Mzalishaji pombe bandia aishukuru Mahakama kumtia hatiani

Dar es Salaam. Mfanyabiashara aliyekuwa akimiliki kiwanda bubu cha kutengeneza na kusambaza pombe kali bandia, Frank Donatus Mrema na wenzake wawili aliokuwa amewaajiri katika kiwanda hicho, wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela, huku mmoja akimwaga shukrani kwa Mungu na Mahakama baada ya kutiwa hatiani.

Frank na wenzake hao, Faham Salim Ngoda na Issa Juma Hassan walihuhukumiwa adhabu hiyo jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni (Kinondoni), baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kukutwa na kemikali hatarishi aina ya Ethanol isivyo halali, katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili.

Walikuwa wakitumia kemikali hiyo kutengeneza vileo vikali aina ya K-Vant, Double Kick na Smart Gin na kisha kubandika stika za Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) na nembo bandia za kampuni zinazozalisha vileo hivyo.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Veneranda Kaseko.

Mbali na shtaka hilo la kukutwa na kemikali hatarishi isivyo halali, kinyume cha Sheria ya Udhibiti Dawa za Kulevya, mashtaka mengine yaliyokuwa yakiwakabili ni kukutwa na mihuri yaani stika bandia za TRA na kutumia isivyo halali nembo bandia za biashara za kampuni hizo zinazozalisha vileo hivyo.

Baada ya kutiwa hatiani, kabla ya kusomewa adhabu hiyo, walipewa fursa ya kujitetea kuhusu adhabu,  ndipo Issa akaanza kwa kutoa shukrani kwa Mungu kwa  kufikisha siku hiyo na kumwezesha kufika mahakamani hapo na Mahakama kwa kile alichoeleza kuwa ni uamuzi sahihi dhidi yake.

Hata hivyo,  licha ya shukrani hizo hasa kwa mahakama kwa kutoa uamuzi sahihi dhidi yake ( baada ya kumtia hatiani) amehtimisha kwa kuiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa si mtendaji wa makosa walivyoshtakiwa nayo.

“Mheshimiwa nipende kuishukru siku hii ya leo na Mwenyezi Mungu mpaka kufika hapa na inipende kuishukru Mahakama kwa kutoa uamuzi huu sahihi kwangu japo kuwa inaniuma kwa kuwa  si mtendaji ila niombe Mahakama inipunguzie adhabu”, amesema Issa.

Kwa upande wake Frank aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza aliiomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria, kwamba alionewa na kwamba vielelezo vilivyowasilishwa  mahakamani sivyo vilivyokamatwa eneo la tukio. Pia aliiomba Mahakama izingatie muda waliokaa  mahabusu.

Aliyekuwa mshtakiwa wa pili, Faham kwa upande wake badala ya kuomba kupunguziwa adhabu alianza kutoa utetezi wa kukana makosa yaliyokuwa yakiwakabili, hatua ambayo ilishapita.

“Mheshimiwa  mimi kwa kweli tangu nizaliwe mpaka nifikie umri huu sijui…”, alianza Faham, lakini Hakimu Kaseko akamkatisha kwa kumweleza kuwa anatakiwa kujitetea kuhusu adhabu.

“Kama ndio hivyo mimi sina zaidi ya hapo”, alisema Faham.

“Kwa hiyo huna cha kuongea?” alihoji Hakimu na Fahamu akaitikia, kukubaliana na swali la Hakimu.

Awali mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Deborah Mushi aliieleza Mahakama kuwa upande wa mashtaka haukuwa na kumbukumbu zozote za nyuma za uhalifu wa washtakiwa, lakini akaiomba Mahakama iwape adhabu kali kwa mujibu wa sheria kulinga na madhara ya makosa yao. 

“Mheshimiwa, hatuna kumbukumbu za makosa yao ya nyuma, lakini kama mashahidi walivyotoa ushahidi tunaomba mahakama izingatie madhara yanayotokana na kemikali hiyo hatarishi kwa viungo vya binadamu kama ini, figo na moyo kutanuka na Serikali kutumia gharama kubwa kuwatibu”, amesema wakili Mushi.

Amebainisha madhara mengine kuwa kukwepa mapato kutokana na kitendo cha washtakiwa kutumia nembo za biashara za kampuni nyingine zilizosajiliwa na kupewa leseni kuzalisha bidhaa hizo, jambo lililozikosesha mapato na kuziondolea imani kwa wananchi kwa kuwaharibia bidhaa zao.

“Hivyo kwa kuzingatia uharibifu wa afya za Watanzania washtakiwa wapewe adhabu kali iwe onyo kwa wengine wote wanaofanya makosa kama haya”, amesisitiza Wakili Mushi.

