilo na kama kuna vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyodaiwa kufanywa na walinzi wa shamba hilo.

Pia rejea nyingine ni kubaini iwapo vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani vinavyodaiwa kufanywa na walinzi wa shamba hilo, vinatokana na miongozo ya wamiliki wa shamba hilo.

Hadidu nyingine ni kubaini kama kuna jambo lolote lingine linalohusiana na mgogoro huo.

Wajumbe wa kamati hiyo itakayoongozwa na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya ni Dk Hamisi Kigwangalla (Nzega Vijijini), Stela Manyanya (Nyasa), Lucy Mayenga (Viti Maalumu), Innocent Bilakwate (Kyerwa), Festo Sanga (Makete).

Wengine ni Asia Halamga (Viti Maalumu) Erick Shigongo (Buchosa), Ester Bulaya (Viti Maalumu), Joseph Tadayo (Mwanga) na  Tauhida Cassian Gallos (Viti Maalumu).

Kamati hiyo itafanya kazi kuanzia Julai 15 hadi 18, 2024 na kwamba kamati hiyo itakabidhi taarifa yake kwa spika kabla ya Agosti 2,2024.

Related Posts