Unguja. Upatikanaji wa fedha kidogo katika Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo umetajwa kuwa sababu ya wizara kushindwa kutekeleza miradi iliyoidhinishiwa fedha katika bajeti ya mwaka 2023/24.
Kutokana na hilo, Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii imeitaka Serikali kuhakikisha inatoa fedha zinazopangwa kuiwezesha wizara kutekeleza majukumu yake.
Katika Bajeti ya mwaka 2023/24 Wizara hiyo iliidhinishiwa Sh98.716 bilioni na hadi Machi, mwaka huu imepata Sh47.694 bilioni sawa na asilimia 48.31 ya fedha zilizoidhinishwa.
Akisoma maoni ya kamati wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumzi ya Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25, Mei 28, 2025, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mtumwa Peya Yussuf amesema kwa utaratibu huo wizara haiwezi kupiga hatua, kwani mipango itabaki katika makaratasi.
“Wizara ya Kilimo inashindwa kutekeleza baadhi ya miradi iliyopangwa kwa wakati kutokana na Wizara ya Fedha kushindwa kuwaingizia fedha hizo kama zilivyoidhinishwa kupitia Baraza,” amesema.
Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Wizara ilipanga kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo ya ujenzi wa machinjio ya Kisakasaka, karantini ya wanyama Kisakasaka, na josho la wanyama –Donge.
“Zilipangwa Sh5 bilioni kutumika kwa utekelezaji wa miradi hiyo katika mwaka wa fedha 2023/24 lakini cha kusikitisha, fedha hiyo haikuingia hata robo yake. Kwa mwaka huu wa fedha tunaoumalizia bado miradi hii inasuasua kwa vile haijaingiziwa fedha,” amesema.
Kamati inaishauri Serikali kuangalia umuhimu wa miradi hiyo kwa maendeleo ya Taifa.
Vipaumbele vya wizara 2024/25
Wizara imeweka vipaumbele vinane ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za kilimo, maliasili na mifugo, kwa kujenga vituo vya huduma za kilimo kwenye wilaya.
Pia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, yakiwamo ya ndizi, mpunga, mboga na matunda na uzalishaji wa asali kwa kufanya tafiti, utaalamu na kusambaza teknolojia kwa wakulima.
Akisoma hotuba, Waziri wa wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis amesema wataendeleza utoaji wa huduma za ukulima na zana za kilimo kwa wakulima, Pia kuhamasisha sekta binafsi.
“Kuimarisha upandaji miti kwa kuotesha miche 1.7 milioni ya misitu, mikarafuu, minazi, matunda na viungo na kutathmini hali ya uhuishaji wa miti iliyopandwa, kuimarisha usimamizi wa misitu na kuendeleza uwekezaji wa miradi yenye tija katika hifadhi za misitu,” amesema.
Waziri amesema wamepanga kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea hifadhi kutoka 64,000 hadi kufikia 100,000 kwa kuimarisha vivutio na kuhamasisha miradi ya uwekezaji katika maeneo ya hifadhi za misitu.
Pia wanatarajia kuotesha miche milioni moja, kati ya hiyo 800,000 ni ya misitu na 200,000 ya matunda na viungo na kuhamasisha na kupanda miti hekta 130.
Waziri Shamata amesema wataongeza uzalishaji wa asali na mazao mengine ya nyuki kutoka tani 13 kufikia tani 17.
Pia kufanya utafiti kubaini idadi, aina na hali ya wanyamapori kwa lengo la kuandaa mpango wa kuwanusuru waliohatarini kutoweka.
Amesema watalii 55,870 walitembelea hifadhi na kuingiza mapato ya Sh1.06 bilioni na Dola za Marekani 43,419.
Amesema wizara inalenga kupandisha ng’ombe 2,000 kwa njia ya sindano, kupanda eka 10 za malisho katika shamba la malisho Kizimbani kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa mbegu za majani ya malisho ya mifugo na kuwapatia wafugaji 1,000 waoteshe katika mashamba yao kwa ajili ya kulisha mifugo.
“Wizara itachunguza sampuli 1,500 za maradhi ya mifugo na uanzishaji wa mfumo wa kielektroniki wa ufutiliaji wa magonjwa ya mifugo,” alisema
Waziri Shamata amesema wanatarajia kuotesha miche 700,000 (400,000 mikarafuu na 300,000 miti ya matunda na viungo) na kuigawa bure kwa wakulima, kuimarisha uwepo wa uhakika wa chakula na uzalishaji mbegu za mpunga.
Amesema mapitio ya Sera ya Kilimo ya mwaka 2002 yamekamilika na yamewasilishwa kwa kamati ya makatibu wakuu kwa mapitio na baadaye kupelekwa kikao cha Baraza la Mapinduzi.
Waziri amesema mapitio ya sera ya misitu ya mwaka 1995, na mapitio ya Sheria ya udhibiti wa mimea yanaendelea kwa hatua za uandishi wa waraka kupelekwa kwa makatibu wakuu.
Kuhusu mpango wa mageuzi ya sekta ya kilimo, amesema umepitiwa na kuwasilishwa kwa wadau Unguja na Pemba na sasa upo katika hatua za kujumuisha maoni.
Wizara imeombwa kuidhinishiwa Sh128.108 bilioni kati ya hizo Sh23.423 bilioni ni kwa ajili ya kazi za kawaida Sh19.134 bilioni ni mishahara na Sh4.289 bilioni kwa matumizi mengineyo.
Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema wizara hiyo imekuwa na miakati mizuri lakini hakuna utekelzaji.
“Kuna hili suala la umwagiliaji, bado wananchi hawajaona matokeo yake bado ipo haja kuhakikisha tunawaondolea wananchi changamoto za kilimo,” amesema.