Akitoa adhabu, Hakimu Kaseko amesema kuwa mahakama imezingatia maelezo ya Jamhuri na maombolezo (utetezi wa adhabu) ya washtakiwa.

Hata hivyo,  licha ya utetezi huo Hakimu Kaseko amesema kuwa Mahakama hiyo imezingatia kifungu namba 15(1), (2) na ( 3) cha Sheria ya Udhibiti Dawa za Kulevya, kinachotoa adhabu kwa shtaka la kujihusisha na kemikali hatarishi kwa afya za binadamu kama hiyo ya ethanol.

“Kwa kuwa adhabu pekee kwa mujibu wa kifungu hicho ni kifungo cha gerezani maisha yote, mahakama inafungwa mikono haiwezi kuamua tofauti na hivyo. Hivyo katika shtaka la kwanza washtakiwa wote Mahakama inawahukumu watumikie kifungo. ha maisha gerezani”, amesema Hakimua Kaseko na kuongeza:

“Kwa kosa la pili kila mshtakiwa atalipa faini ya Sh5 milioni na la tatu, kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani”.

Hakimu Kaseko alifafanua kuwa  kwa kuwa adhabu zote zinakwenda pamoja.

Pia Mahakama iliamuru vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa mahakamani walivyokamatwa navyo washtakiwa ikiwemo kemikali hiyo hatarishi, chupa vizibo, stika za TRA na nembo bandia za kampuni viteketezwe.

Vijana hao walitiwa mbaroni Septemba 17, 2022, katika eneo la Uwanja wa Panda, Tegeta, wilayani Kinondoni, baada ya kukutwa na askari wa Kituo cha Polisi Kawe, Wilayani Kinondoni, wakimiliki lita 531.2 za kemikali hiyo katika kiwanda walichokuwa wakitengenezea vileo hivyo.

Walipopandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka hayo katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 10 ya mwaka 2022, washtakiwa wote waliyakana.

Upande wa mashtaka uliita jumla ya mashahidi 12 na kuwasilisha vielelezo 25, zikiwemo nyaraka, hasa maelezo ya onyo ya washtakiwa (walipohojiwa na Polisi) na bidhaa bandia zilizokuwa zikitengenezwa na washtakiwa

Washtakiwa katika utetezi wao walikana kutenda makosa hayo wala kufahamiana.

Hata hivyo katika hukumu yake katika kuwa hatiani washtakiwa, Hakimu Kaseko amesema kuwa  Mahakama pamoja na utetezi wa washtakiwa, imezingatia ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Miongoni mwa mashahidi hao ni shahidi wa kwanza, Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe, Kinondoni Dar es Salaam, Inapekta Omary Wawa, aliyeongoza kikosi cha doria kwenda kuwakamata washtakiwa wengine kiwandani hapo wakiongozwa na mshtakiwa wa kwanza.

Mashahidi wengine ni waliokuwepo eneo la kiwanda hicho bubu, ambamo washtakiwa wengine wawili walikutwa na vifaa na bidhaa hizo zikiwemo stika za TRA ambazo zilikuwa zimetumika kwa kuwekwa kwenye vizibo, akiwemo shahidi wa pili ambaye ni shahidi huru.

Wengine ni shahidi wa sita, ofisa kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali aliyechunguza kemikali na bidhaa hizo walizokutwa nazo washtakiwa (pombe bandia) na shahidi wa 10, mfanyabiashara wa vileo ambaye washtakiwa hao walikuwa wakimpelekea bidhaa hizo.

Pia alizingatia ushahidi wa ofisa kutoka TRA ambaye alithibitisha kuwa stika walizokutwa nazo washtakiwa, zilikuwa za bandia na maofisa kutoka kampuni za kuzalisha vileo hivyo, K-Vant na nyingine waliothibitishia kuwa pombe na nembo walizokuwa wamezimia washtakiwa zilikuwa  bandia.

“Mshtakiwa wa pili katika maelezo yake ya onyo (aliyoyatoa Polisi), alieleza kuwa mshtakiwa wa kwanza ndio alimwajiri. Mahakamani imebaini kuna uhusiano wa moja kwa moja kwa washtakiwa wote maana si rahisi wakati wa usiku wote wawe katika nyumba moja (kiwanda bubu walimokutwa) bila uhusiano wowote”, amesema Hakimu Kasekwa na kusisitiza:

“Mahakama haina shaka kwamba mashtaka yote matatu yamethibitishwa dhidi ya washtakiwa wote licha ya kukana kwao.Hivyo  Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote katika makosa yote matatu.”amesema.

Related Posts