Prof.Mkenda,elimu, ujuzi na ubunifu zinachangia maendeleo kiuchumi na kijamii

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu ni sehemu ya mikakati ya serikali katika kuongeza hamasa ya kukuza elimu ujuzi na ubunifu katika kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mkenda amesema hayo jijini Tanga wakati akifungua Maadhimisho hayo ambapo amesema matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ni nyenzo zinazosaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla.

‘’Serikali inatambua umuhimu na mchango mkubwa wa elimu, ujuzi na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na imepiga hatua katika kuhakikisha maeneo yanatekelezwa kikamilifu kwa kuwa na Mipango na Mikakati mbalimbali ya Kitaifa ikiwemo Dira ya Taifa 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023; Ajenda 2063: The Africa We Want; Malengo ya Maendeleo Endelevu-2030, ambayo inaonesha utekelezaji wske kupitia rasimali yenye naarifa na ujuzi, “alieleza Waziri Mkenda.

Aidha amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, sambamba na kuanza utekelezaji wa Sera ya elimu na mitaala iliyoboreshwa pamoja na kuendelea ujuzi na ubunifu.

Amesema azma kuu ya mageuzi ni kujenga ujuzi na umahiri na kuongeza kuwa katika mitaala iliyoboreshwa Elimu ya Amali imemepewa mkazo.

” tumeanza shule 96 zenye kibali cha kuendesha elimu ya amali , tunajenga shule 100 mpya za amali ufundi pamoja na mikakati mingine ikiwemo mikopo kwa wanafunzi ngazi ya Diploma na Shahada bila kusahau kuibua kuendeleza na kubuasharisha bunifu na teknolojia za ndani “, amesema Mkenda.

Waziri Mkenda amesema wabunifu Nchini wasisite kufika katika Wizara na taasisi hususan COSTECH ili bunifu zao ziendelezwe.
” kumekuwa na hisia kuwa wabunifu hawaendelezwi , hapana ziko bunifu zaidi ya 40 ambazo zimeendelezwa na sasa ni bidhaa ziko sokoni”, ameongeza Mkenda

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Elimu, Michezo na Utamaduni Mhe. Husna Sekiboko amesema Bunge la Tanzania linatamani kuona bunifu zinazoibuliwa hazibaki kwenye Maonesho, badala yake ziendelezwe na kufikia hatua ya kubiasharishwa ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kutoa hamasa kwa Wabunifu mbalimbali.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Dkt. Baltida Burian ameshukuru kuufanya mkoa huo Mwenyeji wa Maadhimisho na kwamba ni heshima kubwa kwa Wanatanga wote na kuwataka kutumia fursa hiyo kikamilifu kutembelea maonesho hayo kujifunza juu ya teknolojia mbalimbali.

Related Posts