Wanafunzi 600 Dar walevi? | Mwananchi

Dar es Salaam. ’Inawezekanaje zaidi ya wanafunzi 600 wa shule moja kulewa na kulala darasani wakati wa masomo?

Swali hili limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu kudai kuwapo kwa  tatizo kubwa la maadili ya watoto ndani ya jimbo lake.

“Katika Jimbo la Kibamba ambako Rais amejenga shule nzuri kwa gharama ya zaidi ya Sh400 milioni Shule ya Ukombozi yenye watoto 1,400 ikifika saa tano  asubuhi, zaidi ya asilimia 70, yaani watoto 600, wameshalewa dawa za kulevya wanalala darasani,”alisema akiwa bungeni jijini Dodoma Mei 7 mwaka huu.

Kauli hiyo ya Mtemvu ilikuwa sehemu ya maelezo yake ya taarifa kwa Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), Hassan Kungu aliyekuwa akichangia hoja kwenye hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Hii ndio shule ya Sekondari Ukombozi UMC

Madai haya yakalisukuma gazeti la Mwananchi kufuatilia kwa kina madai ya mbunge. Mwandishi anasimulia alivyotumia saa 30 kutazama yale yanayojiri shuleni hapo.

‘’Alfajiri na mapema naelekea Shule ya Ukombozi UMC iliyopo kata ya Saranga Wilaya ya Ubungo. kutoka Barabara kuu ya  Morogoro kuanzia  kituo cha daladala Kimara Temboni hadi shuleni hapo ni mwendo wa  takribani kilomita nane  kwa usafiri wa bajaji ambao ni maarufu eneo hilo.

Kwa usafiri huo unaweza kutumia  takribani nusu saa hadi dakika 45 kufika shuleni na wakati mwingine zaidi ya muda huo kutokana na miundombinu ya barabara kuwa katika hali mbaya. Miinuko mikali na mashimo makubwa yametawala barabarani.’’

Usafiri huo unakugharimu Sh1, 000 kutoka Kimara Temboni,  lakini  kwa walimu, wanafunzi na hata wakazi, ni jambo la kawaida kuwaona wakitembea kwa miguu.

Mandhari ya shule ya Ukombozi UMC lazima yamwache na mshangao yeyote anayeitazama shule kwa jicho la tafakuri tunduizi.

Pengine unaweza kujiuliza je, kulikuwa na ulazima wa shule hiyo kujengwa mahala ilipo ilipo sasa?

Wakati imezoeleka shule kuwa na vyumba vya madarasa eneo moja, shule hii unaweza kusema ni kama chuo chenye kampasi mbili tofauti.

Madarasa yameachana kwa umbali wa  zaidi ya mita 50 huku  katikati  kukiwa  na bonde, hivyo kufanya shule ionekane kama shule A na B.

Kama haitoshi, shule imezungukwa na makazi, kiasi cha kuruhusu mwingiliano mkubwa kati ya wakazi na wanafunzi.

Kama haitoshi, eneo lenye bonde linatumika kama njia  na hapo utakutana wafanyabiashara ndongondogo wanaotafuta mkate wao wa siku kupitia mifuko ya wanafunzi.

Mwanafunzi mmoja aliyezungumza na Mwananchi shuleni hapo, alikiri kuwapo kwa wanafunzi wanaotumia bangi shuleni hapo na hatimaye kusimamishwa masomo.

“Mwezi uliopita (Aprili 2024) kweli kuna wanafunzi wanane walifukuzwa baada ya kukamatwa na bangi na wengine wanatumia sigara. Kabla ya kufukuzwa walikuja askari na kuwakamata baadaye wakaachiwa wakaja shule tukaitwa wakatangazwa ndipo wakafukuzwa,”amesema mwanafunzi huyo ambaye jina lake tunalihifadhi.

Kufuatia taarifa ya uwepo wa tuhuma za wanafunzi zaidi ya wanafunzi 600 kulala darasani kutokana na matumizi ya dawa za kulevya,  mwanafunzi huyo anaeleza kuwa  wanafunzi 20 walichukuliwa sampuli za mkojo kwa ajili ya uchunguzi.

Mei17, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Ubungo akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya na viongozi mbalimbali,  walifika shuleni hapo kuzungumza na wanafunzi hao.
“Alichotuambia ni tuwe na tabia nzuri suala la dawa za kulevya tuepukane nalo, tuhakikishe tunasoma,”amesema mwanafunzi huyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ukombozi,  James Molokozi ambaye pia ni mlezi wa shule hiyo, amesema changamoto ya uvutaji bangi shuleni hapo ipo lakini si kwa kiwango kilichoripotiwa na mbunge, huku akikiri kuwa  hatua kali kwa wanafunzi waliobainika imeshachukuliwa.

“Sisi kama Serikali hata ikiwa ni kwa kiwango kidogo bado ni mapambano, tulipopata taarifa wanafunzi sita walifukuzwa kwa tuhuma hizo na wengine wawili walikuwa chini ya uangalizi,ila sio kweli kwamba tuna wanafunzi 600 wanalala asubuhi,”amesema.

