KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameipa timu hiyo mtihani mzito baada ya kupokea ofa kutoka timu tatu tofauti.
Gamondi aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja kuinoa timu hiyo akichukua mikoba ya Nasreddine Nabi aliyejiunga na FAR Rabat ya Morocco, kwa asilimia 80 ametimiza malengo aliyokuwa amepewa kabla ya kusaini mkataba ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kocha huyo alitakiwa kuipa ubingwa wa ligi, kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ambako alivuka hadi robo fainali na kutetea Kombe la Shirikisho ambalo anatarajia kucheza fainali Juni 2 dhidi ya Azam FC.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa timu hiyo imempa ofa Gamondi ya kuendelea kusalia Yanga na tayari amepokea ofa nyingine kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, USM Alger ya Algeria na Simba ya Dar es Salaam.
“Ni kweli mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na sisi tayari tumempa ofa yetu ambayo bado hajatupa majibu kama yupo tayari au la, kinachozingatiwa sasa ni mchezo wa fainali ulio mbele yetu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Ofa yetu tuliyompa ni mara mbili ya tuliyompa msimu uliopita na nina imani kama mambo yatakwenda kama tulivyopanga tutaendelea naye kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Wakati Yanga ikifanya hivyo pia Mwanaspoti limezinasa za ndani kutoka Simba kuwa wababe hao wa Msimbazi pia wametuma ofa kama ya watani wao jambo ambalo linawapa ugumu kumnasa kocha huyo kwani kwa mujibu wa chanzo chetu timu anayoipa kipaumbele kwa Tanzania ni waajiri wake.
Mbali na ofa hizo pia inaelezwa kuwa Kaizer Chiefs wamewekeza nguvu zaidi kuinasa saini ya kocha huyo wakiwa na mpango wa kuona anaitengeneza timu yao na kuirudisha kwenye ushindani.
“Ni kweli kuna ofa hizo lakini Kaizer Chiefs na USM Alger wameingilia kati dili letu kwa kutaja ofa kubwa zaidi sipendi kuzungumza mengi zaidi kwa sasa kwani nguvu zetu tumewekeza kwenye fainali na mechi mmoja ya ligi iliyobaki,” kimesema.
“Mazungumzo kati yetu na Gamondi sio mabaya lolote linaweza kutokea muhimu sasa tunamsikiliza yeye kwa sababu katuomba tumuache atimize makujukumu yake na amekiri kuwa na furaha ndani ya timu yetu.”
Mwanaspoti lilipomtafuta Gamondi ili aweze kuzungumzia suala la mkataba wake ndani ya Yanga amesema bado ni mwajiriwa wa timu hiyo na anazingatia majukumu yake kwasasa aache akamilishe kazi.
“Mimi ni mwajiriwa wa Yanga na ndio maana mnaniona na timu na nafanya majukumu yangu kama inavyotakiwa. Nina furaha nimeweza kutwaa taji la ligi sasa nawekeza nguvu kwenye mchezo wa mwisho na fainali ya Kombe la Shirikisho (FA). Nina matumaini ya kutetea taji hilo kutokana na kikosi imara nilicho nacho,” amesema Gamondi.