KAMATI ya mpito ya Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imesitisha pambano la kimataifa kati ya Mtanzania, Hassan Mwakinyo dhidi ya Mghana, Patrick Allotey kufuatia promota wa pambano hilo, Shomari Kimbau wa Golden Boy Promotion kushindwa kutimizi vigezo na matakwa ya kimikataba.
Pambano hilo lilipangwa kufanyika Ijumaa ya wiki hii jijini Dar es Salaam kwa mabondia hao kuwania Mkanda wa Ubingwa wa WBO Afrika uzani wa middle.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya mpito, Alex Galinoma alisema sababu ya kutoidhinisha kuwepo kwa mtanange huo ni kutokana na promota wa pambano hilo, Shomari Kimbau kushindwa kuwasilisha mikataba kamili ya mabondia, rekodi za matibabu na vibali vya tukio.
“Tulikaa na promota zaidi ya mara mbili, lakini amekuwa akitoa ahadi feki bila kutimiza mambo ambayo alipaswa afanye ikiwemo malipo ya mabondia na kushindwa kupata ukumbi unaofaa kwa tukio ndani ya muda tuliokubaliana au kuwasilisha nakala za upatikanaji wa ukumbi,” alisema Galinoma.
Galinoma alisema mabondia wanaposhuka ulingoni wanatakiwa kupata fedha zao ndiyo maana wao TPBRC wanapambana kuhakikisha mchezo huo unakuwa na maendeleo.
“Tulikaa na mabondia ambao wanacheza katika pambano la Mwakinyo wengi wao tumegundua hawana elimu ya mikataba yao, wengine walisema walitakiwa kucheza bila malipo,” alisema Galinoma.
Alisema endapo promota atawasilisha mikataba hiyo kwa wakati basi pambano hilo litafanyika bila tatizo lolote na wadau wa mchezo huo kupata burudani.