Anasema baada ya kusikia taarifa hizo kutoka kwa mbunge walifika shuleni hapo kujiridhisha ukweli lakini na hawakubaini tatizo hilo.
Mulokozi anasema tayari wanafunzi 20 wameshachukuliwa sampuli kwa ajili ya uchunguzi,  baada ya kutuhumiwa kuwa kwenye mtandao wa matumizi ya dawa za kulevya.

Wanachosema majirani
Mmoja wa majirani wa shule, Hashim Zuberi amesema: “Kuna wanafunzi waliomaliza shule sasa wanajihusisha na dawa za kulevya kwa sababu shule hii haina uzio imekuwa rahisi kwao kuja kuwauzia wengine, na wanachukuliwa hatua,”ameeleza.

Zuberi anaongeza kuwa  wanafunzi hao hufikia hatua ya  kupigana na kutishiana visu,  hali inayowalazimu kuwaamua na kuwataka waondoke karibu na eneo la shule.

Tuhuma wanafunzi 600 walevi

Jirani  aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Peter, anasema kwa upande wake,  hajawahi kuona darasa zima la wanafunzi wakiwa wamelewa darasani.

“Tungekuwa wa kwanza kuwanaona hao wanafunzi, ila kama matukio yapo ni machache na hii si kwa hapa tu maeneo mengi hizi changamoto zipo,”amesema.

Naye Maiko Stephano mzazi mwenye mwanafunzi shuleni hapo anasema kama tatizo hilo  lingekuwepo,  wangeshirikishwa na walimu huku akikiri kuwapo kwa wanafunzi wachache wasio na maadili ambao wamechukuliwa hatua.

Akizungumzia sakata la ulevi kwa wanafunzi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,  Hassan Bomboko amesema tuhuma hizo si za kweli na amefika shuleni hapo na kuona uhalisia.

“Uhalisia eneo la shule haina uzio na hivyo kuna mwingiliano baina ya raia na eneo hilo ambapo pembezoni kuna watu wenye makazi yao, kiwanja cha mpira na maskani ya vijana ambayo inatumika vibaya na vijana kwenye matukio ya mihadarati, ila idadi ya watoto 600 kulewa hakuna ukweli,”anasema.

Ili kubaini ukweli, anasema amefanya ziara ya kushtukiza kwenye shule hiyo na kukagua madarasa  na kutuma wataalamu mbalimbali na kujiridhisha hakuna tukuio hilo.

“Shule ina wanafunzi 1,200, ukisema watoto 600 maana yake ni karibu shule nzima na hatuna kidato cha nne kwenye shule hiyo hawa ni  kidato cha tatu. Wakiwa kidato cha pili ndio walioshika nafasi ya tatu kwa ufaulu kwa wilaya, hivyo wangekuwa mateja wasingeweza kuwa na ufaulu huu,”amesema.

Mpaka sasa anabainisha kuwa, tukio ambalo tayari limeshachukuliwa hatua ni la wanafunzi waliobainika kuwa na kete za bangi na baada ya kufuatiliwa anayewatuma,  walibainika  ni kaka zao ndio wanaowapa wakauze na kufanya matumizi.

“Walikamatwa watano na wakawataja wenzao watatu ambao wanatumia na walifukuzwa shule, kwenye shule korofi,  Ukombozi haipo,”anasema.

Akizungumza na Mwananchi, Mbunge wa Kibamba Mtemvu amesema kama mbunge ana njia nyingi za kupata taarifa.

“Mbunge anaweza kupata taarifa kutoka kwa viongozi, wananchi kupitia mikutano ya hadhara na mwananchi moja moja, uzuri taarifa hii nilipata kwa viongozi, sasa hivi tunahangaika na idadi,

 “Tatizo lipo au halipo lakini maadili ya watoto wetu yakoje, unasema hakuna dawa za kulevya kuna bangi tu kwani nilitamka aina ya dawa za kulevya?”anahoji.

Anaendelea kuhoji:  ‘’Kama imekuwa ngumu kufanya uchunguzi kubaini namna tatizo lilivyo ni jambo la hatari. Wanaojadili kuwa tukio hilo limekuzwa walitaka kuwa dogo kwa kiasi gani?

Katikati ya madai ya mbunge na ukweli kuhusu nidhamu mbovu ya baadhi ya wanafunzi,  matokeo ya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2022 yanaonyesha hali halisi ya taaluma shuleni hapo.

Kwa mujibu wa matokeo kwenye mtandao wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), shule hiyo ilikuwa na  wanafunzi 144.Waliopata daraja la kwanza ni wanne, 13 walipata  daraja la pili, 25 daraja la tatu, 100 daraja la nne, huku  wawili wakipata sifuri.

Mwaka 2023, kulikuwa na watahiniwa 240 wa kidato cha pili, huku wanane wakiibuka na daraja la kwanza, 27 daraja la pili, 37 daraja la tatu na 159 wakipata daraja la nne. Wanafunzi tisa walifeli kwa kupata daraja sifuri.

Related Posts