Wananchi Mtama wajichangisha Sh1.5 milioni kujenga zahanati

Mtama. Wananchi wa Kijiji cha Nahukahuka mkoani Lindi wameanza ujenzi wa zahanati ili kupunguza adha ya kutembea umbali wa kilometa tano kufuata huduma za afya katika Kijiji cha Nyangamara, kilichopo Halmashauri ya Mtama mkoani humo.

Zahanati hiyo itakayogharimu zaidi ya Sh68 milioni ikijengwa na Halmashauri ya Mtama na nguvu za wananchi inatarajia kuhudumia wakazi wapatao 1,973.

Mkazi wa Nahukahuka Birigita Bernad amesema kuwa wanawake na watoto walikuwa wakipata shida kutokana na kukosa huduma ya afya katika kijiji hicho wanalazimika kufuata huduma hiyo umbali mrefu.

Akizungumza baada ya kuwekwa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa leo Jumatatu Mei 27, 2024, Birigita amesema kuwa kutokana na changamoto hiyo waliamua kuanza kwa ujenzi huo wao wenyewe na baadaye wakasaidiwa na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, marehemu Bernad Membe aliyewapa vifaa pamoja na kujenga kufikia hatua ya boma.

“Kutokana na shida kubwa ambayo tulikuwa tunaipata tuliamua kutafuta eneo sisi wenyewe na kuanza kufanya usafi na baadae tukaanza kujenga wanakijiji wote tulikuwa tunafanya kazi kwa ushirikiano na baadaye tukamuomba marehemu Berrnad Membe akatusaidia hadi usawa wa boma,” amesema Birigita

Amesema pia kutokana na juhudi walizokuwa wamefanya Serikali ikawasaidia kumalizia majengo yote ambapo mwenge wa uhuru uliweka jiwe la msingi.

“Tumefurahi sana, baada ya kuona zahanati yetu sasa itaanza kufanya kazi, tunamshukuru. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia zahanati yetu,” amesema pia.

Akisoma taarifa ya mradi wa zahanati hiyo, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Nahukahuka, Hamis Mkuya amesema kuwa mradi huo umegharimu Sh68 milioni, ambapo nguvu za wananchi ni Sh1.5 milioni, mapato ya ndani ya halmashauri Sh15 milioni na Serikali kuu imetoa Sh50 milioni.

Mkimbiza Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava amewapongeza wananchi wa Nahukahuka kwa kujitolea kwa moyo kuweza kuanzisha ujenzi wa zahanati.

“Niwapongeze wananchi wa Nahukahuka, kwa ushirikiano wenu wa kujitoa katika shughuli za kimaendeleo, niwaombe kutunza mazingira ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi,” amesema Mzava.

Related Posts