WANANCHI wa vitongoji vilivyopo kijiji cha Ngwala wilayani Songwe mkoani hapa, wamemuomba mkuu wa mkoa huo, Danie Chongolo kukwamua mradi wa maji ambao umegharimu fedha zaidi ya Sh 300 milioni. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Wananchi hao wameyasema hayo leo tarehe 28 Mei 2024 katika mkutano wa hadhara uliongozwa na mkuu wa mkoa kwenye kijiji cha Ngwala na kusikiliza kero mbalimbali.
Anastazia Staford mkazi wa Ngwala amesema kwa muda mrefu kijiji hicho kina ukosefu wa maji safi na salama.
Amesema walipeleka malalamiko na maombi ofisi za mkurugenzi kupitia diwani wao ili wapatiwe mradi wa maji ili waondokane na kadhia hiyo.
Amesema baada ya ombi lao kukubaliwa walipata taarifa kutoka kwa diwani wao kuwa zimetolewa Sh 300 milioni kujenga mradi huo na muda mfupi ulianza kujengwa lakini wanashangaa kuona mradi umetelekezwa na tenki limepasuka.
Akijibu madai hayo, Meneja wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Songwe, Boniface Mfungo amesema ni kweli mradi umekwama lakini umetokana na ubabaishaji wa mkandarasi ambaye walivunja naye mkataba mradi ukiwa umefikia asilimia 45.
Amesema walipokea Sh 300.7 milioni kujenga mradi huo, lakini baada ya migongano ya hapa na pale waliamua kusitisha mkataba na mkandarasi huyo na hivi sasa wanatarajiwa kutangaza zabuni upya kumpata mkandarasi atakayekamilisha mradi huo.
Aidha, Mkuu wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo mbali na kusikitishwa na kukwama kwa mradi huo, ameiagiza RUWASA kuukamilisha wenyewe kwa kutumia ‘Force Akaunt’ ili ukamilike haraka na wananchi wapate maji.
“Mkuu wa wilaya upo hapa hakikisha unatembelea mara kwa mara hapa kusimamia mradi ukamilike haraka na kwa viwango, kwani Rais Samia kaleta fedha nyingi kutatua kero za wananchi, kitendo cha kukwama mradi unaumiza wananchi,’’ amesema Chongolo.