SOKO KULIINGIZIA JIJI MAPATO BILIONI 3.5 KWA MWAKA



Mmoja wa wahandisi wa kampuni ya United Bulders (katikati),inayojenga soko la Jiji la Mwanza,leo akiwaelekeza wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza ilipokagua ujenzi wa soko hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (wa pili kushoto) akiingoza Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza,kukagua soko la kimkakati la Jiji la Mwanza,leo.


Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mwanza, wakitoka kukagua mradi wa soko la kimkakati leo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ akizungumza na wananchi baada ya kukagua mradi wa soko la Jiji la Mwanza.

NA BALTAZAR MASHAKA,NYAMAGANA
SERIKALI imeagizwa kuharakisha malipo ya mkandarasi wa mradi wa kimkakati wa soko la Jiji la Mwanza likamilike wananchi wapate huduma na halmashauri ipate mapato.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja “Smart’,baada ya Kamati ya Siasa kukagua mradi huo unaogharimu zaidi ya sh.bilioni 23.37.

Amesema kuchelewa kukamilika kwa soko hilo kutasababisha mapato ya Jiji kuwa chini,ukikamilika watakusanya sh.bilioni 3.5 kwa mwaka,hivyo serikali iharakishe malipo ya mkandarasi na fedha zikiletwa zisimamiwe ukamilike kwa kumalizia kazi iliyobaki ulete manufaa na tija kwa wananchi.

“Rais Dk.Samia anastahili pongezi kwa fedha sh.bilioni 23 za ujenzi wa soko hili la kimkakati ambalo litachochea uchumi wa Jiji la Mwanza,Mkoa na taifa kwa mapato na hivyo kuuendelea kuchelewa ni kukosa mapato tunayoyahitaji kwa maendeleo,nina uhakika kwa miaka tutarejesha fedha iliyotumika,”amesema Smart.

Kamati hiyo iliagiza uongozi wa Jiji wakati wa kugawa maeneo ya kufanyia biashara wawape kipaumbele zaidi wafanyabiashara waliokuwa katika soko ila awali kabla ya kuvunjwa na kujengwa jipya.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Jiji,Erick Mvati amesema mradi huo unaogharimu sh.bilioni 23.367 utaongeza mapato ya halmashauri na kupunguza utegemezi wa serikali kuu ukikamilika kwa mwakautaingiza bilioni 3.5.

Amesema mradi ambao umefikia asilimia 94.5 umesimama kutokana na malipo ya mkandarasi kuchelewa zaidi ya sh.bilioni 3.6 ambapo ameshalipwa bilioni 18.9 za kazi alizofanya.

Kwa mujibu wa Mvati soko hilo litapunguza msongamano wa machinga barabarani,litakuwa na maduka makubwa na madogo, vizimba vya wafanyabiashara,mama lishe,maegesho ya magari, vibanda vya matunda na nafaka.

Naibu Meya wa Jiji,Bhiku Kotecha alisema wanamshukuru Rais Dk.Samia kwamradi huo wenye manufaa makubwa kwa jamii na kuahidi kuusimamia kwa weledi wananchi wafaidi matunda ya kodi zao.

Pia Kamati hiyo ya Siasa ilikagua na kuridhishwa na upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza kaskazini ukiwemo ujenzi wa jengo la abiria na mizigo.

“Tunampongeza Dk.Samia kwa mradi huu mkubwa wa maegesho ya meli ya MV Mwanza,aliposema Kazi Iendelee kweli kazi inaendelea,tumeridhika na hatuna shaka mradi utatekelezwa kwa viwango,”amesema Smart.

Kaimu Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa,Fransisco Mwanga, amesema mradi huo unagharimu sh.bilioni 18.6 ukiwemo uboreshaji wa mto Mirongo,watahakikisha inakamilika kwa wakati na wamejipanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kuzingati Dira ya Taifa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Related Posts