Ubungo na matumaini kibao Umitashumta

LICHA ya Wilaya ya Ubungo kuanza vibaya baadhi ya michezo ikiwemo mpira wa mikono (handball) kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta), makocha wa timu hizo wamepanga kupindua meza katika michezo inayofuata.

Ubungo  waliopewa vifaa vya michezo na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na La Liga, walianza kwa kupoteza kwenye Uwanja wa Jitegemee kwa wanaume kwa mabao 11-3 dhidi ya Temeke na wanawake kwa mabao 5-2.

Akizungumzia mwanzo huo, kocha wa upande wa wanawake katika mchezo wa mpira wa mikono, Mwanaulu Boga alisema vijana wake walipoteana tu katika michezo miwili waliyocheza katika siku ya ufunguzi lakini anaamini wanaweza kujirekebisha makosa yao na kufanya vizuri.

“Ilikuwa siku ngumu kwa sababu mechi yetu ya kwanza tulifungwa na Temeke kwa mabao 5-2, tukacheza tena dhidi ya Kigamboni wakatufunga mabao 6-5, sio kwamba tulikuwa na maandalizi mabaya hapana ila imetokea tu vijana wetu wamepoteana ila tunanafasi bado ya kufanya vizuri,” alisema kocha huyo.

Kwa upande wa kocha wa timu ya mpira wa miguu kwa wanaume ambao walifungwa mabao 2-1 dhidi ya Kigamboni na wasichana ambao walishinda kwa bao 1-0, Reuben Kusaka Juma alisema,”Tulianza vizuri kwa wanawake ila kwa wanaume  mambo yalienda tofauti kwa kufungwa ila tunajinga kwa mechi nyingine.”

Hekaheka za Umitashumta zitaendelea tena leo, Jumatano na kesho, Alhamisi kabla ya kutangazwa mabingwa wa mkoa katika michezo tofauti huku wachezaji 120 ambao walifanya vizuri wakichanguliwa kwa ajili ya kuunda timu ya mkoa.

Baada ya ngazi ya mkoa kumalizika michuano hiyo itachukua sura nyingine ambapo itakuwa katika ngazi ya taifa kila mkoa utakuwa vitani katika michezo tofauti kwa ajili ya kuusaka ubingwa wa Tanzania.

Related Posts