Katavi. Wakazi wa Kijiji cha Kapanga katika Wilayani Tanganyika mkoani Katavi, wamesema biashara ya hewa ukaa inayoendelea kutekelezwa kiwilaya, inazidi kuwanufaisha baada ya fedha zake kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo
Wilaya hiyo ni miongoni mwa zinazonufaika na utunzaji wa mazingira kwa kufanya biashara ya hewa ukaa, na kwa mwaka inapata zaidi ya Sh14 bilioni zinazosaidia kutekeleza miradi ikiwamo ya ujenzi wa vito vya afya na zahanati.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 28, 2024 wakati wa ziara ya Waziri Jafo aliyetembelea kijijini hapo, Abdallah Gabona Mkazi wa Kijiji cha Kapanga amesema biashara hiyo fedha zake zinasaidia kutekeleza miradi waliyojipangia.
Anasema tayari wameshanufaika na upanuzi wa shule ya msingi ilyopo kijijini hapo, ambayo madarasa yake yamejengwa kwa fedha ya hewa ukaa.
“Ukiangalia shule yetu ya msingi ilikuwa na wanafunzi wengi walikuwa hawatoshi kukaa madarasani, lakini sasa tumeongeza madarasa mengine mawili na madawati yaliyonunuliwa kwa fedha hizi, mbanano sasa haupo, na wanafunzi hawabanani tena darasani wanasoma vizuri,” amesema Gabona.
Amesema mbali ya ujenzi wa madarasa, lakini pia fedha hizo zimetumika kutengeneza zahanati ya kijiji na sasa wanatekeleza mradi wa maji.
“Sasa hivi tunakunywa maji safi kabisa, huu mradi ni mzuri uongozi wa vijiji unabidi uusimamie sana,” amesema Mary Mwashiuya.
Awali, akizungumza kijijini hapo alipofika kukagua mradi wa ujenzi wa zahanati iliyojengwa kwa fedha za hewa ukaa leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Suleiman Jafo, amesema kutokana na utunzaji mzuri wa mazingira ndiyo maana wilaya ya Tanganyika inapata fedha hizo.
Waziri huyo amewapongeza wananchi wa kijiji hicho huku akisema ni mfano wa kuigwa katika maeneo mengine nchini.
“Nimefurahi sana kufika katika kijiji hiki cha Kapanga hasa kwenye zahanati hii ambayo imejengwa na wananchi kupitia fedha zilizopatikana kutokana na biashara ya hewa ukaa, hili ni jambo la kuingwa na ni maamuzi sahihi katika kutumia rasilimali mlizonazo kujiletea maendeleo. Zahanati hii inaondoa kero kwa wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya,” amesema Jafo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema katika vijiji vinane vinavyozungukwa na mradi wa biashara hiyo tayari vimenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imeondoa kero kwa wananchi.
“Malengo ya Mkoa wa Katavi ni biashara hii iwanufaishe wananchi, tumeanza na ujenzi wa miradi ya afya, elimu, maji na mingine, baadaye tuna malengo ya biashara hii iwanufaishe wananchi moja kwa moja,” amesema.